Thursday, February 27, 2020

CHANGAMOTO YA UMEME NA UTITIRI WA KODI VYALALAMIKIWA MKOA WA MARA

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika Manispaa ya Shinyanga wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (hayupo pichani) Februari 26, 2020.
Mmoja wa wafanyabiashara mkoa wa Shinyanga Bw. Idsam Mapande akiwasilisha hoja zinazohusu kero za madereva pikipiki wakati wa mkutano huo.
Mmoja wa wachimbaji wadogo mkoa wa Shinyanga Bw. Ludaki Shaban akiwasilisha kero za ukosefu wa umeme katika maeneo ya uchimbaji wakati wa mkutano wa kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara katika mkoa huo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akisalimiana na Mhe.Steven Masele (Mb) wakati wa Mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Tellack akieleza kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa wake wakati wa Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika Manispaa ya Shinyanga Februari 26, 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akihutubia wakati wa Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika Manispaa ya Shinyanga Februari 26, 2020.
Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mhe. Constantine Kanyasu akijibu hoja wakati Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika Manispaa ya Shinyanga  mkoani Shinyanga.
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akijibu hoja za masuala ya wafugaji na wavuvi wakati wa mkutano huo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akijibu hoja za masuala ya wafugaji na wavuvi wakati wa mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa mkutano huo.

Wednesday, February 26, 2020

ZAIDI YA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI 560 WASIKILIZWA KERO ZAO SHINYANGA

NA. MWANDISHI WETU
Zaidi ya wafanyabiashara na wawekezaji 560 mkoani Shinyanga wamekutana katika mkutano wa mashauriano baina ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa changamoto katika maeneo yao ya uwekezaji na biashara ili kuendelea kuwa na tija katika maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Mkutano huo ulililofanyika tarehe 26 Februari, 2020 ulioandaliwa na  Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga na  kufanyika  katika Ukumbi wa mikutano wa NSSF mkoani humo.
Mkutano ulijumuisha makundi yote ikiwemo, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wachimba madini, wavuvi pamoja na wenye viwanda na  wawekezaji katika sekta mbalimbali.
Mkutano ulihudhuriwa na Mawaziri na Manaibu mawaziri kutoka Wizara nane ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Wizara ya Fedha na Mipango, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Madini.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe.Angellah Kairuki alieleza namna Serikali ilivyoendelea na jitihada za kuhakikisha uboreshwaji wa mazingira ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria mpya ya uwezeshaji biashara (Business Facilitation Acts)
Aidha sheria itasaidia kufanya mapitia ya sera na sheria stahiki kwa lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.
Aliongezea kuwa, uwepo wa mikutano hiyo inaongeza hamasa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kueleza kero wanazokabiliana nazo pamoja na kupatiwa majibu ya papo kwa hapo na Mawaziri wa Sekta husika.

“Mikutano imeibua hoja muhimu zilizopatiwa ufumbuzi na mawaziri wa sekta mbalimbali  niwatoe shaka Serikali itaendelea kuwaunga mkono na ni vyema mkaendelea kufuata sheria na kanuni zilizopo katika kuwekeza kwenu,”.alisisitiza Waziri Kairuki.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewahakikishia wafugaji wa samaki kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wafugaji kufuga samaki na kueleza kuwa, mabwawa ya samaki yameongezaka kutokana na jitihada zilizopo na kueleza namna Serikali inavyoendelea kudhiti uvuvi haramu baharini na maziwa.
Sambamba na hili Naibu Waziri alieleza kuwa  jitihada za ujenzi wa viwanda vikubwa vya kuchakata mazao yatokanayo na mifugo nchini zinaendelea hivyo wananchi hawana budi kuwa na matumaini makubwa na Serikali yao.
Aidha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashantu Kijaji aliwahaikishia wajumbe wa mkutano huo namna wizara yake ilivyojipanga kuondoa changamoto za gharama kubwa za mikopo katika benki pamoja na suala la utitiri wa kodi baada ya kulalamikiwa na wafanyabiashala hao.
“Nimewafurahia wana Shinyanga kwa uwazi wenu wa kujieleza vizuri, niwahakikishie kuwa,mwisho wa malalaiko yenu haupo mbali tutahakikisha sekta ya fedha inatatua kero zenu na kushughulikia upatikanaji wa mikopo na kwa gharama zinazoeleweka,”alieleza Dkt. Kijaji
Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha Taasisi zetu za mikopo zinashusha gharama za mikopo (riba) kwa ajili ya shughuli za kijamii zinazowahusu.

