Saturday, February 28, 2026

WATU WENYE ULEMAVU WAJIKWAMUA KIUCHUMI KWA MIKOPO YA SERIKALI

 


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, amekutana na kundi la watu wenye ulemavu katika ziara iliyowakutanisha na  wanufaika wa mikopo ya 10% ya mapato ya Halmashauri (2% kwa wenye Ulemavu) na wale ambao wameomba na hawajapata.

Ziara hiyo imelenga kujadili maslahi,Fursa na changamoto mbalimbali za watu wenye ulemavu tukio hilo limefanyika, katika Ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri Wilaya ya Moshi.

"Ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa upendo kwa kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa mikopo kwa watu wenye ulemavu na ninawahimiza watu wenye ulemavu kuchangamkia Fursa hizo na kujitokeza katika kupata zabuni za tenda za serikali kwa mfumo wa manunuzi ya umma (30% kwa watu wenye ulemavu) zinazotolewa ili kuwaletea tija na kujikwamua kiuchumi". Amesema hayo Naibu Waziri Mhe. Nderiananga.

Pia, ameautaka Uongozi wa Wilaya ya Moshi kuhakikisha unaeaendelea  kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwapa Fursa za Tenda za manunuzi ya ndani kwa makampuni ya vikundi vya watu wenye ulemavu ili kuwasaidia watu wenye ulemavu kuondoka kwenye umaskini.

Aidha, amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Moshi na Uongozi wote  kwa kukata kiu ya Mheshimiwaa Rais ya kuwasikiliza wananchi na kuwaletea faraja Watanzania kwa kutoa mikopo ya Asilimia 2% kwa kiwango cha 98% yaani shilingi 60.4M, pia hata wale ambao bado hawajanufaika wameondoka hapa wakiwa na Matumaini.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe.Godfrey Mzava ameihakikishia jamii ya watu wenye ulemavu kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwasaidia na kuwakwamua kiuchumi.

Ameongeza kuwa, Serikali iko tayari kushirikiana na Jamii na Vyama vyote vya watu wenye ulemavu na itatetenga eneo maalumu la biashara kwaajili ya watu wenye ulemavu ili wafanye biashara zao vizuri.

Nae, Bw. Mwacha, Mlemavu wa viungo na mnufaika wa Mkopo aliemaliza deni lake amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwapa vipaumbe na kuahihidi kuendelea kuhamasishana na kuelimishana kuhusu umuhimu wa mikopo hii ili kutoka kwenye dhana ya utegemezi.







Friday, February 27, 2026

MRADI WA JNHPP KICHOCHEO MUHIMU KATIKA ZA FURSA ZA KIUCHUMI NA KIJAMII


 Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), tarehe 26 Februari 2026, imekagua maendeleo ya uzalishaji wa umeme katika mradi huo na kueleza kuridhishwa na usimamizi pamoja na utekelezaji wake, uliokidhi viwango vya ubora vinavyoendana na thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amesema kamati imefurahishwa na namna bwawa hilo linavyochochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza uzalishaji wa umeme unaosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayochangia kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme.

“Tumeridhishwa na jinsi mradi huu ulivyosimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Ukilinganisha na miradi mingine barani Afrika, mradi huu umejengwa kwa ubora wa hali ya juu na umeleta unafuu katika huduma ya umeme nchini. Haya ni mafanikio makubwa kwa Taifa,” alieleza Dkt. Yonazi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Petro Lyatuu, amesema mradi huo umekamilika  kwa asilimia 100 na mchango wake tayari umeanza kuonekana.

Amefafanua kuwa mwaka 2021, gridi ya taifa ilikuwa na jumla ya megawati 1,600, lakini kwa sasa uwezo wa uzalishaji umefikia zaidi ya megawati 4,000, zaidi ya mara mbili ya kiwango cha awali.

“Kwa sasa bwawa linazalisha umeme na tija yake imeonekana wazi. Kuongezeka kwa uzalishaji kumeimarisha gridi ya taifa na tunaendelea kuongeza nguvu katika sekta ya nishati kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi,” alisisitiza Bw. Lyatuu.

