WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba akutane na Bodi ya mazao mchanganyiko kwa ajili ya kuliondoa zao la ufuta na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Pia amewaagiza wakuu wa mikoa yote inayolima zao la ufuta kukutana na Dkt. Tizeba kwa ajili ya kupanga mfumo mzuri wa uuzaji katika msimu wa mwaka 2016/2017 wakati Serikali ikijipanga kuliingiza zao hilo katika mfumo wa stakabadhi ghalani.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Julai 10, 2017) wakati akisalimiana na wananchi katika vijiji vya Nangano, Kibutuka na Kiangara alipowasili katika wilaya ya Liwale kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi.
Ametoa kauli hiyo baada ya mbunge wa jimbo la Liwale, Mheshimiwa Kuchauka pamoja na wananchi kuiomba Serikali iwasaidie kuboresha bei ya zao la ufuta ambayo imekuwa ikiyumba.
Waziri Mkuu amesema “tatizo lipo kwenye mfumo wa uuzaji zao la ufuta, unauzwa kwa bei ya rejareja, wanunuzi wako huru. Serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuliondoa zao katika bodi ya mazao mchanganyiko na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuboresha bei yake.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Justine Monko kuhakikisha anamaliza tatizo la maji katika vijiji vya Nangano,Kibutuka na Kiangara.
Amesema Serikali imedhamiria kuondoa tatizo la maji kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400. “Ndio maana Serikali imekuja na Kampeni inayosema mtue mama ndoo kichwani.”
Pia amemtaka Mhandisi wa Maji Bw. Andrew Kilembe kuandika barua ya kufuatilia fedha za maji sh. milioni 76 kwa ajili ya kijiji cha Kiangara walizopangiwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa Waziri wa Maji ili waweze kukamilisha uchimbaji wa kisima.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.