Tuesday, February 25, 2020

MAJALIWA AONGOZA KIKAO CHA KUJADILI MAENDELEO YA MICHEZO NCHINI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza   na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia kwake ) na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao cha kujadili maendeleo ya michezo nchini kilichofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini  Dar es salaam, Februari 25, 2020.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza   na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia kwake ) na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao cha kujadili maendeleo ya michezo nchini kilichofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini  Dar es salaam, Februari 25, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza   na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia kwake ) na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao cha kujadili maendeleo ya michezo nchini kilichofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini  Dar es salaam, Februari 25, 2020.


Monday, February 24, 2020

CHANGAMOTO YA UMEME NA UTITIRI WA KODI VYALALAMIKIWA MKOA WA MARA


MWANDISHI WETU MUSOMA

Wafanyabiashara na wawekezaji wa Mkoa wa Mara wameelezea kero mbalimbali zinazochangia kukwamisha ukuaji wa uwekezaji mkoani humo ikiwemo tatizo la umeme na wengine kueleza changamoto za utitiri wa kodi.

Wameeleza changamoto hizo Februari 24, 2020 wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara wa mkoa wa Mara uliohusisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka Sekta mbalimbali ikiwemo Viwanda na Biashara na masuala ya Fedha wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki   uliofanyika Wilaya Musoma Mjini katika Mkoa wa Mara.

Lengo la mkutano huo lilikuwa kusikiliza changamoto na kero wanazokabiliana nazo katika maeneo yao ya  biashara na uwekezaji na kuzitatua, ambapo wameeleza namna utitiri wa kodi na kukatikatika kwa umeme kunavyochangia uzorotaji kwa ukuaji wa uchumi na kuiomba Serikali kushughulikia tatizo hilo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Wafanyabiashara hao walieleza kuwa, kukosekana kwa umeme wa uhakika umekwamisha shughuli za uzalishaji ikiwemo zile za viwandani.

Kufuatia hali hiyo wameiomba Serikali kutatua kero hiyo huku wengine wakibainisha hasara wanazopata katika changamoto hiyo.

Akieleza changamoto za uwekezaji Dkt. John Changwa alieleza kuwa, TANESCO imechangia kukwamisha uzalishaji katika viwanda kutokana na  umeme kukatika mara kwa mara pamoja na kutofika kwa wakati katika viwanda vidogo kwa kuhusisha changamoto ya miundombinu hafifu ikiwemo barabara.

“Ni kweli kabisa TANESCO hamtutendei haki kwani mmekuwa mnatukwamisha kwa muda mrefu na mmeshindwa kufika kwa wakati hasa katika maeneo vinavyojengwa viwanda  huku  vikiwa vihitaji huduma za umeme hivyo ni vyema mkabadili utaratibu na kuona namna ya kutufikia kwa wakati,”Alieleza Dkt. Changwa

Akijibu baadhi ya kero hizo kwa kushirikiana na mawaziri wengine Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu uwekezaji Mhe. Angellah  Kairuki ametumia fursa hiyo kuzikumbusha Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maamuzi ya Serikali kwa kuhakikisha changamoto zilizoainishwa ikiwemo utitiri wa kodi, uwepo wa riba kubwa zinazotozwa na benki, ucheleweshwaji wa vibali vya ajira, ukosefu wa ajira kwa vijana, na uvuvi wa kutumia vyavu zisizokidhi mahitaji halisi na bei elekezi kuwa juu.

 ‘’Ni wakati sahihi kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kuhakikisha tunatatua na kumaliza kero zinazowakabili wawekezaji na wafanyabiashara ili kuendelea kuwa na maendeleo katika nchi yetu na niwahakikishie Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwa na tija inayotakiwa,”alisema  Waziri Kairuki.

