Wednesday, April 26, 2023

SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 59 YA MUUNGANO MWAKA HUU YAFANYIKA KILA MKOA


Kilele cha sherehe za Maadhisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwaka huu yamefanyika kiaina yake, ambapo kila mkoa unaadhimisha kwa kutelekeza maelekezo mahsusi ya Serikali.

Mkurugenzi wa Kitengo ya Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Batholomeo Jungu ameyamesema hayo jana wakati ziara maalum ya Kamati ya Kitaifa ya maadhimisho hayo mwaka huu ilipotembelea na kukagua utekelezaji wa maelekezo mahsusi kwa Ofisi za Serikali Jijini Dodoma.

Bw. Jungu alisema kuwa kwenye mikoa ndipo kwenye wananchi hivyo shughuli hizi kufanyika katika mikoa zinaleta chachu ya uzalendo kwa wananchi sababu kila mtu anapata nafasi ya kushiriki kuanzia kwenye uzinduzi wa miradi, mashindano ya insha kwa wanafunzi, michezo mbalimbali, usafi wa mazingira na maswala mengine muhimu.

"Watu wapo katika kila mkoa, hivyo tukio hili la kushirikisha wananchi linaleta tija kwa jamii kwa kuona ni sehemu ya maadhimisho haya kwa vitendo,"alisisitiza Jungu.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Bi. Mary Maganga aliseme

Kila mwaka tarehe 26 mwezi Aprili hututumika kama kumbukumbu ya sherehe za Muungano wa Iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar, uliyofanya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo kaulimbiu ya Mwaka huu inasema “ Umoja wetu na Mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza uchumi wetu.”

Katibu Mkuu Masanja alitumia fursa hiyo kueleza namna ofisi yake ilivyotekeleza maelekezo mahsusi ikiwemo kulipamba jengo la ofisi hiyo na kuweka picha za viongozi wakuu wa nchi pamoja na waasisi wa taifa leo

Read More

Tuesday, April 25, 2023

WAZIRI MHAGAMA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 13

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waziri wa Ardhi Nyumba Maendeleo na Makazi Mhe. Dkt Angeline  Mabula na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja Wakati wa Bunge la 12 Mkutano wa 11Kikao cha 13 Mjini Dodoma.

Read More

Monday, April 24, 2023

WAZIRI MHAGAMA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 12

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wakati wa Bunge la 12 Mkutano wa 11Kikao cha 12 Mjini Dodoma.

Read More

Tuesday, April 18, 2023

WATAALAM WAJADILI KUHUSU MPANGO HARAKISHI WA UPATIKANAJI WA RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA.



SERIKALI imefanya uwekezaji mkubwa na maboresho katika sekta ya Afya yanayokwenda sambamba na uwepo wa rasilimali watu itakayotoa huduma zenye ubora ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Hayo yameelezwa  na Mratibu wa Mipango ya Rasilimaliwatu katika sekta ya Afya Bw. Issa Mmbaga kutoka Wizara ya afya wakati wa mawasilisho yaliyohusu upatikanaji wa rasilimali watu katika sekta ya Afya, kwenye kikao cha wataalam kilichofanyika Jijini Dodoma.

Bw. Mmbaga alisema kuwa, baadhi ya maboresho yaliyofanywa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita katika sekta hiyo ni pamoja na ujenzi wa hosptali mpya, ongezeko la vifaa tiba na kuboreshwa kwa miundombinu iliyopo katika eneo la huduma.

“Maboresho haya yamesababisha mahitaji ya ziada ya watumishi katika sekta hii hivyo serikali ina mikakati maalum ya kuhakikisha kunaupatikanaji wa kutosha wa wataalam ili kuwa na sekta ya afya yenye nguvu na uwezo wa kutoka huduma bora za afya”. Alisema Bw. Mmbaga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Sera na Program Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Crispin Musiba, amesema kuwa, uzalishaji wa madaktari na wataalamu wengine katika sekta ya Afya umekuwa mkubwa zaidi kiasi kwamba, idadi kubwa ya wataalam hao wapo nje ya ajira.

