Hiyo ni kauli ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akiirudia mara kwa mara pale
anapopata fursa ya kuwahutubia wananchi. Lengo lake ni kuwadhihirishia
watanzania kuwa Serikali ya awam ya Tano anayoingoza imedhamiria kutekeleza sheria,
Sera, Mipango na mikakati ili kila mtanzania apate matokeo chanya ya
utekelezaji huo.
Bila shaka msomaji wa Makala hii tunaposema matokeo
chanya ya utekelezaji wa serikali ya awam ya tano utakubaliana na mimi kuwa
unayafahamu, baadhi ya matokeo hayo ni kuimarika uwajibikaji na nidhamu katika
Utumishi wa Umma; kuboresha huduma za kiuchumi na za kijamii; na kutekeleza
Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Serikali Kuhamia Dodoma.
Kimsingi matokeo hayo ni chanya lakini pia yanamgusa
kila mtanzania ambaye ni wa hali ya juu na chini. Hii ni kutokana na uongozi mahiri,
uzalendo uliotukuka na dhamira njema aliyonayo Mhe. Rais kwa Watanzania.
Ili dhamira
hiyo iwe endelevu lazima kuwepo na uratibu imara, unaofanywa kiufanisi katika kuhakikisha
kuwa sheria, Sera, Mipango na mikakati ya serikali inaratibiwa na inatekelezwa
kwa manufaa ya Watanzania.
Ifahamike tu, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye
majukumu ya kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali katika sekta zote na
Bungeni. Ofisi hii imepata jukumu hilo kwa mara kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara (52).Pamoja na majukumu hayo ya msingi wa kikatiba, Aidha,
Ofisi hii inahusika na kuratibu masuala yote mtambuka, ambapo ni yale masuala
yanayuhusisha sekta Zaidi ya moja kama vile; (UKIMWI, Madawa ya Kulevya, Uendelezaji
wa Makao Makuu ya Nchi Dodoma, Uchaguzi, Bunge, Vyama vya siasa, Kazi, Ajira, Vijana
na Watu wenye ulemavu).
Makala hii itajikita katika kuangalia jinsi ofisi
hii ilivyodhamiria kutekeleza majukumu yake ya kuratibu na kusimamia shughuli zote
za serikali ndani na nje ya Bunge na masuala mtambuka, ili kuleta matokea
chanya nchini na hatimaye kufanikisha adhima ya serikali ya awam ya tano ya
kujenga uchumi wa viwanda.
Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli
za Serikali
Hatuwezi kuzungumzia matokeo chanya ya shughuli za
serikali bila kuwa na nyenzo bora za kusimamia na kuratibu shughuli hizo
kuanzia katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na kitaifa.
Kwa kulitambua hilo
Ofisi ya Waziri Mkuu imeanzisha Mfumo wa Wazi wa Kielektroniki wa kufuatilia
uwajibikaji na utendaji Serikalini. Mfumo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika
uratibu wa shughuli za Serikali kwa kuwawezesha Viongozi kutoa maelekezo na
kufuatilia utekelezaji wake.
Kama tunavyojua
serikali hii inaongozwa na falsafa ya “HAPA
KAZI TU” hivyo mfumo huu unajikita katika dhana hiyo ya kuona kazi
inafanyika kwa kutekeleza maagizo ya viongozi wakuu na Mpango wa Taifa wa
Maendeleo.
Ofisi ya Waziri Mkuu
imedhamiria kuratibu kwa matokeo chanya kwa kupitia mfumo huo ambao utaongeza
kasi ya utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za Serikali kwa wakati na pia
kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma.
Wizara na Taasisi zote
za Serikali zinatakiwa kuutumia Mfumo huo kikamilifu ili kurahisisha
ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Serikali na kusaidia viongozi kutatua
vikwazo pale vinapojitokeza.
“Mfumo huu
utasaidia sisi waratibu washughuli za serikali kuangalia maagizo na ahadi
zilizotolewa na viongozi wakuu wa serikali ambazo zitakuwa zinawekwa katika
mfumo huo na wasaidizi wao. Mfumo huo utaainisha mhusika wa kutekeleza agizo
hilo, kama limetekelezwa ama bado halijatekelezwa hivyo unakuwa unauwezo wa
kuangalia nini kilielekezwa na utekelezaji wake, tunataka utekelezaji wa
shughuli za serikali ziwe za ufanisi na kwa wakati”
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Jenista Mhagama, Machi 2017, Dodoma, alipokuwa
akizindua Mfumo huo.
Ikiwa ni zaidi ya miaka 40 tangu serikali
kuwa na dhamira ya kuhamia Dodoma, serikali ya awam ya Tano kupitia Ofisi ya
Waziri mkuu imeweza kuratibu uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za
Serikali Kuu Dodoma kwa awamu.