Sambamba na hilo alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na Serikali katika ulipaji wa kodi mbalimbali kwa utaratibu uliopo na kuhakikisha wanachangia katika ukuaji wa pato la taifa.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inasisitiza ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya watanzania na taifa kwa ujumla hivyo lazima tuzingatie na kutimiza wajibu wetu ili kuepuka kuingia katika makosa yasiyo ya lazima na kupelekea uwekezaji wenu kuwa wa hasara”,alisisitiza Waziri Kairuki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima alimhakikishia Waziri kuendelea kutatua kero na changamoto katika mkoa wake ili kuwahakikishia mazingira rafiki ya uwekezaji wao huku akiahidi kuendelea kusimamia sheria zote zinazowahusu ili kuwa na tija katika kuwekeza mkoani humo kwa kuzingatia fursa zilizopo.

“Mkutano huu umekuwa wa faida sana kwa kuzingatia umetoa fursa kubwa kwa kuwakusanya wafanyabiashara na wawekezaji 400 kwa pamoja na kuweza kuzieleza kero zao, tunaahidi kero ambazo hazijapatiwa majibu kwa siku ya leo zitatatuliwa haraka iwezekanavyo,”Alisisitiza Mhe. Malima.


=MWISHO=

CHANGAMOTO YA UMEME NA UTITIRI WA KODI VYALALAMIKIWA MKOA WA MARA

Mfanyabiashara na mkulima mkoa wa Mara Bw. Wambura Mwita akichangia hoja wakati wa mkutano wa wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto cha wawekezaji na wafanyabiashara.
Mfanyabiashara mkoa wa Mara Bw. Edward Masato akichangia hoja wakati mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara uliofanyika Februari 24, 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima wakiangalia viatu vya ngozi vinavyotengenezwa na wafanyabiashara wa mkoa huo, wakati wa maonesho ya wafanyabiashara wakati wa Mkutano huo.
Naibu Waziri Viwanda na Biashara Mhe. Mhandisi Stella Manyanya akijibu hoja za wawekezaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara wakati wa Kongamano lao la kueleza changamoto na kupatiwa ufumbuzi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipata maelezo kuhusu biashara ya ngozi kutoka kwa mfanyabiashara na mfugaji Bw. Jonath Magige wakati wa maonesho ya wafanyabiashara walioshiriki katika mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara  uliofanyika Wilaya ya Musoma Mjini Mkoa wa Mara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akihutubia wakati wa Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika Wilaya ya Musoma Mijini Mkoa wa Mara Februari 24, 2020.
Naibu Waziri Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akijibu hoja za wawekezaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara wakati wa Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara mkoa wa Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima akitoa maelezo kuhusu mkoa wake wakati wa Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara na kuzipatia ufumbuzi uliofanyika katika Mkoa wa Mara Februari 24, 2020.
Sehemu ya wajumbe walioshiriki mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara wakifuatili hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (hayupo pichani).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (wa pili kutoka kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima, Mhe. Dkt. Ashatu kijaji Naibu Waziri Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri Viwanda na Biashara Mhe. Mhandishi Stella (Manyanya wa kwanza kushoto) wakiimba wito wa Taifa wakati wa mkutano wa wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angelah Kairuki akioneshwa nyavu inayotumika kuvulia samaki na Mvuvi Bw. Msendo Mwigine wakati wa mkutano wa wa mashauriano kati ya Serikali na Sekta binafsi ili kusikiliza changamoto za wawekezaji katika Mkoa wa Mara.

Sunday, February 23, 2020

MAJALIWA: SEKTA YA MADINI KUCHANGIA ASILIMIA 10 YA PATO LA TAIFA IFIKAPO 2025


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hatua iliyofikiwa ya kuzuia uvunaji haramu wa rasilimali kwa utaoji wa cheti cha uhalisia kwa madini ya bati, kutaiwezesha sekta ya madini nchini kuchangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 23, 2020) wakati wa kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere.