“Kwa hivyo ili kupunguza muonekano wa wataalam hao kuwepo nje ya Ajira, tumeita kikao hiki ili kuweza kuwa accommodate wataalam hao katika kupata ajira, na kikao hiki kimetoka na maazimio nane (8) ambayo tumepeana muda wa mwezi mmoja ili yaweze kukamilishwa na kuwasilishwa katika ngazi za juu.” Alisisitiza

Naye Mkurugenzi wa Afya kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapalagwe alisema, ipo haja ya kuendelea kuwa na program za elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii hususan katika masuala ya huduma za kiafya ikiwemo zile za kibingwa zinazotolewa pamoja na kuwa na mikakati madhubuti ya tafiti mbalimbali zitakazoweza kusaidia kujua rasilimali iliyopo katika masuala ya afya.

“Maendeleo yaliyopo katika sekta ya afya, hayatazaa matunda ikiwa hatutaendelea kutoa elimu kwa umma kwa upana wake na kuwa na mikakati ya makusudi inayolenga kuboresha kada hii,”alisema Dkt. Ntuli

Kikao Hicho kilihusisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Utumishi, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu.

=MWISHO=


Read More

Sunday, April 16, 2023

SERIKALI YADHAMIRIA KUENDELEA KUZINGATIA MASUALA YA UTAWALA BORA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema serikali imeridhia kuwa kifungu maalumu cha bajeti kwa ajili ya kuendesha baraza la Vyama Vya Siasa ili kuweza kufanya shughuli zake kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetoloewa wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Vyama Vya Siasa kilichofanyika Mjini Dar es salaam . Amesema serikali Imepitisha Bajeti ya shilingi Billioni Shilingi 1,586,662,000.00 kwa ajili ya kuendesha baraza la Vyama Vya Siasa kwa Mwaka wa fedha 2023/24.

“Kwa kuwa sasa Mhe. Rais Dkt. Samia Sulluhu Hassan ameamua kutenga fedha ya kuendesha baraza, naomba vikao vyote vya kikatiba vya baraza la vyama vya siasa vikae kwa kwa mujibu wa ratiba ikiwa ni pamoja na vikao vya kamati kwa kufuata kanuni na sheria.”

Ameongeza kusema baraza la vyama vya siasa lipewe nafasi ya kukutana serikali ili kujadiliana kuhusu mambo mabalimbali yanayohusu ustawi wa Demokrasia Nchini.

Iko miradi ya kimkakati hapa nchini, kuna kila sababu viongozi wa vyama vya siasa na baraza la vyama vya siasa wapate nafasi ya kuangalia miradihiyo , kwa sababu tunapofika kwenye masuala ya maendeleo ya nchi na ustawi nchi hakuna chama.

“kuna nafasi ya viongozi wa vyama vya siasa kutushauri vizuri zaidi kwa ustawi wa wananchi, “alisema Waziri Mhagama.

Aidha tunahitaji kutengeneza programu maalumu ya mafunzo kwa ajili ya viongozi wetu wa vyama vya siasa, ili tuendele kuimarisha  Demokrasia ya vyama vingi chini, hatuwezi kufanikiwa kama viongozi wetu hawataendana na mabadiliko yanayoyendelea kwenye ulimwengu wa sasa.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama ameomba migogoro ya vyama imalizwe ndani ya vyama, tunauwezo wa kuimaliza sisi wenyewe, tujenge uwezo wa kutizama matatizo yetu ndani ya chama na kuyamaliza ndani ya vyama vyetu.

Waziri amehimiza viongozi wa vyama vya siasa, kuzingatia sheria za matumizi na mapato ya fedha.

Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.

“Mhe. Rais alipoingia madarakani aliasisi ” 4r” ambazo ni (reconcilian, resiliance, reform and rebuilding) kwa kiswahili ni maridhiano, ustamilivu, mageuzi na mabadiliko hii ikiwa ni kwa lengo la kutoa mwongozo wa jinsi ambavyo siasa za nchi yetu zinapaswa kuwa.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama Siasa Juma Ally Khatibu,  ameomba mfaunzo ya siku  tatu mara tu baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili kuwa na uelewa mkubwa kuhusu ” 4r”

Mafanikio ya kikosi kazi katika Mkutano ule uliofunguliwa  Mhe. Dkt,  Samia Suluhu Hassan Jijini Dodoma ambao ni zao la Baraza la Vyama Vya Siasa, ni pamoja na kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa,  mafanikio mengine ni kuundwa kwa Tume ya  Rais ya  kuangalia namna ya  kuboresha Taasisi za Haki jinai.

