Friday, January 6, 2017

WAZIRI MKUU AONYA VITA YA MADIWANI NA WATUMISHI

*Ataka Wakuu wa Idara watoe ushauri wa kitaalamu bila woga   

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Idara kwenye Halmashauri za Wilaya na Manispaa wasaidie kutoa utaalamu badala ya kupingana na madiwani ili wawezeshe kuleta maendeleo kwa wananchi.

Pia amewataka madiwani wasikilize ushauri wa kitaalamu unaotolewa na Wakuu wa Idara katika utekelezaji wa miradi iliyotengwa na Halmashauri.

Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Januari 5, 2017) wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mabada na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani humo.

“Wakuu wa Idara nyie ni washauri. Tumieni taaluma zenu kutoa ushauri, semeni bila woga pale inapodidi. Ninawasihi waheshimiwa madiwani wasitumie fursa yao ya ‘kuazimia’ pale inapotokea kuna watumishi wenye msimamo,” amesema.

Akizungumzia kuhsu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu amesema Serikali iko makini kwenye matumizi kwa kila senti inayokusanywa na akawataka watumishi hao kila mmoja aongeze mapato ya Serikali kupitia sekta aliyopo. Pia amepiga marufuku matumizi holela ya fedha za umma.

“Kuanzia leo, marufuku kwa fedha iliyokusanya kwa mapato ya ndani kutumika bila utaratibu. Serikali hii haina mzaha na miradi inayotekelezwa chini ya viwango. Mtumishi ukiharibu hapa Madaba, usidhani utahamishwa, tunamalizana na wewe hapahapa. Wala usiombe ndugu yako akuombee uhamisho, tutakufuata hukohuko,” amesisitiza.

Amewataka watumishi wa umma wote watumie Ilani ya Chaguzi ya CCM katika kutekeleza majukumu kwani inaeleza kila kitu ambacho Serikali inatakiwa kukifanya katika kipindi ca miaka mitano.

“Zaidi ya hayo, ninawasihi kila Mkurugenzi atoe nakala ya hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa Novemba 20, 2015 wakati akizindua Bunge la 11, awape watendaji wake waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwani ilitoa dira ya nini anataka kufanya katika Serikali hii,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi na imeanza kulipa madeni yaliyokuwa yamelimbikizwa. “Serikali imedhamiria kupunguza madeni ya watumishi na hadi kufikia Novemba 30, 2015 jumala ya sh. bilioni 28.9 zilikuwa zimekwishlipwa kwa watumishi 31,032 wenye madai katika sekta mbalimbali. Zoezi hili linaendelea.”

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa wilaya hiyo wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali dini, itikadi, kabila au hali zao na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.

Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu amesema Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.

"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo, " amesema.
Read More

Thursday, January 5, 2017

WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI WA HALMASHAURI YA MADABA WILAYA YA SONGEA KULINDA VYANZO VYA MAJI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo ya mradi wa maji  kutoka kwa mkurugenzi wa Halimashauri ya  Madaba Bwana Safi Mpenda,Waziri Mkuu amezindua mradi huo ambao umejengwa katika kijiji cha Magingi wilaya ya Songea leo 05 Desemba,2017  mradi ambao unauwezo wa kutoa lita 200,000(laki mbili) na kuhudumia zaidi ya watu  5,000(Elfu tano) 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimtwisha ndoo ya majai Bibi Leonara Kibuno ikiwa ni ishara ya uzinduzi  wa mradi huo ambao umejengwa katika kijiji cha Magingi wilaya ya Songea  mradi ambao unauwezo kutoa lita 200,000 (laki mbili) na kuhudumia zaidi ya watu 5,000(Elfu tano) katika Halimashauri ya madaba Songea.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akiwa hutubia wananchi wa halimashauri ya Madaba leo Desemba 5,2017.

Read More

WAZIRI MKUU AKAGUA GHALA LA NFRA SONGEA

*Aagiza akiba iliyopo itunzwe hadi msimu ujao wa mavuno
* RC, Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.

“Angalieni ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”

“Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,” alisisitiza.

“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.

Alisema kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.

“Kanda ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.

“Kanda ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu utakapokamilika.”

Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.

Alipolizwa ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila mwaka).

“Kuimarika kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. “Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.


Waziri Mkuu leo anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.
Read More

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KUMZIKA KAPTENI MHAIKI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wakazi wa mji wa Songea na kata ya Matogoro kuuaga mwili wa aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan Mhaiki katika ibada iliyofanyika kwenye parokia ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu iliyoko Matogoro, mjini Songea.