Waziri Mkuu ambaye amezindua utoaji wa cheti cha uhalisia (certificate of origin) kwa madini ya bati kitakachokuwa kinatolewa na Tanzania, amesema cheti hicho ni muhimu kwa Taifa letu na nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maziwa Makuu kwa kuwa kitaweka utaratibu wa kudhibiti madini hayo.

Waziri Mkuu amesema mambo waliyojifunza katika mkutano huo yatasaidia kuongeza kasi ya kukua kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa. “Wizara ya Madini shirikianeni na wadau wengine katika kuhakikisha mkutano huu unaendelea kuboreshwa kila mwaka na kuongeza washiriki ili kupanua uelewa wa pamoja.” 

Waziri Mkuu amesema kuwa ni matarajio ya kila mmoja wao kwamba uzinduzi huo walioufanya utasaidia katika kutekeleza Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu wa Rasilimali yaani ‘Protocol Against the Illegal Exploitation of Natural Resources’

“…nafahamu kwamba mkutano wa aina hii unaoihusu sekta ya madini unafanyika kwa mara ya pili hapa nchini. Nitoe wito kwa nchi wananchama kuhakikisha mikutano ya aina hii iweze kuandaliwa katika nchi nyingine na iwe endelevu katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa zilizopo nchi nyingine.” 

 Waziri Mkuu amesema Serikali inaridhishwa na kuimarika kwa utendaji kazi wa sekta ya madini nchini kutokana na mafanikio yake ikiwemo kuongezeka kwa mchango wake katika pato la Taifa. “Mathalan, kupitia Taarifa ya Hali ya uchumi ya Mwaka 2019, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020, mchango wa Sekta ya Madini ulikua kwa asilimia 13.7.”

Waziri Mkuu amesema kwenye kipindi hicho, sekta ya madini ilikuwa ya pili katika kuchangia pato la Taifa ikitanguliwa na sekta ya ujenzi ambayo ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 16.5. 

“Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya sh. bilioni 242.53 sawa na asilimia 51.5 ya lengo la mwaka la kukusanya sh. bilioni 470.89.Makusanyo hayo yalitokana na mrabaha, ada ya ukaguzi wa madini, huduma za kimaabara, mauzo ya machapisho mbalimbali ya kijiolojia na ada za leseni.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini, Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi. “Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 28 kote nchini.” 

Amesema masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwake, hivyo ametumia fursa hiyo kuwafahamisha wadau wa mkutano huo kuwa masoko hayo yapo wazi kwa wadau wa ndani na nje ya nchi. 

Waziri Mkuu ametoa wito kwa nchi ambazo bado hazijaanzisha masoko ya madini kutumia masoko yaliyoko nchini wakati wakijipanga kuanzisha masoko yao. 

“Masoko haya yanafanya kazi katika misingi ya kiushindani na uwazi wa kibiashara. Pia, niwahakikishie kuwa masoko yetu yana ulinzi na usalama wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha biashara hiyo. Hivyo, yatumieni vizuri masoko haya.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa sambamba na kuanzishwa kwa masoko ya madini, Serikali pia imefanikiwa kuhamasisha wamiliki wa migodi kuchangia zaidi katika huduma za jamii nakuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa na wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo wa madini.

“Vilevile, Serikali imefanikiwa kuongeza ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali katika kumiliki na kusimamia migodi, ikiwa ni pamoja na kumilikishwa asilimia 16 ya hisa katika migodi;na kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi.”

Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema mkutano huo umehudhuriwa na nchi 11 wanachama waJumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) pamoja na wadau wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi.

Waziri Biteko alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa madini katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo wachimbaji, wanaotengeneza na kuuza tekinolojia, wadau wenye mitaji na wasionayo lakini pia kwa upande wa Serikali kujifunza namna ya kuboresha na kuifanya sekta ya madini kuwa ni sekta yenye kuongeza tija kwa Taifa.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akikata utepe kuzindua  Utoaji wa Cheti cha Uhalisia kwa Madini ya Bati kwenye  ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 23, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 23, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha  Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Februari 23, 2020.