Aidha kwa hatua nyingine Kamati hiyo ilitembelea kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze, kinachopokea umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere na kusambaza katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Mhandisi Antony Mbushi, amesema kituo hicho kimekamilika na tayari kinafanya kazi.

Ameongeza kuwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma umefikia asilimia 71.58, huku mradi wa kusafirisha umeme kutoka Chalinze kupitia Kinyerezi hadi Mkuranga umefikia asilimia 59.76.

SERIKALI YADHAMIRIA KUMALIZA CHANGAMOTO YA USAFIRI DAR ES SALAAM


 

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa DART amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha inamaliza changamoto ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, ili wananchi waweze kupata huduma bora, ya haraka na yenye uhakika.

Akizungumza hii mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya usafirishaji jijini humo, Dkt. Yonazi amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha sekta ya usafiri wa umma.

Alisema katika ziara hiyo, kamati ilitembelea Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) pamoja na Kampuni ya Uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) na kujionea maendeleo ya uwekezaji uliofanywa.

“Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha usafiri wa Dar es Salaam unakuwa bora, wa kisasa na unaokidhi mahitaji ya wananchi. Tumejionea miundombinu iliyowekwa na jitihada zinazoendelea kuboresha huduma,” alisema.

Dkt. Yonazi alibainisha kuwa tayari kampuni zimeanza kuleta mabasi mapya, hatua itakayoliwezesha jiji hilo kuwa miongoni mwa majiji yenye usafiri wa kisasa barani Afrika. Aliongeza kuwa mabasi mengi yatatumia gesi asilia, huku Serikali ikiwa imejenga miundombinu ya vituo vya gesi ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi.

Aidha, alisema Serikali imewekeza katika mifumo ya TEHAMA itakayomwezesha mwananchi kutumia kadi maalumu kulipia nauli bila kulazimika kupanga foleni, jambo litakaloongeza ufanisi na kupunguza usumbufu.

Katika hatua nyingine, aliwahakikishia wananchi kuwa mabasi yote yaliyoharibika yatafanyiwa ukarabati na kurejea barabarani ili kuimarisha upatikanaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Bw. Said Tunda alisema lengo kuu ni kurejesha furaha kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kuwapatia usafiri wa uhakika.

Pia aliwataka waendesha daladala kuendelea kutoa huduma huku Serikali ikiendelea kufanya mazungumzo nao ili kupata utaratibu bora wa ushirikiano, hususan kwa zile zilizopewa kibali cha kutumia barabara ya mwendokasi.

Hatua hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miundombinu imara na huduma bora za kijamii.



Tuesday, February 17, 2026

SERIKALI YAENDELEZA JITIHADA KUHAKIKISHA WENYE ULEMAVU HAWAACHWI NYUMA KATIKA MAENDELEO YA TAIFA.

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amebainisha jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo  ukamilishwaji wa Mfumo tambuzi wa Kielektroniki wa taarifa za Watu wenye Ulemavu (PD-MIS).

Pamoja na mahitaji ya msingi ya Wenye Ulemavu yanayoendelea kutolewa, Serikali pia imeweka vipaumbele kwa Wenye Ulemavu katika ajira, elimu, afya sambamba na Mpango wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ambao unajumuisha Kaya za Wenye Ulemavu kama kigezo kimojawapo.

Naibu Waziri amebainisha hayo kwenye kikao na wajumbe wa Shirika lisilo la Kiserikali  Patronage Center for Persons with Disability (PPD), kilichofanyika leo katika ukumbi mdogo wa Waziri Mkuu Ngome Jijini Dodoma.



Saturday, February 14, 2026

SERIKALI YAPELEKA TABASAMU KWA WANAWAKE,VIJANA NA WENYE ULEMAVU MTWARA

Serikali kupitia Ofisi ya  Halmashauri ya Mtwara Mikindani imekabidhi vifaa saidizi na kiasi cha shilingi milioni 342 ikiwa ni jitihada ya kujikita katika utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Mkoani Mtwara, Mkindani  leo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa sera na mwelekeo wa maendeleo unaolenga kujenga uchumi jumuishi unaowawezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa.

