*Aagiza
akiba iliyopo itunzwe hadi msimu ujao wa mavuno
* RC,
Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo
iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi
ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa
Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo
hicho.
Waziri
Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika
mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua
ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.
“Angalieni
ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza
kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo
(jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza
kunyauka.”
“Kama
mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija
hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED
toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni
waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi
kikubwa cha chakula,” alisisitiza.
“Msiruhusu
kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee
kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja
wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba
msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini
hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani
ya sh. bilioni 5.28.
Alisema
kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo
inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote
nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.
“Kanda
ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka.
Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa
Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa
kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.
“Kanda
ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili
yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani
56,000 mradi huu utakapokamilika.”
Alisema
kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa
kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.
Alipolizwa
ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma
alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani
wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni
Julai mosi kila mwaka).
“Kuimarika
kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo
kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia
sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.
Alisema
changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima
ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula
na biashara. “Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka
zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,”
alisema.
Waziri
Mkuu leo anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme
katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia
atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia
mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.