(mwisho)

Saturday, February 22, 2020

MAJALIWA AONDOKA KIGOMA BAADA YA ZIARA YA SIKU MOJA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngoma kwenye uwanja wa Ndege wa Kigoma  kabla ya kuondoka baada ya kukamilisha ziara ya siku moja mkoani humo, Februari 22, 2020.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga kwenye uwanja wa Ndege wa Kigoma baada ya kukamilisha ziara ya siku moja mkoani humo, Februari 22, 2020. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kigoma, Amandus Nzamba.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo  Februari 22, 2020 ameondoka mkoani Kigoma baada ya kukamilisha ziara ya kikazi ya siku moja. Pichani, Mheshimiwa Majaliwa akiwaaga viongozi  kwenye uwanja wa Ndege wa Kigoma.

Friday, February 21, 2020

DKT. SHEIN ATAKA MIKAKATI YA PAMOJA YA KUKABILIANA NA MAAFA KWA NCHI ZA SADC

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema “Kufanyika kwa Mkutano wa SADC ni hatua muhimu katika kujenga matumaini mapya ya wananchi kuhusiana na maafa, tukizingatia kwamba katika miaka ya hivi karibuni  kumekuwa na ongezeko kubwa la  maafa pamoja na viashiria  vyake  katika nchi wanachama wa SADC.”Ameyasema hayo wakati akifungua  Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi za SADC, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu  Mhe. Jenista Mhagama amesisitiza “Ushiriki wa kisekta katika kukabiliana na maafa ni njia pekee ya kupunguza madhara ya  maafa kwa Nchi wanachama wa SADC”, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa kwa Nchi za SADC.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia maafa na kusisitiza kuwa  “Majanga hayana urasimu kitu muhimu kushirikiana kwa pamoja katika kukabiliana nayo pindi yanapotokea nchini”, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.  
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC wakiwemo Mawaziri, Washauri wa Rais na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi na Usalama wakisikiliza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na Maafa Zanzibar, leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Baadhi ya waalikwa kwenye mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya  Maafa kwa Nchi  wanachama wa SADC, wakifuatilia  mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wenye dhamana ya Menejementi ya maafa kwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC baada ya kufungua Mkutano huo leo tarehe 21, Februari, 2020, Zanzibar.


Na. OWM, ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein amesema maeneo ya visiwa yapo katika hatari  kubwa  zaidi ya kukumbwa na maafa ukilinginisha na maeneo mengine duniani, hivyo alitoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuja na mikakati imara itakayoainisha mbinu za kutambua na kuwahi viashiria vya maafa kabla madhara hayajatokea.

“Tuna jukumu la kuendelea kushirikiana kati ya Serikali zetu, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kimataifa, Taasisi za Utafiti, Sekta Binafsi, Taasisi za Kidini, Taasisi za Fedha na  Mashirika yasiyo ya Serikali, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari katika suala hili. Tukifanya hivyo, itakuwa tumeitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mkutano huu isemayo:  “Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kujenga uhimili katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.” 

Rais Shein amesema hayo leo tarehe 21, Februari, 2020 Zanzibar alipokuwa anafungua kikao cha Mawaziri wa nchi za SADC wenye Dhamana ya Menejimenti ya Maafa.

Rais Shein ameeleza kuwa maafa yana madhara makubwa katika nchi, endapo hakutakuwa na mipango thabiti ya kukabiliana nayo na kutolea mfano namna vimbunga vya Idai, Kenneth na vinginevyo vilivyosababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbawe, Msumbiji na Comoro.

Rais Shein amefafanua kuwa maafa yanabadilisha agenda za maendeleo ya nchi mbali mbali duniani kwa sababu fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinabadilishwa matumizi kukidhi dharura za maafa kwa gharama kubwa zaidi.

Akitoa mfano wa mpango wa Sendai wa kukabiliana na maafa ambao unaonesha kati ya mwaka 2015 hadi 2018 nchi za Afrika zimekubwa na matukio 160 ya maafa ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Ameeleza kuwa mpango huo unaonesha kuwa zinahitajika Dola za Marekani bilioni 3700 ili nchi zilizoathirika ziweze kurejesha hali yake ya kawaida. “Kiasi kikubwa hiki cha fedha kinatumika kujenga upya miundombinu iliyoharibika badala ya kujenga miundombinu mipya”, Rais Shein alisema.