Waziri Mkuu ambaye ameshiriki msiba huo kwa niaba ya Serikali, pia alishiriki mazishi ya Kapteni Mhaiki ambaye pia alikuwa rubani wa ndege za Serikali yaliyofanyika kwenye makaburi ya parokia ya Matogoro.

Akizungumza kwenye ibada ya mazishi mara baada ya kutoa heshima za mwisho, leo jioni (Jumatano, Januari 4, 2017), Waziri Mkuu aliwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.

“Msiba huu ni wetu sote na umetugusa wote. Ni msiba mzito kwa wanafamilia na kwa Serikali pia. Kapteni Mhaiki amekuwa rubani wa ndege za Serikali kwa muda mrefu na amewaendesha viongozi wa kitaifa kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu ya tano. Kwa niaba ya Serikali tunawapa pole sana,” amesema.

“Ninawaomba wafiwa wote hasa mke wa marehemu na watoto tushikamane katika kipindi hiki na tuendelee kuwa wavumilivu huku tukimuombea Baba yetu apate pumziko la milele,” amesema.


Kapteni Mhaiki alifariki dunia Desemba 31, 2016 katika hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam. Alilazwa katika hospitali hiyo, kabla ya sikukuu ya Krismasi, kwa ugonjwa wa saratani ya ini.
Read More

WAZIRI MKUU: MADIWANI WASIPEWE FEDHA ZA MAENDELEO MKONONI

*Asema kama tabia hiyo ilikuwepo, mwisho wake ni jana

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini kuacha kutoa fedha taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.

Badala yake amewataka waandae mfumo maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za mfuko wa Jimbo ambazo ni maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za maendeleo jimboni.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo Manispaa ya Songea.

“Nimepata taarifa kuwa fedha za maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana. Msiwape fedha mkononi, bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na matumizi ya aina hiyo, mwisho wake ni jana,” amesisitiza.

“Fedha za mfuko wa Jimbo ni za Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri na yeye anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni miradi ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa imekwishaidhinishwa na vikao husika,” ameongeza.

Alisema makusanyo ya fedha yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha hizo zinavyotumiwa. “Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila diwani. Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo,” amesisitiza.

Amesema kuna baadhi ya watu wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia kutumia fedha hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building). “Hii si sahihi na jana nimepiga marufuku posho za aina hii pamoja na fedha za vitafunwa kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na waliozikusanya hawapati chochote,” ameongeza.

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu amewataka waangalie baadhi ya makampuni ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini wanatumia software ambazo zinawanufaisha na wao pia.

“Tumieni watu wenu wa TEHAMA kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile mashine siyo waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna mianya ya wizi. Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia kwenye akaunti za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu wanayoijua wao. Ukiangalia unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia unaibiwa. Jaribuni kuchunguza na mjiridhishe na hizo software zao,” amesisitiza.


Read More

Wednesday, January 4, 2017

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWASILI MKOANI RUVUMA KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkuu wa mkoa wa ruvuma Mhandisi Binilis Mahenge mara alipowasili katika uwanja wa ndege wa Ruvuma kwa ziara ya kikazi kulia ni mke wa mkuu wa mkoa wa ruvuma Mama Mahenge.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Songea Mh Salima Chikoyo ambaye alikuwepo katika uwanja wa ndege wa Ruvuma katika mapokezi ya waziri mkuu Kushoto ni Naibu waziri wa maliasili na utali Mhandisi Ramo Makani na kushoto ni katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassani Bndeheko
Waziri mkuu amewasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Songea Mh Salima Chikoyo ambaye alikuwepo katika uwanja wa ndege wa Ruvuma katika mapokezi ya waziri mkuu Kushoto ni Naibu waziri wa maliasili na utali Mhandisi Ramo Makani na kushoto ni katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassani Bndeheko
Waziri mkuu amewasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi .

Read More

MAJALIWA AKAGUA MAGAHALA YA NFRA CHANG'OMBE DAR

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mhahindi wakati alipotembelea magahala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) , Chang'ombe jijini Dar es salaam Januari  4, 2017.  Kulia kwake ni  Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Deusdedit Mpazi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mhahindi wakati alipotembelea magahala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) , Chang'ombe jijini Dar es salaam Januari  4, 2017.  Kulia kwake ni  Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Deusdedit Mpazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Deusdedit Mpazi wakati alipotembelea  maghala ya NFRA, Chang'ombe jijini Dar es salaam Januari 4, 2017.

