Tuesday, April 18, 2017

NEEC FANYENI TATHMINI YA KISAYANSI KUHUSU MANUFAA YA MIFUKO YOTE YA UWEZESHAJI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wanachama wa kikundi cha Juhudi kinachojishughulisha na usindikaji vyakula kabla ya kufungua maonyesho ya Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi ya Serikali kwenye uwanja wa  Mashujaa mjini Dodoma Aprili 18, 2017. 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelitaka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), lianze kufanya tathmini ya kisayansi kuhusu manufaa ya Mifuko yote ya uwekezaji nchini ili kujiridhisha endapo inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Pia amelitaka baraza hilo lifanye tathmini kuhusu namna ya kuunganisha mifuko hiyo bila ya kuathiri majukumu ya msingi na mantiki ya kuanzishwa kwake, ili inayofanya kazi zinazofanana iunganishwe .

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Aprili 18, 2017) wakati akifungua maonesho ya mifuko ya uwezeshaji katika uwanja wa Mashujaa mjini Dodoma. Amesema uzinduzi wa maonesho hayo ni fursa nzuri kwa wananchi kuweza kudadisi kuhusu huduma zitolewazo na Mifuko hiyo na kutoa ushauri, ili kuboresha huduma.

“Lengo ni kuwa na Mifuko michache, lakini inayobadilisha maisha ya wanufaika, ambao ni wananchi. Nitafurahi kupata taarifa hiyo kabla au ifikapo Mwezi Mei, 2018,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi yanayofanywa na Serikali yanalenga kuwawezesha Watanzania wengi wafanye  shughuli za kujiongezea kipato bila kusumbuliwa na baadhi ya Watumishi wasio waadilifu. 

Ameongeza kuwa “uwezeshaji wananchi kiuchumi ni jambo ambalo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 - 2020/2021,”.

Amesema kuwawezesha wananchi kiuchumi, sio ubaguzi wala upendeleo, bali ni jitihada za makusudi za kuwashirikisha wananchi walio wengi ambao kwa sababu za kihistoria, wamejikuta wakiwa nje ya mfumo rasmi wa kiuchumi, hivyo kubaki kwenye hali duni jambo ambalo ni hatari kwa ustawi na usalama wa nchi.
Waziri Mkuu amesema jitihada za uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizoanza tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza na kuendelezwa na awamu zote zilizofuata, ambapo kwa sasa kuna mifuko 19 ya kuwezesha wananchi kiuchumi.

Amesema mifuko hiyo imesaidia upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na kupunguza kiwango cha umaskini nchini. “Hadi kufikia mwaka 2016 Mifuko hiyo kwa pamoja ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 1.759 kwa wajasiriamali 400,000.

Awali Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi. Beng` Issa alisema maonesho hayo ya siku nne yatawezesha kuwaongezea wananchi uelewa juu ya shughuli zinazofanywa na mifuko ya uwezeshaji.

Amesema kati ya mifuko 19 ya uwezeshaji mifuko 13 imeweza kushiriki katika maonesho hayo ya kwanza kufanyika nchini, ambapo kauli mbiu ya maonesho hayo ni “Wezesha wananchi kiuchumi ili kujenga uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda”

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TPB Bank PLC, Bw. Sabasaba Moshingi aliyezungumza kwa niaba ya washiriki alisema madhumuni ya maonesho hayo ni kukuza uelewa juu ya uwepo wa mifuko ya kuwezesha wananchi kiuchumi na fursa zitolewazo na mifuko hiyo.

Pia kuhamasisha wananchi juu ya kujijengea utamaduni wa kujiwekea akiba na kuwekeza katika miradi yenye kuleta faida pamoja na uanzishwaji na uimarishwaji wa vikundi na miradi ya kiuchumi ili kuunganisha wananchi na fursa za huduma ya mikopo, mafunzo na huduma nyingine zinazotolewa na mifuko hiyo.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.