Rais wa Zanzibar amewambia wajumbe wa mkutano huo hatua zilizo fanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha uhimili wa kukabiliana na maafa, kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni miongoni mwa visiwa ambavyo hupata madhara ya maafa.

Hatua hizo ni pamoja na kuandaa Sera ya kukabiliana na maafa ya mwaka 2011 na sheria yake ya mwaka 2015, kuanzisha Kamisheni inayoshughulikia masuala ya maafa na mpango wa mawasiliano wakati wa maafa. 

Aidha, amebainisha hatua nyingine kuwa ni pamoja na mpango wa elimu ya kujikinga na maafa kwa wanianchi, kuimarisha vyombo vya usafiri wa baharini ikiwemo ununuzi wa meli mbili kubwa za MV. Mapinduzi II ya abiria na MV. Ukombozi II kwa ajili ya kubeba mafuta, ujenzi wa vituo vitatu vya uokozi, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufuatilia usafiri wa majini ikwemo ndege zisizokuwa na rubani na boat za uokoaji na kuzimia moto.

Dkt. Shein amesema ili kukabiliana na maafa ya mafuriko ambayo huwa yanakikumba kisiwa hicho kutokana na mvua za mwezi Oktoba hadi Desemba na mwezi Machi hadi Juni, nchi hiyo kwa msaada wa Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) imejenga kituo cha kuhifadhi watu wanaoathirika na mafuriko ambacho kina nyumba 30 zenye miundombinu yote kwa ajili ya maisha ya mwanadamu.

Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua mkopo wa Dola za Marekani milioni 93 kwa ajili ya ujenzi wa mitaro inayopeleka maji baharini wakati wa mafuriko. Ujenzi huo ambao upo katika hatua za mwisho utakapokamilika, Dkt. Shein aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa, Zanzibar itaweza kuepuka mafuriko au Kupunguza kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenista Muhagama (Mb)ameeleza kuwa malengo ya kuanzishwa kwa Kamati ya Mawaziri wenye Dhamana ya Maafa likiwemo lengo la kulishauri Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC namna ya kupunguza madhara ya maafa. Alisema maafa yaliyosababishwa na majanga ya vimbunga vya Idai na Kenneth katika nchi za SADC, ukame na mafuriko ambayo hayana mipaka yamedhihirisha umuhimu wa nchi hizo kuwa na mpango wa ushirikiano wa kukabiliana na maafa.

Alieleza ili kwenda sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli itaendelea kuimarisha uwezo wake wa usimamizi wa maafa katika Nyanja zote. 

Amebainisha hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Madhara ya Maafa; kuandaa Wasifu wa Janga la Mafuriko na Ukame; kuandaa Mpango wa Dhamira ya Taifa wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi; kuandaa Mfumo wa Taifa wa Ufuatiliaji wa Taarifa za Gesi Joto;  Kuandaa Mipango ya Kukabiliana na Dharura za Afya ya Binadamu, Mifugo na Wanyama; kuandaa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya Kuvuna.

Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena Tax aliwambia wajumbe wa mkutano huo kuwa majanga hayataki urasimu yanapotokea, yanahitaji hatua za haraka na zinazoeleweka ili kuyakabili ipasavyo kabla hayajasababisha madhara makubwa.

Dkt. Tax alifafanua kuwa mkutano huo kufanyika Zanzibar ni fursa nzuri kwa nchi za SADC kujua vizuri muungano wa Tanzania na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka mingi sasa. Aidha, alisema itakuwa fursa nzuri kwa nchi hizo kujionea vivutio vya kipekee vya kisiwa cha Zanzibar ambacho kina umaarufu mkubwa duniani kote.

Serikali ya Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika baada ya Tanzania kuchukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa jumuiya kuanzia mwezi Agosti, 2019 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, mwaka huu (2020).  Hatua hii inatokana na utaratibu wa kawaida wa mzunguko wa kushika nafasi hiyo kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
MWISHO.