WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameungana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, viongozi waandamizi
wa Serikali na mamia ya wananchi kuuaga mwili wa aliyekuwa Karani wa Baraza la
Mawaziri Bw. Hassan Shebuge.
Marehemu Bw. Shebuge ameagwa
leo (Ijumaa, Julai 7,2017) nyumbani kwake Mbagala- Majimatitu jijini Dar es
Salaam na anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumamosi, Julai 8, 2017), katika kijiji
cha Funta, Bumbuli mkoani Tanga.
Bw. Shebuge amefariki dunia
jana (Alhamisi, Julai 6, 2017) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata na shinikizo la damu.
Akizungumza kwa niaba ya
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia, Waziri Mkuu amesema kifo hicho ni pigo kwa
Serikali.
Amesema enzi za uhai wake
marehemu Bw. Shebuge alikuwa mpole na muadilifu na kutoa mchango mkubwa kwenye kufanikisha maamuzi na
utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ufanisi.
“Kwa kweli hatuna budi kwa
sasa “Wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.”
Awali,
Katibu Mkuu Ikulu, Bw. Alphayo Kidata akisoma wasifu wa marehemu Bw. Shebuge
alisema marehemu alizaliwa Mei 25, 1969 wilayani Korogwe, Tanga.
Alisema marehemu alipata
elimu ya msingi katika shule ya Mkwakwani kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1983,
ambapo alipata elimu ya sekondari katika shule ya Usagara kuanzia mwaka 1984
hadi mwaka 1987, zote za mkoani Tanga.
Bw. Kidata alisema mwaka
1988, marehemu alijiunga na shule ya sekondari ya Ilboru mkoani Arusha kwa
ajili ya masomo ya kidato cha tano na cha sita.
Alisema mwaka 1992 alijiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata shahada ya Sanaa na Ustawi wa Jamii
mwaka 1995, mwaka 1998 alipata shahada ya uzamili ya Sanaa na Ustawi wa jamii.
Pia marehemu alipata mafunzo mengine mbalimbali ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.