 

 

 

Read More

Thursday, April 13, 2023

BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU IMEZINGATIA VIPAOMBELE MUHIMU KATIKA MASUALA YOTE YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista  Mhagama amesema Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia vipaombele muhimu katika maeneo yote yanayoratibiwa na Ofisi hiyo ili kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija kwa Taifa.

Ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Mwaka wa fedha  2023/24 wakati wa Kikao cha Bunge la 12 Mkutano wa 11 Kikao cha sita Mjini Dodoma.

Waziri Mhagama amesema pamoja na mambo mengine, Bajeti ya Mwaka huu ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia masuala muhimu ikiwemo la Uratibu wa shughuli za Serikali kwa kueleza tayari ofisi hiyo umeunda  Idara ya ufuatiliaji na Tathimini ya utendaji wa serikaliambapo itawezesha kuwa na taarifa sahihi za utekelezaji wa Shughuki za Serikali.

Akizungumzia kuhusu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Waziri Mhagama amesema, Mamlaka imefanya   kazi ya kutosha katika maeneo yote manne ya kimkakati ya kupambana na dawa za kulevya, kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya, kufanya ukaguzi katika maeneo yanayofanya biashara ya kemikali bashirifu na kufanya maboresho ya sheria na kuteketeza mashamba mengi ya bangi nchini.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Mamlaka imefanya vizuri katika kutoa elimu ya uelewa kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya.

“Tumefanya vizuri katika kupunguza athari za madhara ya dawa za kulevya kwa waathirika, na huduma ya za kutibu urahibu wa dawa za kulevya na bado tunaendelea kufanya mashirikiano ya nchi, kikanda na kimataifa ili kukabiliana na jambo hili mtambuka.”Alisisitiza  

Kwa Upande wa suala la  Sera ya lishe, Waziri amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, itakuja na Mkakati wa kuwa na Sera ya lishe, UKIMWI na Janga la matumizi ya Dawa za kulevya.

Pamoja na hilo, Waziri alieleza kuwa ofisi yale inasimamia Dawati la Afya Moja linaloshughulikia uratibu wa magonjwa ya mlipuko yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, ili kuweza kukabiliana nayo na kuangalia usalama wa wananchi.

Aidha alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kwa falsafa yake ya kuliwezesha Taifa kuwa na ustahimilivu na kuleta mabadiliko makubwa ya kiuongozi, kidemokrasia, kiuchumi na mahusiano ya kimataifa na kuwataka  wabunge kuunga  mkono falsafa hiyo.

 

 

Read More

Friday, April 7, 2023

WAZIRI MHAGAMA NA SIMBACHAWENE WAKABIDHIANA OFISI


 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa umma kutekeleza  majukumu yao ipasavyo  kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo wakati wa hafla ya makabidhiano  kati ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya uteuzi uliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan  Aprili 01 mwaka 2023.

Waziri  Mhagama  amesema dhamira ya mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kikamilifu katika kuwahudumia wananchi mahali na kwa nafasi yoyote anayopangwa  kwa kuzingatia miongozo na taratibu  zilizopo.

“Mara zote dhamira ya mtumishi wa umma  Nchini ni kuhakikisha kila unapopangwa unafanya kazi kwa nguvu zako zote pamoja na utii  na kuwa tayari kutumikia Taifa mahali popote kwahiyo kurudi kwangu hapa najihesabu ni sehemu yenu pia kama mtumishi wa umma,” Amesema Mhe. Jenista.

Pia amebainisha kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za Serikali haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi wake watashindwa kujidhatiti na kufanya kazi kwa moyo kwa kuzingatia mazingira husika.

“Msingi wa tija katika utendaji wa kazi Serikalini  unatutaka  kuwa na uratibu mzuri unaozingatia sera, miongozo na kanuni zilizopo kwa kuzingatia jukumu kubwa la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu shughuli zote za Serikali na tuna jukumu la kusimamia Bunge kama mhimili mwingine ndani ya Nchi hivyo bila kuwa na ushirikiano hatutafikia malengo tunayokusudia,” Ameeleza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amemshukuru  Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa  kumuamini na kumpa  fursa ya kulitumikia Taifa pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu  kwa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini  kuendelea  kuwatumikia wananchi katika nafasi hii na watumishi pia nawashukuru kwa ushirikiano mlionipatia na kuwezesha kufanikisha shughuli za uratibu kwa kipindi chote,” Ameshukuru Mhe. Simbachawene.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Mhe. Simbachawene kwa utumishi wake mwema katika Ofisi hiyo.