Naibu Waziri Ummy amefafanua, “Mikopo hii inalenga kuchochea na kuinua uchumi wa chini kwenda juu sambamba na mwelekeo wa dira ya Taifa ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.”

Ameongeza kuwa, utoaji wa vifaa saidizi ikiwemo viti mwendo, magongo, fimbo nyeupe za wasioona pamoja na taulo za kike, ni utekelezaji wa sera ya kutomwacha mtu nyuma katika safari ya maendeleo, sambamba na maono ya kitaifa ya kujenga jamii yenye heshima, utu na usawa wa fursa.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Dkt. Joel Arthur Nanauka, ameweka wazi kuwa Serikali katika jitahada za kuwakwamua wananchi kiuchumi itaendelea na utekelezaji wa kuleta miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mtwara ikiwemo kuboresha Bandari ya Mtwara, ujenzi wa reli, na uboreshaji wa uwanja wa ndege pamoja na marekebisho ya miundombinu ya Barabara.

Waziri Nanauka amehimiza, “Wanufaika wa mikopo hiyo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, na kurejesha kwa wakati ili kushirikiana katika kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.”


 

Thursday, February 12, 2026

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO BAINA YA VYUO VYA ELIMU YA JUU, TAASISI ZA UTAFITI KATIKA USIMAMIZI WA MAAFA NCHINI


 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu  Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa, imefanya kikao kazi kinacholenga kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi za Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti katika eneo la usimamizi wa maafa leo Mkoani Morogoro.

Akifungua Kikao hicho Dkt. James  Kilabuko Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa niaba ya Dkt. Jim Yonazi  Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo amesema;

Lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuandaa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano na Mpango Kazi wa kuimarisha matumizi ya Sayansi, Teknolojia, Utafiti na Ubunifu katika usimamizi wa maafa kwa pamoja nchini ili kuweza kuwasaidia wananchi katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.

Aidha ameeleza kuwa, Serikali inadhamira ya kuimarisha Mfumo wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa kwa kuzingatia mzingo mzima wa menejimenti ya maafa unaojumuisha kuzuia na kupunguza madhara, kujiandaa, kukabiliana na maafa yanapotokea pamoja na kurejesha hali baada ya maafa.

Amesema Mwelekeo huu, umeainishwa wazi katika Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, (Toleo la Mwaka 2025) inayosisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na tafiti katika kufanya maamuzi na utendaji wenye ufanisi.

"Katika utekelezaji wa sera na sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu imeona umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Vyuo vya Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti nchini, Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha kuwa tafiti, mafunzo na teknolojia zinajibu changamoto zinazokabili taifa letu" amesema Dkt. Kilabuko

Pamoja na hayo, Dkt. Kilabuko amesisitiza uunganishaji wa nguvu, maarifa na rasilimali tulizonazo,  utajenga Taifa lenye ustahimilivu dhidi ya maafa na lenye uwezo wa kufikia malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Jenerali Hosea  Ndagala alisema, kikao hiki kinatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja kati ya wahadhiri, wataalam wa kitaaluma na watendaji wa Serikali kuhusu mahitaji halisi ya shughuli za usimamizi wa maafa katika ngazi ya kitaifa, mkoa hadi wilaya kwa lengo la kuongeza ufanisi wa majibu wakati wa maafa na kuboresha mikakati ya kurejesha hali baada ya maafa.



Wednesday, February 11, 2026

SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKISHWAJI JAMII YA WATU WASIOONA KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII, KIUCHUMI NA KIUTAMADUNI ILI KUONGEZA TIJA.


Serikali inatambua Breli si mfumo pekee wa kusoma, bali ni nyenzo ya kufungua milango ya elimu, ujuzi, ukarimu wa jamii, na ushiriki kamili wa kijamii.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu (SBUU) Mhe. Ummy Nderiananga kwa niaba ya Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Mhe. William Lukuvi leo Jijini Dodoma huku akieleza kuwa Mfumo huo umebadilisha maisha ya mamilioni ya wasioona na wenye uoni hafifu duniani kote ikiwemo Tanzania.