“Ninafurahi
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tayari watumishi 2,069 wakiwemo Mawaziri,
Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, baadhi ya Wakuu wa Idara
na Vitengo na watumishi wengine wamekwishahamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Vilevile, Wizara zote zimepata majengo ya Ofisi yatakayotumika katika kipindi
cha mpito”
Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa, Julai, 2017 Bungeni.
Katika kuhakikisha matokeo chanya ya zoezi hili
yanapatikana, Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu zoezi la kuupitia upya
Mpango Kabambe wa Mji wa Dodoma. Mapitio hayo yatasaidia sana kuepuka makosa
yaliyofanyika katika miji mingi hususan ujenzi holela unaochangia katika
uchafuzi wa mazingira na kuharibu mandhari ya miji.
Ni wazi kwamba, Ili Mji wa Dodoma uweze kuendelezwa
kwa mpangilio mzuri wenye kukidhi uchumi wa viwanda unaokusudiwa na serikali ya
awam ya Tano. ujenzi wa Mji wa Dodoma hautafanywa na Serikali pekee, bali serikali
inaendelea kuhamasisha Sekta binafsi na wadau wengine kuwekeza Dodoma.
Kwa upande wa serikali kupitia Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC), limejenga nyumba 300 za makazi ambazo watumishi wanaweza kununua
au kupangishwa. Manispaa ya Dodoma na Taasisi nyingine za Serikali.zinaendelea
na zoezi la upimaji wa viwanja, kuboresha miundombinu na kudhibiti ujenzi
holela kwa kushirikiana.
Msomaji wa
Makala hii utakubaliana nami kuwa dhamira ya kuratibu uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za
Serikali Kuu Dodoma, inaleta matokeo chanya nchini kwani serikali itakuwa
imetoa fursa kwa wananchi kutoka pande zote nchini kupata huduma zote za
serikali bila kusafiri umbali mrefu hadi Dar es salaam kama ilivyokuwa awali.
Lakini pia
uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za Serikali Kuu Dodoma wananchi watapata
fursa ya kupata huduma hizo kwa wakati na kwa pamoja mara tu serikali itakapo
kamilisha ujenzi wa maeneo ya mji wa serikali ambao utakuwa na ofisi zote za
serikali mahali pamoja.
Siasa
Ukiniuliza
siasa nini? Kwa ufupi nitakwambia neno siasa linaashiria mambo yanyaoihusu jamii,
tunaweza kueleza kwa ufupi kuwa hiyo ndiyo maana ya siasa. Kwani siasa hubeba
taswira nzima ya jamii katika; Uchumi, elimu, mfumo wa, haki, wajibu na sheria,
mgawanyo wa mali katika jamii, mila, utamaduni, desturi, imani na mahusiano miongoni
mwa jamii au nje ya jamii husika.
Kwakuwa
siasa inahusu maisha ya wanadamu na wanasiasa wanajishughulisha na mambo
yanayoihusu jamii, hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa
kisiasa, ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini.
Ofisi ya
Waziri Mkuu ndiyo yenye dhamana ya Kuratibu shughuli za siasa nchini kupitia
ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Ninatoa rai kwa
wadau wa siasa kote nchini kujenga utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa
za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa za kuunganisha watu wetu
badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea. Serikali
itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga kuleta ustawi wa
wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi” Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa, Julai, 2017 Bungeni.
Katika
misingi ya kuboresha demokrasia nchini, ofisi hiyo imeweza kuratibu Chaguzi
Ndogo zilizofanyika tarehe 22 Januari, 2017 katika Jimbo la Dimani - Zanzibar
na Udiwani katika kata 20 Tanzania Bara kwa kushirikisha wagombea kutoka vyama
15 vya siasa.
Katika
kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata uwakilishi, tayari Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeweza kuendesha
kesi kwa kasi na weledi za baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Mashauri yaliyofunguliwa
baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 yalikuwa ni mashauri 53 ya kupinga ushindi
wa Ubunge na mashauri 194 ya kupinga ushindi wa Udiwani, Mashauri hayo yamekwisha
sikilizwa na hukumu kutolewa.
Tukiacha masuala ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, bila shaka msomaji wa Makala hi utakuwa
unaufikiria pia uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Tayari Ofisi ya Waziri Mkuu katika
dhana ya kuratibu kwa matokeo chanya imeshaanza kuratibu zoezi hilo kupitia
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Serikali imetenga
shilingi bilioni 10 kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura
kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi
ya kufanya uboreshaji wa daftari hilo utakaojikita katika kufanya mapitio ya
mifumo ya menejimenti ya Uchaguzi.