Aidha ametumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Waziri Mhagama katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuahidi kumpa ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananachi.

Read More

Sunday, April 2, 2023

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. DKT, SAMIA SULUHU HASSAN AMEWAPISHA MAWAZIRI WAWILI LEO BAADA YA KUFANYA MABADILIKO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Aprili, 2023

Read More

Saturday, March 25, 2023

SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YAKABIDHI MISAADA YA KIBINADAMU KWA SERIKALI YA MALAWI

Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole ameshiriki katIka zoezi la kukabidhi misaada ya Kibinadamu kutoka Tanzania kwa Serikali ya Malawi ili kusaidia wahanga wa Kimbunga Freddy.

Balozi amekabidhi misaada hiyo ya kibinadamu inayojumuisha Mablanket, Mahema, Unga wa Mahindi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo katika Mji wa   Blantrey Nchini Malawi mapema.

Balozi Polepole alibainisha kuwa  wa watanzania, na watu wa Malawi ni jamii moja, na Nia ni kuendekeza umoja uliojengwa na waasisi wa Nchi zetu.

 " Msaada huu wa kibinadamu  utasaidia, katika jitihada za kurejesha matumaini na ustawi kwa ndugu zetu Wananchi wa Malawi", Alisisitiza Balozi Polepole.

Aliongeza kusema kuwa ana imani na wapiganaji  wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioenda  Nchini Malawi  watashirikiana na wenzao Wanajeshi wa Malawi, kuhakikisha kwamba misaada iliyotolewa inawafikia  Wahanga wa Kimbunga Freddy.  

Aidha, Tanzania imetoa madawa ya binadamu, ambayo yataweza kusaidia kwenye maeneo ambayo vituo vya afya vimeathirika. Hizi zote ni jitihada za kusaidia Nchi ya Malawi katika kurejesha huduma za afya.

 

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Msaada aliotoa kwa Nchi ya Malawi, kwa uwezeshaji wa fedha na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Wahandisi wa Medani) ambao watasaidia katika kurejesha hali ya miundo mbinu Nchini Malawi," alisema Balozi.

 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Nchi ya Malawi Mhe. Nancy Tembo amesema ameshukuru Nchi ya Tanzania kwa Msaada wa kibinadamu iliowapatia, ambao umefika katika wakati muafaka.

“Msaada huu ni muhimu kwetu kwa sababu tunao Wanachi wengi ambao makazi yao yameharibika, na tunahitaji msaada wa kila mtu ili kuhakikisha wahanga wa Kimbunga Freddy wanapatiwa huduma za msingi kwa wakati,” alisema Waziri Nancy

Aliongeza kusema Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wamekuja kutusaidia na wataungana na askari wetu wa Nchini Malawi katika kurudisha miundo mbinu iliyoharibika katika hali ya kawaida.

“Nachukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia katika wakati ambao tunahitaji msaada sana, janga hili ambalo limeathiri Nchi ya Malawi, limegharimu maisha ya watu, na limeharibu miundo mbinu” alisema Waziri Nancy.

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na Operesheni pamoja na Uratibu wa shughuli za Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu Luteni Kanali Selestine Masalamado ametoa pole kwa wananchi wa Malawi kwa Maafa ya Kimbunga Freddy.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa kuratibu swala la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Wahanga  wa Kimbunga Freddy Nchini Malawi, ambapo kwa awamu ya kwanza helikopta mbili kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilisafiri kuja Malawi kufanya kazi za wokozi,  lakini msaada wa pili ilikuwa ni msaada wa fedha kwa serikali ya Malawi na tatu ni kutoa msaada wa kibinadamu kwa Wahanga wa Kimbunga Freddy.

 

 

 

Read More

Thursday, March 23, 2023

MISAADA ILIYOTOLEWA NA SERIKALI YA TANZANIA KWA WAHANGA WA KIMBUNGA FREDDY YAVUKA MPAKA KUELEKEA NCHINI MALAWI.


