Monday, July 31, 2017

NITAFUATILIA KWA KINA UJENZI WA MIRADI YA MAJI-MAJALIWA

*Lengo ni kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atahakikisha anafuatilia kwa kina ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya maji ili kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa katika kugharamia miradi hiyo.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Julai 31, 2017) alipozungumza na wananchi wa Jiji la Mbeya katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.

Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga sh. bilioni 237.8 kugharamia miradi ya maji nchini.

Alisema atafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa ujenzi wa miradi yote ya maji nchini ili kuhakikisha malengo ya kampeni hiyo ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao yanatimia.

“Nitafuatilia katika maeneo yote nchini ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maji iwapo kinalingana na thamani halisi ya miradi husika. Lengo ni kuhakikisha kwamba thamani ya miradi yote inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.”

Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383  kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 1.693 zinatarajiwa kutumika kwenye Halmashauri ya Jiji la Mbeya huku sh. milioni 622.049 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maji ya Halmashauri ya wilaya ya Mbeya.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuendelea kutekeleza kwa vitendo kauli ya Rais Dkt. Magufuli ya Hapa Kazi Tu kwa kufanya kazi kwa bidi ili kuweza kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi kumuomba Serikali iruhusu mikutano ya hadhara kwa ajili ya viongozi wa vyama vya siasa, ambapo alimweleza kwamba hakuna kiongozi aliyezuiwa kufanya mikutano katika eneo lake la kiutawala.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.