WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ina mkakati wa kufanya Majiji yote nchini
yawe na barabara za viwango vya kimataifa na zinazopitika kwa urahisi.
“Tumeanza
kujenga barabara za kisasa katika jiji la Arusha ambalo ni jiji la utalii,
tutakwenda Mwanza na Dar es Salaam kwa kujenga barabara zenye njia za juu
(flyovers) zikiwemo za magari na za waenda kwa miguu,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Mei 4, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa
Tengeru, wilayani Arumeru, mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya
Sakina-Tengeru yenye urefu wa km. 14.1 ambayo itakuwa na njia nne za magari.
“Nimekuja
kukagua ujenzi wa barabara hii ya Sakina hadi Tengeru lakini mkandarasi
akimaliza anajenga barabara nyingine ya kilometa 42.1 na hivyo hapa Arusha
tutakuwa na kilometa 56.5 za awamu ya kwanza,” alisema.
Alisema
maboresho ya barabara za Jiji la Arusha yanafanyika ili kuwezesha
wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na viwanda vitakapoanza
kujengwa, itakuwa hawana shida ya mawasiliano.
Akizungumzia
tatizo la uhaba wa ardhi ambalo liliibuliwa na mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw.
Joshua Nassari, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo
aendelee na zoezi la kuuzungukia mkoa wake ili kubaini maeneo yenye matatizo
sugu.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa
barabara hiyo kwa Waziri Mkuu, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng.
Mgeni Mwanga alisema ujenzi wa barabara hiyo ambao ulianza Juni 2015,
unatarajia kukamilika Juni 2018.
“Ujenzi
wa barabara ya Sakina –Tengeru ni wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara
yenye urefu wa km. 230 ya kutoka Arusha - Holili - Taveta - Voi ambayo ujenzi
wake unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 139.34. Ujenzi huo unagharimiwa na Serikali
ya Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Sambamba
na barabara hiyo, Eng. Mwanga alisema mkandarasi wa barabara hiyo ataanza
kujenga barabara nyingine ya km. 42.1 inayoanzaia Usa River hadi Kisongo kwa
kiwango cha lami ambayo itakuwa na madaraja saba wakati ile ya Sakina hadi
Tengeru ina madaraja makubwa mawili.
Naye
mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari alisema uhaba wa ardhi bado ni
tatizo kubwa kwenye wilaya hiyo kiasi kwamba hawana hata eneo la kujenga shule
au zahanati.
“Maeneo
yote yameuzwa na wenyeviti wa vijiji na madiwani, hivi sasa ukitaka kujenga
shule au zahanati hakuna eneo hata moja. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba
utusaidie kufuatilia suala hilo licha ya kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya
Makazi alishakuja na kuelezwa hali halisi ilivyo,” alisema.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.