WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha wanatumia uwakilishi
wao kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu
la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 7, 2017) alipokutana na mabalozi
wa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italy,
Ufaransa, Jamuhuri ya Kidemkrasi ya Congo (DRC) na Uswisi.
Mabalozi
hao ni Balozi Dk. Emmanuel Nchini (Brazil), Balozi Elizabeth Kiondo (Uturuki),
Balozi George Madafa (Italy), Balozi James Msekela (Uswisi),Balozi Samuel
Shelukindo (Ufaransa), Balozi Paul Mella (DRC), Balozi Mbelwa Kairuki (China).
“Serikali
inahitaji watu wa kuja kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao
kabla ya kuyauza nje ya nchi, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha tunapata
wawekezaji wenye sifa,” amesema.
Pia
Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kutumia uwakilishi wao katika nchi hizo kwa kuhakikisha
wanatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii
wanaokuja Tanzania.
“Tulinde
bidhaa za ndani ya nchi yetu mfano madini ya tanzanite ambayo yanazalishwa Tanzania
pekee lakini leo zinazalisifiwa nchi nyingine kwa uzalishaji huo zikiwemo India
na China, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha mnatangaza madini yetu ipasavyo,”
amesema.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao
kulinda maslahi ya Taifa katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuimarisha
uhusiano uliopo kati ya Tanzania na mataifa hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao
kuhakikisha wanawatambua Watanzania wanaoishi katika mataifa hayo na
kushirikiana nao katika kutafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini.
Kwa
upande wake Balozi Mella ambaye alizungumza kwa niaba ya mabozi wenzake
alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watakwenda kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.