WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la nyumba Nchini kwenda kujenga nyumba bora za makazi katika maeneo yote mapya ya utawala ikiwemo mikoa na wilaya ili kusaidia kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi.
Pia ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Momba mkoani Songwe zinazojengwa katika kijiji cha Tindingoma, unaojengwa na Shirika la Nyumba Nchini.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Julai 21, 2017) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Naming’ongo wilaya ya Momba akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.
“Nalipongeza Shirika la Nyumba kwa mikakati waliyonayo ndani ya shirika hilo na kwamba waendelee na utekelezaji wa mipango hiyo ya ujenzi wa nyumba ili maeneo yote mapya ya utawala yaweze kuwa na makazi bora ya kuishi watumishi.”
Pia aliwataka wakazi wa kata ya Chitete yaliko makao makuu ya wilaya ya Momba kuhakikisha wanachangamkia fursa ya uwepo wa makao makuu wa wilaya kwenye kata yao kwa kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kupangisha watumishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemia Mchechu amesema mradi huo wenye thamani ya sh bilioni 2.2 ulianza kujengwa Machi 2016 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Amesema mradi huo ulibuniwa baada kupokea maombi kutoka Halmashauri ya wilaya ya Momba na kwamba unatekelezwa kwa awamu mbili ya kwanza ni ujenzi nyumba nane na tayari zimekamilika.
Ameongeza kwamba ujenzi wa awamu ya pili unajumuisha nyumba tisa ambapo gharama ya ujenzi wa nyumba itatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya ofisi za Halmashauri hiyo.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya NHC , Bi. Blandina Nyoni amesema shirika hilo lilianzisha mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha wananchi kuwa na makazi bora.
Amesema katika miradi 54 ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa na shirika hilo katika maeneo mbalimbali nchini kati yake miradi 24 imekamilika ikiwemo 14 ya nyumba za gharama nafuu.
Pia Mbunge wa jimbo la Momba (CHADEMA) Mheshimiwa David Silinde amesema anashukuru Serikali kwa ujenzi wa nyumba hizo na kumueleza Waziri Mkuu kwamba wananchi wa Momba wanaridhishwa na utendaji wa Serikali na kwamba maendeleo
hayana chama.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.