Mkurugenzi Msaidizi  anayeshughulika na Operesheni pamoja na Uratibu wa shughuli za Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Luteni Kanali Selestine Masalamado ameongoza ujumbe wa kutoka Nchini Tanzania kupeleka misaada ya unga, mahindi, mablanketi, mahema na madawa mbalimbali ambayo yatasaidia wahanga wa Kimbunga Freddy kilichotokea nchini Malawi.

Luteni Kanali Masalamado amesema hayo wakati Msafara wa magari ya jeshi la Wanachi wa Tanzania yakivuka mpaka wa Kasumulu wilaya ya Kyela kuelekea Mji wa Blantyre Nchini Malawi.

“Natoa pole kwa ndugu zetu, wananchi wa Malawi tuko nao katika hali hii ngumu,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa kikosi Luteni Kanali George Kamya amesema wanasikitika kwa yale yaliyotokea nchini Malawi baada ya kupigwa na Kimbunga Freddy.

“Katika kuitikia hilo serikali ya Tanzania imetoa msaada kuwasaidia wenzetu waliopata na haya Majanga,” alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Msafara Luteni Kanali George Kamya amesema wanasikitika kwa yale yaliyotokea nchini Malawi baada ya kupigwa na Kimbunga Freddy.

“Katika kuitikia hilo serikali ya Tanzania imetoa msaada kuwasaidia wenzetu waliopata na haya Majanga,” alisema

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Karonga Nchini Malawi Mhe. Roderick Mateauma ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema kwamba msaada huo utasaidia kupunguza athari kwa wahanga na inaonesha mahusiano ya karibu yalipo kati ya nchi hizo mbili.

Read More

Saturday, March 18, 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA, YATEMBELEA MIRADI YA UJENZI WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA KIWANDA CHA UCHAPAJI WA NYARAKA ZA SERIKALI.


 

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imeonesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ujenzi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali Mjini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria Mhe. Joseph Mhagama, leo 18 March 2023 katika ziara ambayo ililenga kujionea kile ambacho kimepangwa kwenye bajeti ya Serikali na kuangalia hatua zilizopigwa, changamoto zilizojitokeza na namna ya utatuzi wake.

“Ziara hii imetuwezesha kupata uhalisia wa hali jinsi ilivyo, ili iweze kutusaidia wakati wa kupanga bajeti, tuwe na uhalisia wa utekelezaji miradi” alisema.

Akizungumzia kuhusu Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Mhe. Mhagama amesema upo muhimu wa Idara hiyo kuwa na mifumo rasmi ya kujisimamia bajeti yake yenyewe (kama wakala) ili isaidie idara hiyo iweze kuingia katika soko shindani.

Aliongeza kusema Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ikiweza kujisimamia katika bajeti yake, itasaidia kuongeza Makusanyo mengi ambayo yanategemewa kutoka katika Idara hiyo.

Tunachangamoto kubwa sana katika utengenezaji wa nembo ya Taifa, “lazima tuwe na Mamlaka moja ya kutengeneza nembo ya Taifa na watu wengine wote waipate kupitia katika Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali, “alisema Mhe. Mhagama.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema anakubaliana na maelekezo ya Kamati. Wizara itatoa taarifa mbele ya Kamati hatua iliyofikia katika kuandaa mabadiliko ya sheria ili kuwezesha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa wakala.

Naye Mhe. Ahmed Ngwali Mjumbe wa Kamati, ameshauri Idara ya Mpiga Chapa Mkuu Wa serikali Kufanyia kazi mapendekezo ya Kamati mapema ili iweze kubadilishwa na kuwa wakala.

Awali Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bwn. George Lugome amesema Utakapokamilika mradi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali itasaidia kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu ikiwa ni sambamba na kuongeza ajira na kuwa sehemu ya mafunzo kwa watu wanasomea maswala ya uchapishaji.

Read More

Tuesday, March 14, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE “TUTUMIE RASILIMALI ZILIZOTOLEWA KUFANYA KAZI”


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene, amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kutumia rasilimali zilizotolewa kufanya kazi kwa bidii na ufanisi.

Mhe.Simbachawene ameyasema hayo mapema leo Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo kilichokutana kwa lengo la kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na makisio ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Aliendelea kusema kuwa, Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu sana mahala pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Watumishi, na alibainisha kuwa, Serikali inazingatia sana suala la Wizara na Taasisi zake kuwa na mabaraza ya wafanyakazi kwani, yanaanzishwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za Idara, Taasisi na Wizara  ili kuweza kusimamia kazi na rasilimali watu.

