WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji safi na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi
lita 200,000 ambao utahudumia vijiji viwili vya Mkongotema na Magingo katika
kata ya Mkongotema, wilayani Songea, mkoani Ruvuma.
Akisoma
taarifa ya mradi huo kwa Waziri Mkuu jana (Alhamisi, Januari 5, 2017),
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Bw. Shafi Mpenda alisema mradi huo
ulioanza kujengwa mwaka 2013, umegharimu sh. bilioni 1.09.
“Hadi
kukamilika kwake, mradi huu umegharimu sh. 1,092,439,812 ambapo kati ya hizo
sh. 1,069,647,312 zimetolewa na Serikali kuu na sh. 22,792,500 zimechangwa na
wananchi,” alisema.
Bw. Mpenda
alisema mpaka sasa kaya 915 zenye watu 5,300 zinahudumiwa na mradi huo wenye
vituo 57 vya kutolea huduma za maji kwa jamii. Alisema lengo lao ni kufikisha
vituo 71 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Akifafanua
zaidi, Bw. Mpenda alisema kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuwapunguzia
wananchi gharama za kununua maji ambapo pipa moja liligharimu sh. 3,000. “Pia
kutasaidia kupunguza adha ya kufuata maji umbali mrefu; kupunguza magonjwa
yanayotokana na mlipuko na kuwapa wananchi muda wa kutosha kufanya shughuli
nyingine za maendeleo,” alisema.
Akizungumza
na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu aliwapongeza
wakazi hao kuwa kukubali kuchangia ujenzi wa mradi huo kwani katika baadhi ya
maeneo miradi kama hiyo imekwama kukamilika kwa sababu wananchi waligomea
kuchangia.
Aliwataka
wakazi wa vijiji hivyo wasiharibu mazingira na watunze vyanzo vya maji ili
mradi huo uweze kuwa endelevu. “Mradi huu ni lazima tuutunze kwani hali ya hewa
imebadilika sana hivi sasa, sababu ni sisi wenyewe wananchi ambao tumekata miti
sana ili kupanua maeneo ya kilimo.”
“Changamoto
inayotupata hivi sasa ni kwama tumebakia kuwa na eneo kubwa la kilimo lakini
mazao yanayopatikana ni kidogo. Mtazamo wetu katika Serikali hivi sasa ni
kulima kwenye eneo dogo lakini mavuno yawe mengi,” alisema.
“Mtu asilime
chochote karibu na chanzo hiki ili tuweze kukitunza chanzo chetu. Na wenyeviti
wa Serikali za vijiji vyote viwili, wekeni utaratibu wa wananchi kwenda kupanda
miti ili eneo hili libaki kuwa na unyevunyevu kwa muda mrefu,” alisisitiza.
“Sera ya
Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji katika umbali usiozidi
mita 400, na hili tutaweza kulitimiza kama tu mtatunza vyanzo vya maji
vilivyopo,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo kuwaomba wakazi wa vijiji hivyo watunze akiba ya chakula
walichonachi kwa sababu hali ya hewa imebadilika na hakuna anayejua mvua
itaanza kunyesha lini. “Hatujui mvua itakuja lini na kwa kiasi gani; mara
zitakapoanza kunyesha kila mmoja katika familia ahakikishe analima mazao
mbadala kama kunde, maharage na mihogo ambayo yanastahimili ukame,” alisema.
Waziri Mkuu
pia alikagua utoaji huduma kwenye kituo cha afya cha madaba na ujenzi wa kituo
cha kupozea umeme cha Madaba.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.