*Asema waliouza eneo la hifadhi wawajibishwe
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Majid
Mwanga aende kata ya Saadani na kukaa na uongozi wa vijiji
vinavyozunguka hifadhi ya Saadani ili watambue kwa pamoja mipaka
iliyowekwa na Serikali.
Waziri
Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya
Saadani na Matipwili wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani ambao walisimamisha
msafara wake wakati akitoka Hifadhi ya Taifa ya Saadani kukagua
miundombinu.
“Mkuu
wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Ardhi njoo na ramani yako na Mhifadhi Mkuu
naye aje na ramani yake, kaeni na Mwenyekiti wa Kijiji na kamati yake
ya ardhi; muende beacon kwa beacon kwa kutumia kifaa cha
GPS ambacho kitawaongoza kubainisha huo mpaka umepitia wapi. Nahitaji
kupata taarifa kuhusu jambo hili kuwa limetekelezwa,” alisema.
Alisema
anazo taarifa kuwa baadhi watu kwenye kijiji hicho wamewauzia ardhi
wakazi kutoka Dar es Salaam wakati wakijua kuwa ardhi hiyo ni mali ya
hifadhi ya Saadani. “Hao watu wasakwe na wafikishwe kwenye vyombo vya
sheria kwa sababu hakuna mtu anayeruhusiwa kuuza ardhi ya hifadhi,”
alisisitiza.
Alisema
mikoa, wilaya, vijiji kila kimoja kina mipaka yake ambayo inatambulika
na ilikwishatolewa kwenye gazeti la Serikali. “Vijiji vyote vina mipaka
ambayo inatambulika rasmi na ramani zake ziko ofisini kwa Mkuu wa Mkoa
kikiwemo na hiki kijiji chenu. Lakini baadhi ya vijiji vina maeneo ya
hifadhi. Tunataka mtambue kuwa mipaka hiyo ipo rasmi, na kwamba inapaswa
iheshimiwe,” aliongeza.
Waziri
Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuwa alilazimika kupita Saadani wakati
akitokea Wami, ili aweze kufuatilia ni kwa nini hifadhi hiyo haitangazwi
vya kutosha wakati iko karibu na Dar es Salaam na watalii wengi
wanapita hapo wakati wakirudi makwao.
“Serikali
imenunua ndege za kuleta watalii wengi zaidi nchini lakini hadi sasa ni
mbuga zilezile ambazo zinapata watalii. Tunataka mbuga hii iliyoko
karibu na Dar es Salaam itangazwe na ijulikane zaidi ili wale ambao
hawana muda wa kwenda mikoa ya mbali waje hapa na kuona rasilmali
tulizonazo,” aliongeza.
Hifadi
ya Saadani ambayo iko umbali wa km. 45 kutoka Bagamoyo na km. 100
kutoka Dar es Salaam, ina mvuto wa kipekee kwani ndiyo hifadhi pekee
unayoweza kuona wanyama wakijivinjari katika fukwe za Bahari ya Hindi
kwa vile imeunganisha nyika na bahari.
Hifadhi
hiyo iko kati ya mikoa ya Pwani na Tanga, katika wilaya za Bagamoyo na
Pangani, ikiwa na ukubwa wa zaidi ya km. za mraba 1,000, ikijumuisha
maeneo ya Mkwaja na misitu ya Zaraninge na Tumbirini.
Katika
ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikuwa amefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa
pwani, Eng. Evarist Ndikilo, viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na Mbunge
wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.