Thursday, May 11, 2017

HUDUMA ZA AFYA ZISIFUNGWE WAKATI WA ZOEZI LA USAFI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali waweke utaratibu utakaoruhusu huduma za afya kuendelea kutolewa kwa wananchi katika maeneo yao hata kama zoezi la usafi la kila mwezi litakuwa linaendelea.

Serikali imeweka utaratibu wa wananchi kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi, zoezi ambalo linashirikisha watu wote wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma nyingine zoezi linalofanyika kuanzia saa 12.00 asubuhi hadi saa 4.00 asubuhi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 11, 2017) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ulega mbunge wa Mkuranga.

Mheshimiwa Ulega alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu maeneo ya kutolea huduma mbalimbali zikiwemo za afya ambayo hufungwa wakati wa zoezi la usafi linalofanyika kila mwezi nchini, jambo linalosababisha kero kwa wagonjwa na wengine wenye dharula.

Waziri Mkuu amesema “Hospitali na maeneo mengine ya kutolea huduma za afya hayawezi kufungwa, viongozi wa maeneo husika waweke utaratibu mzuri utakaoruhusu huduma hizo ziendelee kutolewa bila ya kuathiri zoezi la usafi wa mazingira,”.

Katika hatua nyingineWaziri Mkuu amesema Serikali imeagiza tani 131,000 za sukari ili kukabiliana na upungufu uliopo nchini. Amesema Serikali iko macho na inajua maeneo yanayohitaji kuboreshwa kulingana na mahitaji.

 “Mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 420,000, ambapo tunazalisha tani 320,000, hivyo tunaupungufu wa tani 100,000 hata hivyo tumeagiza tani 131,000 na tayari tani 80,000 zimewasili nchini, ambapo kati yake tani 35,000 zimeingizwa sokoni,” amesema.

Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub aliyetaka Serikali iwahakikishie wananchi upatikanaji wa sukari hususan katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.