Na. OWM, MOROGORO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mwaka
jana kwa Tume hiyo, ambapo aliiagiza Tume hiyo kuwa na mpango mkakati wa Kuhakikisha kuwa
migogoro ya kazi nchini inatatuliwa kwa njia ya Usuluhishi bila kufika katika ngazi
ya maamuzi, kutokana na utekelezaji wa agizo hilo asilimia 86.73 ya migogoro ya
kazi 9,646 iliyosajiliwa nchini imetatuliwa kwa njia ya usuluhishi bila kufika
kwenye ngazi ya maamuzi.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo, tarehe
19, Desemba 2019, mjini Morogoro, wakati akifungua kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji
wa Majukumu ya Tume kilichowakutanisha Wasuluhishi
na Waamuzi wa migogoro ya kikazi na wasaidizi wa Tume hiyo. Aidha, amefafanua kuwa njia bora ya
kutibu mahusiano ya kiajira yaliyotetereka ni kupitia kumaliza mashauri kwa
njia ya usuluhishi.
“Nawapongeza Wasuluhishi na Waamuzi wa
mashauri ya kikazi, jitahidini mfanye kazi kwa uadilifu, kwani hata kwenye
mashauri yaliyohitaji kutatuliwa kwa njia ya maamuzi asilimia 78 ya mashauri 5,131
ya maamuzi yaliyosajiliwa yamepata maamuzi,mmefanya kazi nzuri kwa kuvuka nusu
ya mashauri, pia mmepunguza malalamiko
ya watumishi kupata haki zao ambazo zimekuwa zikipotezwa na baadhi ya wajanja katika sekta ya ajira
bila kuwa na huruma kwa watanzania wenzao ” Amesema Mhagama
Mhe. Mhagama ameeleza kuwa kitendo cha
Tume hiyo kutekeleza agizo lake la kuanzisha kitengo cha Usuluhishi na kuteua
Mkurugenzi anayeratibu Kitengo hicho kunadhihirisha dhamira ya Tume hiyo ya
kuhakikisha migogoro ya kikazi haizalishwi kwa kuwa huchochea kutumika vibaya kwa rasilimali muda kati ya mwajiri na
Mfanyakazi hali inayopelekea kuchelewesha Maendeleo.
“Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza miradi ya
Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii ikiwemo kujenga viwanda, kujenga reli ya kisasa, kujenga bwawa la Nyerere
litakalozalisha Umeme, Utekelezaji wa Miradi hii maana yake kuna ajira
zinazotengenezwa hivyo tutarajie na migogoro ya kazi pia kuzalishwa, kwa
mantiki hiyo Tume haina budi kuendana pia na kasi ya maendeleo ili kuifanya nchi yetu kuwa
mahala salama ya uwekezaji na ufanyaji wa kazi ”
Amesisitiza mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama ameitaka Tume hiyo kuendelea kufanya
utafiti kwa sekta zote zinazoongoza kwa migogoro ya kikazi ili
kubaini chanzo cha migogoro hiyo na kuandaa Mkakati Maalum wa kuishughulikia,
kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Kupitia Tume hiyo imepewa jukumu la kutatua migogoro na kuweka
msisitizo wa kuimaliza migogoro.
“Nimepitia ripoti yenu inaonesha bado sekta ya Ulinzi binafsi
inaendelea kuwa kwenye kundi linaloongoza kwa migogoro, lakini sekta ya Hoteli pia
kila mwaka ipo kwenye kundi hilo, lakini ziko sekta nyingine kama sekta ya
Ujenzi kwa mwaka huu imeondoka lakini sekta ya Viwanda imeingia kwenye sekta zinazoongoza za
migogoro japo si kwa kiwango cha juu, kwa kuwa tumejipambanua tunajenga uchumi
wa viwanda lazima muwe na mpango kazi ili kuweka mazingira wezeshi kwa Taifa
letu” Amesisitiza Mhagama
Awali
akiongea katika kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na
Uamuzi, Shanes Nungu alibainisha kuwa Tume hiyo iliamua kutelekeza maagizo ya
Mhe. Waziri Mhagama kwa kuboresha Mkakati Wa Mpango kazi Wa Tume ambao
umesaidia kuwa na mpango mkakati kwenye mtazamo
Wa kupunguza migogoro na unaolenga kumaliza migogoro, lengo nikutaka kutatua migogoro na kuweka msisitizo wa kuimaliza migogoro
kwenye sekta zinazoongoza kuwa na migogoro
mahala pa kazi.
"Wasuluhishi na Waamuzi wa
mashauri ya Kikazi kwa pamoja wamekuwa wanajitahidi kumaliza na kuipunguza
migogoro ya kikazi, kwani tumefanikiwa kumaliza migogoro hiyo kwa asilimia 86
kwenye hatua ya Usuluhishi na asilimia 78 kwenye hatua ya Uamuzi kwa migogoro
na mashauri yote yaliyosajiliwa," alieleza Nungu.
Naye, mjumbe kutoka Shirika la Kazi
Duniani (ILO) aliye mwakilisha Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani hapa
nchini, Maridadi Marwa amefafanua kuwa ILO wanaunga mkono utatuzi wa migogoro
uishie kwenye hatua ya Usuluhishi, kwani utatuzi wa njia hiyo humaliza
mgogoro kabisa kwani pande mbili zenye tofauti hukubaliana tofauti na hatua ya
uamuzi ambapo mmoja huambiwa kashindwa hivyo ni bora kujikita katika utatuzi wa
usuluhishi.
Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo Kikao cha Baraza la Wafanyakazi
wa Tume hiyo kimefanyika kwa mujibu wa Agizo la Rais Na.1 la mwaka 1970. Baraza
hilo huiwezesha Tume kuboresha Huduma na masuala ya utatuzi Wa
migogoro ya kikazi kwa njia ya Usuluhishi na Uamuzi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama
akisisitiza umuhimu wa kutatua migogoro ya kikazi kwa kutumia njia ya
Usuluhishi wakati kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya
mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019.
|
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Shanes Nungu akiongea,
wakati wa kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa
Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, mjini
Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha wakutanisha Wasuluhishi na Waamuzi wa migogoro ya kikazi na
wasaidizi wa Tume hiyo.
|
|
Baadhi ya
washiriki wa kikao kazi cha
Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, mjini
Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha wakutanisha Wasuluhishi na Waamuzi wa migogoro ya kikazi na
wasaidizi wa Tume hiyo.
|
|
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akimpongeza
mmoja wa watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, wakati kikao kazi
cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019.
|
|
Baadhi ya
washiriki wa kikao kazi cha
Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini,wakifuatilia
kikao kazi cha Tathmini ya utekelezaji
wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao
hicho kimewajumuisha Wasuluhishi na Waamuzi wa migogoro ya kikazi na
wasaidizi wa Tume hiyo.
|
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, wakati kikao
kazi cha Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya mjini Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019
Baadhi ya
washiriki wa kikao kazi cha
Tathmini ya utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi nchini, mjini
Morogoro, tarehe 19 Desemba, 2019, kikao hicho kimewajumuisha wakutanisha Wasuluhishi na Waamuzi wa migogoro ya kikazi na
wasaidizi wa Tume hiyo.