Read More

ZIARA YA MAJALIWA KIGAMBONI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kitanda wakati alipotembelea wodi ya wazazi iliyojengwa na kampuni ya mafuta ya OILCOM katika  ENEO la  Kisarawe Two wilayani Kigamboni, Januari 4, 2017. Kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa.
Wananchi wa eneo la Kisarawe Two wilayani Kigamboni wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao baada ya kukagua wodi ya wazazi iliyojengwa na kampuni ya mafuta ya OILCOM kijijini hapo. Waziri Mkuu alikuwa katika ziara ya wilaya hiyo Januari 4, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngombe wa kisasa wakati alipotembelea  shamba la ng'ombe wa maziwa  la MILKCOM  TANZANIA LIMITED  lililopo Kigamboni  jijini Dar es salaam. Alikuwa katika ziara ya wilaya ya Kigamboni Januari 4, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngombe wa kisasa wakati alipotembelea  shamba la ng'ombe wa maziwa  la MILKCOM  TANZANIA LIMITED  lililopo Kigamboni  jijini Dar es salaam. Alikuwa katika ziara ya wilaya ya Kigamboni Januari 4, 2017.

Read More

WAZIRI MKUU AAGIZA UMEME WA UHAKIKA KISARAWE 2

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la Kisarawe ii linakuwa na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati hiyo.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Januari 3, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe ii wilayani Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema.

Waziri Mkuu alisema amefarijika na jitihada za muwekezaji huyo za kuungamkono mkakati wa Serikali ya awamu ya Tano wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda utakaoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo, Aboubakar Faraj akisoma taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linasababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.

“Punde umeme unapokatika tunalazimika kutumia majenereta kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji ambazo huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema.

Faraji alisema changamoto nyingine ni miundombinu ya barabara ambayo usababisha wateja wengi kushindwa kufika kwenye viwanda hivyo kwa urahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hilo.

Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2018.

Mapema Waziri Mkuu alizindua wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe ii iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu itawapunguzia akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata huduma hiyo.

Read More

SERIKALI YAFUTA POSHO ZA VITAFUNWA, MAZINGIRA MAGUMU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Ametia agizo hilo leo (Jumanne, Januari 3, 20017) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Kuanzia sasa marufuku Wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.

Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na Halmashauri na Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa kwenye miradi na shughuli za maendeleo.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Katika halmashauri zetu kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato hadi walinzi, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya leo  atakuwa amejifukuzisha kazi.

Aidha, ameagiza fedha zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala yake  zipelekwe kwenye kata husika na zifuatiliwe matumizi yake.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa kwenye halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Pia amewataka watumishi wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri hiyo ambao wamehamishiwa kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika Manispaa hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu yao.
Read More

MAJALIWA AKIZUNGUMZA NA WATUMISHI WA MANISPAA YA KIGAMBONI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Kigamboni baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es salaam akiwa katika ziara ya wilaya ya Kigamboni  Januari 3, 2017.

Read More

Tuesday, January 3, 2017

WAZIRI MKUU AKEMEA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

*Aonya wanaokata miti ovyo, asisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya wakazi wa Ruangwa wanaokata miti kwenye misitu waache kufanya hivyo mara moja ili kuokoa ardhi chepechepe waliyokuwa nayo.

Amesema ukataji miti huo unafanywa zaidi na watu wanaoanzisha mashamba ya ufuta na wapo walioamua kulima karibu na vyanzo vya maji hali iliyosababisha maji ya kauke kwenye maeneo mengi.

“Zamani kuna maeneo ulikuwa haupiti hadi ukunje suruali, na kama una gari napo pia ilikuwa ni taabu kupita kwenye maeneo hayo. Lakini sasa hivi, hakuna tena maeneo hayo ndiyo maana kila unakopita unakuta akinamama wanatembea mwendo mrefu na ndoo huku vijana wakibeba madumu kwenye baiskeli nao wakitafuta maji,” alisema Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa.