“Tume hii ni
huru, hivyo Bunge limepitisha fedha hizo kwa ajili ya Tume kuanza kufanya
maadalizi ya kuboresha Daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa mara ya kwanza na
itafanyika tena mara ya pili kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Lazima Tume
ipitie upya mifumo yake na kuiboresha lakini pia kuangalia na vifaa
ilivyonavyo. Nimeridhika na mpango kazi wa tume wa kukamilisha kazi hiyo kwa
ufanisi na weledi mkubwa, sisi kama serikali tutawasaidia katika maeneo yote
ambayo kikatiba tunaruhusiwa kushirikiana nao katika utekelezaji wa
majukumuyao”
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Jenista Mhagama Agosti, 2017, alipotembelea Ofisi za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Bunge
Nikukumbushe
msomaji wa Makala hii, kuwa nchi yetu inayo mihimili mitatu ya nchi ambayo ni Serikali,
Bunge na Mahakama. Wajibu wa serikali ni kuendesha utawala na utekelezaji kila siku wa shughuli za umma,
Bunge linao wajibu wa kujali sera na kutunga sheria na mahakama zinao wajibu wa
kusikiliza na kuamua kesi na pia kutoa tafsiri ya sheria na katiba ya nchi.
Ofisi ya Waziri Mkuu kama lilivyo jukumu la kikatiba
la kuratibu shughuli za serikali, hata ndani ya Bunge ofisi hii ndiyo inayoratibu
shughuli za serikali Bungeni, Shughuli
hizo zinazojumuisha mikutano minne kwa mwaka pamoja na Kamati zake zimeratibiwa
kwa mafanikio makubwa.
Ofisi hii huakikisha
inakuwa kiungo kati ya serikali na Bunge kama ilivyo mihimili tofauti na yenye
mamlaka yake ya kikatiba. miswada 10 ya sheria ya serikali ilijadiliwa na
kupitishwa na Bunge pamoja na matoleo 41
ya Gazeti la serikali na nyongeza zake yaliwasilishwa Bungeni.
Na hapa
ndipo msomaji utaweza kunielewa kwa nini tumedhamiria kwa matokeo chanya hapa
nchini kwani ofisi hii ndiyo kiungo cha serikali na wananchi kupitia Bungeni
ambapo wabunge huwawakilisha wananchi.
Wabunge kama wawakilishi wawanachi wamewawakilisha
vyema Bungeni nahasa katika kutetea maslah yao. Katika mkutano ulioisha wa saba wa Bunge umefanikisha kuundwa kwa
kamati maalum ya Wabunge tisa itakayotathmini
mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini.
Kuundwa kwa Kamati hiyo kumetokana na pendekezo la
kuunda Tume ya kuchunguza na kufuatilia madini ya Almasi alilolitoa Rais Dk.
John Magufuli Juni 12 mwaka huu wakati akipokea taarifa ya pili ya kamati ya
kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kuhusu usafirishaji wa makinikia.
Kamati hiyo pia itaandaa mapendekezo mahsusi kwa
ajili ya kuishauri Serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya Madini hapa
Nchini. Ofisi ya waziri Mkuu kama mratibu wa shughuli za serikali Bungeni
tumedhamiria kuratibu mapendekezo hayo kwa matokeo chanya kwa watanzania wote.
Lakini
pia, Ofisi hii huratibu maswali ya serikali Bungeni, suala ambalo huipa fursa
ofisi ya waziri mkuu kujua na kutambua nini mahitaji hasa ya watanzania na
kuweza kuelelekeza kwa watekelezaji husika kuweza kuyapatia majibu.
Katika Mkutano wa nne, wa tano na wa sita wa Bunge
la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maswali ya msingi 330 ya
Wabunge yaliulizwa na kujibiwa na Serikali pamoja na maswali 865 ya nyongeza
.
Aidha,
Ofisi ya Waziri Mkuu hupokea malalamiko rufani, kwa maana ya malalamiko ambayo
mhusika hakupata suluhisho katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya kijiji, kata,
wilaya, mkoa na kitaifa, ofisi hii huya pokea kama mratibu wa shughuli zote za
serikali na kuyapatia ufumbuzi kwa wakati.
Tayari Ofisi imeshapokea na kushughulikia jumla ya
kero na malalamiko ya wananchi 278 na kuyapatia ufumbuzi na nyingine
zimewasilishwa katika mamlaka mbalimbali ili kupatiwa ufumbuzi.
Tutoe
wito kwa watanzania amabao wanayo malalamiko ya aina hiyo kufika ofisi ya
Waziri Mkuu, milago huwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa Saba Mchana
kwa siku zote za kazi.
