Monday, February 20, 2017

MSIOGOPE KUKOPA, ASEMA WAZIRI MKUU


*Asisitiza dawa ya deni, kulipa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wakubwa na wadogo wa miwa kwenye kiwanda cha sukari cha Manyara wachukue mikopo kama wanataka kuendeleza kilimo hicho.

Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Februari 19, 2017) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho pamoja na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani katika kijiji cha Matufa wilayani Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara.

“Mkurugenzi wenu amesema hapa kuwa ni vigumu kwa wakulima kupata mikopo na pia mikopo ya benki ina riba kubwa. Napenda niwasisitize kuwa msiogope kukopa kwa sababu hakuna tajiri duniani aliyeendelea bila kukopa,” alisema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwakumbusha wakulima hao kwamba wakishakopa, wasisahau kuwa dawa ya deni ni kulipa.

Aliwaeleza kuwa zipo benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima ambazo ni Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), NMB, CRDB, Benki ya Kilimo (TADB) na Benki ya Rasilmali (TIB). “Benki ya Kilimo TADB inatoa mikopo kwa wakulima na pia Benki ya TIB, Kuna TIB Corporate na TIB Development,” alisema.

Aliwataka wakurugenzi wa kiwanda hicho waharakishe uagizwaji wa mitambo mipya ili kiwanda hicho kiweze kuongeza uzalishaji wake. “Napenda niwahakikishie wakurugenzi kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kulinda viwanda vya ndani. Tunataka muongeze uzalishaji ili kufidia pengo lililopo. Tutaruhusu waagizaji walete suakri kutoka nje baada ya kujiridhisha kuwa uzalishaji wa ndani umejitosheleza,” alisema.

Alisema takwimu za mahitaji ya sukari hapa nchini zinapaswa kupitiwa kwa sababu hazitoi picha halisi. “Tanzania ina watu milioni 50 lakini mahitaji ya sukari tunaambiwa ni tani 420,000 kwa mwaka. Wenzetu wa Kenya wako milioni 45 lakini mahitaji yao ni tani 800,000 kwa mwaka. Tulishawaambia wapiti upya hizi takwimu zao.”

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Mahusiano wa kiwanda hicho, Bw. Dipak Odedra alisema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2006 kikiwa na uwezo mdogo wa kusaga tani 50 za miwa kwa siku lakini sasa kina uwezo wa kusaga tani 500 kwa siku.

“Kuongezeka kwa uzalishaji na kukua kwa kiwanda kumechangiwa na mikataba ya kuwashirikisha wakulima wadogo kuwakopesha mitaji tangu kutayarisha mashamba, kupanda mbegu, usafiri na utaalamu lengo likiwa kununua miwa yao inapokuwa tayari kuvunwa,” alisema.

Alisema mpango huo shirikishi wa kupanda miwa unahusisha vijiji zaidi ya 10 ambapo jumla ya ekari 1,150 zinalimwa na wakulima wadogo waliohamasika na kuona faida za kilimo hicho.

Alisema mwaka jana kiwanda hicho kilisaga tani 64,584 za miwa na kuweza kuzalisha tani 4,251 za sukari. “Kwa msimu ujao baada ya kufunga mitambo ya kisasa, tumepanga kuongeza uzalishaji ili tuweze kusaga tani za miwa 650 kwa siku kutoka tani 500 za sasa. Na mwaka kesho (2018) tunataraji kufikisha tani 750 za miwa kwa siku,” aliongeza.

Akigusia changamoto zinazowakabili, alisema wanaiomba Serikali iwawezeshe kupata mikopo yenye riba nafuu ili waweze kufikia malengo yao kwa haraka zaidi na akagusia sula la wakulima wadogo kunyimwa mikopo kutoka benki za biashara.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.