Ametoa onyo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa vijiji mbalimbali vya  wilaya hiyo ambao walifika Ruangwa mjini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM kusikiliza taarifa ya mambo aliyoyafanya jimboni humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

“Kilimo cha ufuta kimekuwa balaa, sasa hivi hakuna maji sababu ya ukataji miti ovyo. Mfano mzuri ni mto Mbwemkuru ambao ulikuwa ukitiririsha maji mwaka mzima, angalia sasa hivi, umegeuka kuwa mto wa msimu na chanzo ni ukataji wa miti,” alisisitiza.

“Tusipobadilika na kuacha hiyo tabia tutamlaumu mbunge na Serikali kuwa hawaleti maji wakati sisi wenyewe tumechangia hali hiyo kwa kuharibu vyanzo vya maji,” alionya na kuongeza kuwa amelazimika kutafuta mashine ya kuchimba maji ili kupunguza tatizo la maji.

Alisema mapema mwaka huu, wataalamu wataanza kufanya utafiti ili kubaini maji yako umbali gani kwenda ardhini kabla ya kuanza kuchimba visima hivyo. “Ikibidi tutaaza na visima vifupi na vya kati ili maji yapatikane haraka,” alisema.

Akielezea mipango ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi wa jimbo hilo kwamba anatamani kuona kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa vijijini.

“Kila nilikopita vijijini nimewahamasisha wananchi waanze kufyatua mafotali ili ujenzi wa boma ya zahanati uanze. Na mimi nimeahidi kuchangia mabati kwa kila zahanati, na kuna baadhi ya maeneo nimechangia hata mabati ya nyumba ya mganga na muuguzi,” alisema.

Alisema mwaka uliopita, alifanikiwa kukamilisha ujenzi wa wodi ya akinababa, ya akinamama na kukarabati wodi ya magonjwa mchanganyiko katika hospitali ya wilaya ambapo fedha taslimu milioni 100 zilitumika. Pia aliwezesha kufunga umeme wa jua kwenye zahanati zote zinazotoa huduma za afya ndani ya jimbo na kazi hiyo itaendelea kwa awamu ya pili.

“Pia niliweza kulipia kaya 10 zisizokuwa na uwezo kwa kila kijiji ili zijiunge na mfuko wa afya ya Jamii (CHF) kwa gharama za shilingi milioni 9. Jumla ya vijiji 92 vimefikiwa. Ninawasihi wana-Ruangwa kila mmoja ajiunge na mfuko huu ili muweze kupatiwa huduma za afya bila matatizo,” aliongeza.

Akielezea kuhusu sekta ya elimu, Waziri Mkuu alisema ameweza kufadhili ujenzi wa matundu ya vyoo 70 Katika shule za msingi saba ambapo kila shule imejengewa matundu 10 (manne wavulana, manne wasichana na mawili kwa walimu) ambapo jumla ya sh. milioni 63 zimetumika. Alisema kazi hiyo itaendelea awamu ya pili.

“Zaidi ya hayo, nimefanikisha ufungaji wa umeme jua kwenye shule za sekondari nne za Chunyu, Makanjiro, Narungombe na Nambilanje. Katika awamu ya kwanza tumekamilisha kuweka umemejua kwenye sekondari za tarafa ya Mandawa, na tarafa ya Ruangwa imefikiwa nusu tu. Katika awamu ya pili, tutamalizia tarafa ya Ruangwa na kukamilisha tarafa nzima ya Mnacho,” alisema.
Read More

Monday, January 2, 2017

MAJALIWA AMJULIA HALI PROF. MAJI MAREFU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani ambaye amelazwa katika hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es salaam akitibiwa Januari 2, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani ambaye amelazwa katika hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es salaam akitibiwa Januari 2, 2017.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Steven Ngonyani (Profesa Majimarefu) aliyelazwa katika Hospitali ya Kairuki akipatiwa matibabu.

Akiwa hospitalini hapo leo (Jumatatu, Januari 2, 2017), Waziri Mkuu amesema amefurahi baada ya kumkuta Mbunge huyo anaendelea vizuri na kwamba afya yake inaridhisha.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumtakia afya njema Mhe. Ngonyani. Amesema anaamini hivi karibuni atapona na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Kwa upande wake Mbunge huyo ambaye amelazwa katika hospitali ya Kairuki iliyoko Mikocheni jijini  Dar es Salaam, amemshukuru Waziri Mkuu kwa kwenda kumjulia hali.

Pia amesema anaendelea vizuri na anatarajia kwenda nchini India kwa matibabu zaidi mara taratibu zitakapokamilika.

Read More