Alibainisha kuwa mabaraza haya yana majukumu ya kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi, masilahi ya wafanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi. Wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, pia wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya utendaji wa kazi yenye tija, staha na upendo.

Ameshauri menejimenti kupitia baraza hilo la wafanyakazi, kuwa na utaratibu mzuri wa kuwapongeza wafanyakaki wanaotekeleza majumu yao kwa uweledi, ”kuna watumishi ambao kufaya kazi kwa weledi na biidii, na kuwahudumia wananchi kwao ni kama sehemu ya ibada.” Alifafanua

Aliendelea kusema kuwa Utumishi wa umma wa zama hizi ni watu wenye ueledi,wasomi na wenye wasifu mkubwa,lakini wanashindwa kuuonesha kutokana na mazingira kutokuwa rafiki,aliwaasa watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi ya umma kwa bidii.”Jukumu kubwa kwa ninyi viongozi ni kuwahudumia wadogo ili waweze kuleta matoke.”alisema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi aliwashukuru watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza majukumu yao na kusimamia shughuli mbali mbali za serikali kwa kujituma na kwa ufanisi mkubwa.

 

Read More

Thursday, February 23, 2023

TANZANIA YA KWANZA KUSAINI MKATABA WA KITUO CHA HUDUMA YA DHARURA CHA MAAFA MIONGONI MWA NCHI ZA SADC

 


Tanzania imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu na oparesheni za dharura za kanda.

Akizungumza mapema hii leo wakati wa hafla ya utiaji Saini iliyofanyika Jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.

Aliongeza kuwa, Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa  na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi tarehe 21 Juni, 2021.

“Lengo la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa.” Alifafanua.

Aliendelea kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi; Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.

 

Awali mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt Phiness Matto, alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri itavyowezekana.

“Natoa Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea nchi 11 kusaini mkataba huu” Alifafanua Dkt Matto.

Read More

Friday, February 17, 2023

DKT.JINGU:WAKULIMA TUONGEZE MSUKUMO WA KUFANYA KILIMO CHENYE TIJA.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ametoa rai kwa wakulima kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha teknolojia ili kuleta matokeo mazuri zaidi.

Wito huo ameutoa katika kikao cha Kamati ya Tathmini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichohusisha Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo kilichofanyika Februari 17, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Saalam.

Dkt. Jingu amesema dhamira ya Serikali ni kuona wakulima wanatumia rasilimali kidogo na kupata faida zaidi.

Aliongezea kuwa Serikali itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kufanya katika kuimarisha sekta ya Kilimo na Mifugo ili kuongeza ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

“Mwelekeo ni kwamba shughuli wanazofanya ziwe na mwelekeo wa kibishara kwa maana kilimo ni biashara na uvuvi ni biashara,” alisema Dkt.Jingu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema Uvuvi wetu bado tunatumia mbinu za zamani lakini sasa tunaenda kutoa boti mpya za kisasa zitakazofanya wavuvi waongeze tija.

Ameongeza kusema kuwa, jitihada hizo zinaenda sambamba na kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwenye vizimba katika ziwa Viktoria kwa kuwapatia vizimba vya samaki na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki.

“Lengo ni kuongeza uzalishaji wa samaki na kutimiza malengo tuliyopewa na Mhe. Rais wa kuongeza tani za uzalishaji wa samaki ifikapo Mwaka 2026,” alisema Dkt.Madalla

Aidha Serikali itaenda kutoa mikopo kwa wakulima wa zao la Mwani katika ukanda wa Pwani ili waweze kununua vifaa na waweze kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani.

"Tunaimani zao hili litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua kipato na kuboresha maisha hasa kwa wakina mama ambao ndiyo wakulima wakubwa wa zao la Mwani na vyote hivi ni katika utekelezaji wa Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili,"alisisitiza Dkt. Madalla

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema Mpango wa Usimamizi na Ushauri wa Program ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ni mpango jumuishi unaohusisha wizara kupitia Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi  ambayo yanajihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na uwekezaji.

 

Read More

Thursday, February 16, 2023

MEJA JENERALI MBUGE: TUTAENDELEA KUJIPANGA KATIKA KUKABILANA NA MAAFA NCHINI


 SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuweka mikakati madhubuti katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini ili kuhakikisha inapunguza madhara yatokanayo na maafa.

