Thursday, June 29, 2017

MAJALIWA: ZUIO LA USAFIRISHAJI CHAKULA NJE LIKO PALE PALE


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali wa kuzuia usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi uko pale pale.

Pia amesema mahindi iliyokamatwa mkoani Kilimanjaro yakisafirishwa kwenda nje ya nchi yataingizwa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na magari yatabaki polisi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo ( Alhamisi Juni 29, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri  Mkuu wakati akijibu swali la Mheshimiwa Ritha Kabati  (Viti Maalumu) aliyetaka ufafanuzi kuhusu zuio la kusafirisha mazao nje ya nchi kwa mikoa yenye chakula cha ziada.

“Tumedhibiti na kuzuia usafirishaji wa chakula hasa mahindi kwenda nje ya nchi ili kuliepusha Taifa kukumbwa na baa la njaa kutokana na baadhi ya mikoa kutopata mavuno ya kutosha,”

“Kuna maeneo kama ya Sengerema na Geita mahindi yamekauka, hivyo bado tuna upungu wa chakula. Na hata bei ya chakula ipo juu, hatuna namna nyingine zaidi ya kudhibiti utokaji wa chakula kwenda nje na nawasihi wananchi tushirikiane katika jambo hili,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kama kunaulazima wa kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi  wahusika wakaombe kibali katika Wizara ya Kilimo,  Mifugo na Uvuvi na kibali kiwe cha kusafirisha unga na si mahindi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema watumishi wote wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Mkuu Dodoma (CDA) waliokuwa wanaolalamikiwa na wananchi kutokana na utendaji wao wataondolewa wakati wenzao wakihamishiwa Manispaa ya Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na ukaguzi na uhakiki wa kina kwenye masuala ya fedha na utumishi ili waweze kujua CDA ilipovunjwa iliacha fedha kiasi gani na shughuli zake zilifikia hatua gani ili ziendelezwe.

Amesema majukumu yote ya CDA yatafanywa na Manispaa ya Dodoma na baada ya kukamilisha utaratibu huo mpango kazi wote utaendelea kama ulivyopangwa.Kuhusu waliolipia viwanja watakabidhiwa mara baada ya kukamisha utaratibu huo.


Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali la Mheshimiwa Matha Malata (Viti Maalumu) aliyetaka kupata tamko la Serikali kuhusu wananchi ambao waliolipia viwanja CDA ambao bado hawajakabidhiwa.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.