Monday, February 6, 2017

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA AJIRA KWA VIJANA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali imejipanga kusaidia vijana kutambua na kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira zilizopo nchini ili kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na  kutimiza adhma ya kuleta maendeleo hususani kwa vijana.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo jana wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Kinondoni Mhe. Maulid Mtulia iliyohoji juu ya jitihada za Serikali katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wakati wa Mkutano wa Tano wa Bunge unaoendelea Mkoani Dodoma.

Katika Mkutano huo Mhe. Waziri alisisitiza kuwa Serikali ina mipango na mikakati madhubuti inayokusudiwa yakusaidia vijana wa Kitanzania ili kujiletea maendeleo yao wenyewe na kuondokana na umasikini.

Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuweka mikakati ikiwemo uwanzishwaji wa programu mbalimbali zitakazo saidia kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuangalia matokeo ya tafiti mbalimbali ambazo zimepelekea kuwa na programu zinazolenga kukabili tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana” Alisema Waziri

Alisisitiza kuwa programu hizo ni pamoja na; kurasmisha ujuzi usio rasmi kuwa rasmi, mfumo wa mafunzo kwa vitendo, mfumo wa uanangezi pamoja na kukuza mafunzo kwa watanzania kulingana na soko lililopo kwa sasa.

Pamoja na juhudi hizo zinazotarajiwa kuzaa matunda bado Waziri aliwatoa hofu wananchi wote kwa kuwepo kwa fursa hizo za ajira zitakazo jali hali za watu pasipo kuangalia makabila yao, rangi wala dini.

“Katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana hatuta angalia kabila, rangi wala dini ya mtu bali kutakuwa na haki na usawa”.Alisisitiza Waziri

Aliongezea kuwa, Serikali pia inajitihada za kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ili kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira.

“Serikali itatumia sekta zenye uwezo wa kutoa ajira kwa wingi ikiwemo zile za Kilimo, majenzi, Mawasiliano na Utalii ili kuzitumia kuweka mazingira mazuri kwa vijana kupata fursa za ajira”.

Mhe. Mhagama alisisitizia bungeni kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika zitatumika kama chachu ya kuangalia maeneo yanayohitaji kusaidia kwa haraka na kupunguza changamoto hiyo kwa vijana.

“Kwa kuangalia tafiti ya Hali ya Ajira Nchini ya mwaka 2014 imeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3 mwaka 2014 na ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014”,alisema.

Hata hivyo, Waziri Mhagama alieleza kuwa pamoja na jitihada hizo Serikali bado ina wajibu wa kuongeza jitihada zaidi ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa ajira na kuboresha maisha ya vijana.

==Mwisho==

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.