 

Kauli hiyo imetolea na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua kikao kazi cha wadau cha kupitia na kujadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya African Dream Jijini Dodoma.

 

Kikao kazi hicho kililenga kupitia na kujadili rasimu ya mpango huo wenye malengo ya  kusimamia mawasiliano na kuweka utaratibu wa matumizi ya huduma za mawasiliano ndani ya Serikali, Umma, Wadau wa Mawasiliano na Mashirika Binafsi.

 

Meja Jenerali Mbuge alisema, upo umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote wa masuala ya maafa nchini kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kuwa na mikakati madhubuti ya mawasilino wakati wa dharura.

 

“Hakikisheni kuwa mpango unazingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 na Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa 2022 ili kurahisisha utekelezaji wake,”alisisitiza Meja Jenerali Mbuge.

 

Akieleza kuhusu Mpango huo, alisema utarahisisha mawasilino ya haraka, sahihi na kwa wakati unaohitajika kwa kuzingatia mfumo huo uliojikita kidijiti na unahusisha vyombo vya habari ikiwemo matumizi ya radio, televisheni na mitandao ya kijamii.

 

Katika hatua nyingine Idara imeendelea kuchukua hatua za kupunguza madhara kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za dharura zinatolewa kwa wakati kwa kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya kitaifa na kisekta. Juhudi hizi zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi, Mashirika ya kimataifa na Asasi zisizo za kiserikali.

 

“Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inajukumu la kuratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini,”alisema.

 

Idara ya maafa ilizindua nyaraka za usmamizi wa maafa nchini ikiwemo; Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura 2022 ambao umelenga kuhakikisha utendaji kazi, ushirikiano, na mwendelezo wa mawasiliano vinaimarika wakati wa maafa ili kuruhusu watoa huduma za dharura kufanya mawasiliano baina yao na ngazi nyingine za serikali wakati wote, hata pindi miundombinu ya mawasiliano itakapoharibiwa


Read More

Friday, February 10, 2023

WAZIRI MKUU AZINDUA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.

Amesema pamoja na uwepo wa sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, wakati akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Nyaraka zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022).

Nyaraka nyingine ni Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022), Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

Amesema miongozo na mipango hiyo ya usimamizi wa maafa inatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza.

Waziri Mkuu amesema nchi bado inao uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.

“Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu, tuwe sehemu ya watendaji wakati wa dharura zinapojitokeza badala ya kusubiri tuanze kulaumu. Wale wenye nguvu na uwezo wa kusaidia wajitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali badala ya kuwa watazamaji mfano ilipotokea ajali ya ndege wananchi walijitokezakusaidia.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya usimamizi wa maafa.

Pia, Waziri Mkuu amezielekeza wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine zitenge fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za usimamizi wa maafa katika maeneo yao. “Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya nendeni mkasimamie kikamilifu bajeti katika maeneo yenu ili kuwezesha usimamizi wa maafa.”

Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa watenge rasilimali kabla ya kutokea kwa maafa na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejijengea uwezo wa kukabiliana na maafa hayo, pia sekta zote zilizopewa majukumu ya kusimamia maafa zihakikishe zinaratibu upatikanaji wa msaada wa kitaalamu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.

Kwa upande wake, Muwakili Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi Veronica ameihakikishia Serikali kuwa UNDP pamoja na wadau wengine wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na maafa.

Amesema nyaraka hizo zilizozinduliwa leo zitasaidia katika upatikanaji wa taarifa za maafa kwa wakati na hivyo kuwawezesha wahusika kuchukua hatua haraka.

 

Read More

Tuesday, February 7, 2023

WAZIRI MKUU MGENI RASMI UZINDUZI WA NYARAKA ZA USIMAMIZI WA MAAFA.

 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa nchini tarehe 09 Februari, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage uliopo Hazina Jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipokutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya habari Bungeni Dodoma kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi.

Waziri Simbachawene alisema, katika kuendeleza juhudi za kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Maafa Nchini, Serikali imefanya mapitio ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2012), Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2012) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2015-2020). Hivyo, mapitio hayo yamewezesha kuandaliwa kwa nyaraka tano zitakazozinduliwa ikiwemo;Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022),Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa (2022) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027),Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).