“Kwa kutambua mchango wa Jamii ya Wasioona katika maendeleo ya taifa letu, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wasioona kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati na Mipango inayojumuisha huduma na teknolojia ya breli pamoja na kuimarisha elimu jumuishi kwa kuanzisha na kuendeleza shule na vituo maalum kwa wanafunzi wasioona, pamoja na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya Breli, vitabu maalum na teknolojia saidizi” amefafanua Mhe. Waziri.

Aidha, Serikali imetenga madirisha maalum ya huduma kwa watu wenye ulemavu katika vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za uchunguzi, tiba na utengamao kwa watu wenye ulemavu wakiwemo wasioona.

Vilevile, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kubuni na kutekeleza miradi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, mafunzo ya ujuzi na ajira kwa watu wasioona.

“Tunapoadhimisha kilele cha Siku ya Kimataifa ya Breli Duniani nitoe wito kwa kila mwananchi, taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kiraia pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha mazingira jumuishi, kuondoa vikwazo vya kijamii na kimazingira, na kuweka mifumo wezeshi itakayohakikisha Ustawi na Maendeleo ya jamii ya wasioona yanatimizwa kikamilifu. Kwa kufanya hivyo, Taifa letu litaendelea kujenga jamii yenye usawa, haki na mshikamano, inayothamini mchango wa kila mmoja bila ubaguzi” ameomgeza Mhe. Nderiananga

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Breli huadhimishwa tarehe 12 Februari ya kila mwaka kwa lengo la kutoa nafasi kwa mataifa yote kutafakari kuhusu mchango na nafasi ya teknolojia ya Breli katika kuwawezesha watu wasioona kushiriki kikamilifu katika elimu, ujuzi na maendeleo ya taifa. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Teknolojia ya Breli Husaidia Kuchochea Maendeleo kwa Wasioona na Ujenzi wa Taifa” na kwa Tanzania maadhimisho hayo yatafanyika katika Halmashauri zote na kwa ngazi ya Kitaifa yatafanyika mkoani Tanga. 

 

Breli ni mfumo ulioasisiwa na ndugu Louis Braille, ambaye alibuni njia ya maandishi inayowawezesha watu wasioona kusoma, kuandika na kupata elimu na habari kwa usawa na wale wanaoona. Mfumo huu unawapa watumiaji wa Breli fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kifikra. Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Breli.

TGPA YAPOKEA UGENI WA WACHAPISHAJI KUTOKA UGANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO

 


Wakala wa Serikali wa Uchapishaji Tanzania (TGPA) leo umepokea ugeni wa watu 24 kutoka Shirika la Uchapishaji la Uganda (Uganda Printing and Publishing Corporation – UPPC) waliowasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchapishaji wa serikali.

Ujumbe huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UPPC, Profesa Joackim Buwembo, ukijumuisha wajumbe wa bodi, Mpigachapa Mkuu wa Serikali ya Uganda, Profesa Sudi Nangoli, pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali za shirika hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za TGPA, ziara hiyo imelenga kujifunza na kubadilishana uzoefu katika uchapishaji wa nyaraka za serikali, hususan Gazeti la Serikali, pamoja na uchapishaji wa nyaraka zenye alama za usalama (security printing).

Katika ziara hiyo, pande zote mbili zimefanya vikao vya kitaalamu na majadiliano yaliyolenga kuimarisha mifumo ya uchapishaji, kuongeza ubora wa huduma na kuzingatia viwango vya usalama katika uchapishaji wa nyaraka nyeti za serikali.

Aidha, TGPA na UPPC zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya uchapishaji, kuandaa mafunzo kwa watumishi wao, pamoja na kuanzisha utaratibu wa kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuimarisha mahusiano ya kitaasisi kati ya Tanzania na Uganda.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za taasisi hizo kuendeleza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uchapishaji wa serikali na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.