WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Misungwi, Bw. Eliud Mwaiteleke aitishe kikao na
wananchi wa Kigongo na kutafuta ufumbuzi wa tatizo la eneo la kujenga
soko.
Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza
na mamia ya wakazi na wajasiriamali wanaotumia kivuko cha feri cha Kigongo
waliokuwa wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema.
"Mkurugenzi haya mambo ya mipango, mipango na kupanga hayaleti tija
kwa wananchi. Hivi hamjui kuwa wananchi wanahitaji kuwa na soko katika eneo
hili ili waweze kuuza mazao yao au samaki?"
"Ninakuagiza Mkurugenzi, kesho Alhamisi, saa 4 njoo na Afisa
Biashara wako, Mwenyekiti wa kijiji na watu wako pamoja na Diwani wa hapa,
itisheni kikao na muonyeshwe eneo la soko ili mliingize kwenye mipango
yenu," alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za
michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.
Awali, Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi huyo ili aeleze amejipanga vipi kwenye
Halmashauri yake kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo.
Akitoa majibu mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Mwaiteleke alisema hawajawahi
kupata mpango kutoka kwenye kata hiyo na kwa hiyo akawasihi wananchi waibue
mpango huo na kuuwasilisha kwenye Halmashauri ili wao waweze kutenga fedha za
kujenga soko.
Mapema, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Bw. Sebastian Kisumo alimweleza
Waziri Mkuu kwamba eneo hilo linakabiliwa na tatizo la soko pamoja na uhaba wa
maji.
Kuhusu maji, Waziri Mkuu alisema Serikali imetenga sh. bilioni 2.5
kwa ajili ya mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao
utasambaza maji kwenda Misungi, Usagara hadi Kigongo Feri.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.