“Nyaraka zote tano zimeandaliwa kwa kushirikisha wadau ndani na nje ya Serikali. Nyaraka zinazozinduliwa zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na baadaye katika mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa,”alisema Waziri.

Alifafanua kuwa, mipango na mikakati iliyoandaliwa itaimarisha usimamizi wa maafa yanayosababishwa na majanga ya nguvu za asili kama vile mafuriko na matetemeko ya ardhi na majanga yanayochochewa na shughuli za kibinadamu.

Aidha, Majukumu ya utendaji yanazingatia taasisi yenye wajibu wa kisheria, ujuzi pamoja na rasilimali zinazohitajika. Mfumo uliopo umezingatia wajibu wa sekta kutambua hatari za maafa katika eneo lake, kutenga rasilimali za kisekta kabla ya tukio kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabili maafa endapo yatatokea.

Aliongezea kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha shughuli za kuratibu na kusimamia shughuli za maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na Kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na miongozo, mikakati na taratibu za kiutendaji zinazowezesha utekelezaji wa majukumu na kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano wa wadau.

Read More

Friday, February 3, 2023

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU NAMMA YA KUPATA CHAKULA CHA MSAADA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema maswala ya upungufu wa chakula yanachukuliwa kama maafa kwa mujibu ya sheria ya maafa iliyopo.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati akifafanua hoja iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Yahaya Ally Mhata Bungeni  katika Mkutano wa Kumi Kikao cha Nne cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu taratibu za kufuata ili kupata chakula cha bei nafuu.

Alisema kuwa, Ofisi yake inajukumu ya kuratibu upatikanaji wa chakula cha msaada kwa kushirikiana na sekta tofauti tofauti ikiwemo hatua zote muhimu za uzalishaji, upatikanaji hadi matumizi kwa walaji.

Alifafanua Ofisi ya Waziri Mkuu inajukumu la kutoa kibali kwa ajili ya chakula cha bei nafuu au msaada linaratibiwa kwa kuielekeza Wizara ya Kilimo kuchukua hatua kupitia NFRA.

 “Kimsingi jukumu la kutoa chakula cha bei nafuu au msaada ni jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo inalitekeleza kwa kuelekeza Wizara ya Kilimo ili ielekeze NFRA kupeleka eneo la kukipeleka kile chakula na kwenda kukiuza kwa bei nafuu iliyopangwa,” alisisitiza waziri.

Read More

KATIBU MKUU KASPAR MMUYA ATETA NA WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU

 


Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wametakiwa kutumia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali pamoja na Busara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

 

Hayo yamesema na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  Bw. Kaspar Mmuya.

 

Bw. Mmuya alisema ameitumikia Ofisi hiyo na kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja kwa lengo la kuleta matokeo chanya.

 

“Kwa majukumu ya Ofisi hii jinsi yalivyo yalitupa nafasi sisi wengine ya kujua wizara nyingine zinafanya nini katika kutekeleza majukumu ya Serikali kwa ujumla,”alisema Katibu Mkuu huyo.

 

Pia amewahimiza  watumishi wa Ofisi hiyo kuishi kwa upendo na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu hatua itakayochochea maendeleo ya Taifa na shughuli za Serikali kufanyika katika hali ya ubora na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Sambamba na hilo, Bw. Mmuya alimshukuru Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu kwa kumfundisha, kumuongoza na kumpa ushirikiano wakati wote alipokuwa akitumikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu katika ofisi hiyo.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu  Dkt. John Jingu alisema kuwa Katibu Mkuu Mmuya alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa matokeo hivyo  watumishi kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa  kufanya kazi kama timu katika kuitumikia Nchi, kuishi na watu vizuri.

 

 “Tujitahidi kila wakati kufanya kazi kwa matokeo, uliyaishi matokeo na unaendelea kutukumbusha tuyaishi hayo, kila mtu ana nafasi yake lakini lazima kuheshimiana na kujua umuhimu wa kuwajibika, tuendelee kufanya kazi kwa matokeo weledi ushirikino na nidhamu sisi ni timu moja tushirikiane.” Alisisitiza Dkt. Jingu.

 

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Katibu wa  TUGHE tawi la  Ofisi hiyo Bw. Dotto Kyaolang amemshukuru Katibu Mkuu Mmuya kwa kutoa dira ya utendaji kazi na kumtakia afya njema na utendaji mwema katika kituo chake kipya cha kazi.

 

 

Read More