Wednesday, July 12, 2017

MAJALIWA: HAKUNA KIJIJI TANZANIA KITAKACHOACHWA BILA YA UMEME

*Asema vilivyo mbali na gridi kufungwa sola


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

Amesema Serikali imetenga shilingi trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai 11, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa.

Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa aliyasema hayo katika mikutano aliyoifanya kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga, Mbecha na Luchelegwa, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na wilaya ya Ruangwa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Pia Waziri Mkuu amesema  mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliongeza kwamba  lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi.
Waziri Mkuu alisema huduma hiyo ni muhimu kwani mbali ya kutumiwa majumbani lakini pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha zahanati,shule ,viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.

Kwa upande wake Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Mhandisi, Johnson Mwigune  alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu mkandarasi aliyepangiwa katika vijiji hivyo atakuwa tayari ameanza kazi ya kusambaza umeme.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.