Hata hivyo;
kutokana na matokeo chanya ya serikali ya awam ya Tano, ni wazi kuwa wananchi
wenye malalamiko ya aina hiyo wamepungua kwa kiasi kikubwa kufika ofisini, hii
inadhihirisha kuwa uwajibikaji na uadilifu umeongezeka serikalini.
Uratibu
wa Maafa
Kimsingi maafa
yanapotokea huathiri maisha ya watu na kuharibu mali na mazingira. Maafa pia,
hayachagui yanapotokea iwe Vijijini au Mijini, na iwe nchi za dunia ya kwanza
au dunia ya tatu wote wanaathirika. Ili kuweza kupunguza athari zinazoletwa na
maafa ni lazima kuchukua hatua za tahadhari mapema.
Hapa nchini jukumu la
kuratibu shughuli za maafa lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika Idara ya
Uratibu wa shughuli za maafa. Idara hii ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria Na.9
ya mwaka 1990 ya Uratibu wa Misaada ya Maafa.
Serikali
wakati wote inahakikisha kuwa nchi ipo katika hali ya utayari wa kukabiliana na
maafa na pia kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo huduma za matibabu, ushauri wa
kisaikolojia, na vifaa
pale maafa yanapotokea.
Kufuatia tetemeko
la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa mwezi Septemba 2016, Serikali
kwa kushirikiana na wadau iliechukua hatua za kushughulikia athari zilizotokana
na tetemeko hilo. Huduma za afya na tiba na za kibinadamu za chakula na malazi
zilitolewa kwa walioathirika.
Changamoto
ambayo hupatikana wakati wa uratibu wa shughuli za maafa ni kuwa wananchi
wachache kushindwa kuelewa kuwa maafa ya asili ni vigumu kuyazuia lakini pia ni
vigumu hata kuyatabiri kama ilivyo maafa ya tetemeko la ardhi.
Kwa
mantiki hiyo ni vigumu serikali kuwa na makadirio sahihi ya bajeti ya kukabili
na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea. Lakini kwa kuwa serikali hujali
ustawi wa jamii yake huchukua jukumu la moja kwa moja kurejesha hali, ambayo
itaweza kuwaweka wananchi wake kwa mara moja
na kwa wakati katika hali ya kawaida na kuendelea na uzalishaji kama
ilivyo kuwa kabla ya maafa.
Tukiangalia
maafa ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera serikali ilichukua jukumu la kurejesha
hali ya miundo mbinu ya umma badala ya miundo mbinu ya kila mwananchi mmoja
moja isipokuwa kwa wale wazee, wajane/wagane, yatima na watu wenye ulemavu
pamoja na watu ambao nyumba zao zilibomoka kabisa na kubaki bila makazi.
Serikali ilitoa maturubai 6,237, mahema 367, mabati 7,300 na mifuko ya saruji
1,825 kwa walioathirika.
Katika
kuhakikisha jamii iliyoathirika inarejea katika hali ya kawaida Serikali
ilirejesha hali ya miundombinu iliyobomoka, yakiwemo majengo ya Serikali na
Taasisi za Umma 686, Kituo cha wazee Kilima Kituo cha afya Kabyaile Ishozi pamoja
na ukarabati wa Omumwani.
Serikali
inaendelea na ujenzi wa Shule ya Ihungo, Nyakato na Zahanati mpya ya kijiji cha
Rwele. Ofisi ya Waziri Mkuu imeshakabidhi shughuli za kuratibu maafa hayo kwa
kwa Mwenyekiti wa kamati ya maafa ya mkoa huo ambaye
ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, kwa
mujibu wa Sheria ya Maafa ya mwaka 2015 sehemu ya 13(1).
Bila
shaka msomaji wa Makala hii unakubaliana na mimi kuwa Maafa ni tukio kubwa
ambalo husababisha upotevu wa maisha ya watu, wanyama, majeraha, uharibifu wa
mali na mazingira na kuvuruga kabisa mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii
iliyoathirika na hatimaye jamii kushinwa kukabili hali hiyo kwa uwezo wake
wenyewe bila msaada toka sehemu tofauti.
Ili
kuhakikisha menejimenti ya maafa inakuwa na matokeo chanya, tayari Ofisi ya
waziri mkuu inao mradi wa utoaji wa taarifa za tahadhari zinazohusu mabadiliko ya
tabia nchi, ili kuchukua hatua za ufuatiliaji, kufanya tathimini na mbinu
mbalimbali za kukakabiliana na hali hiyo wakati wa kujenga maendeleo ya nchi.
Lengo la Mradi, ni kuimarisha mifumo ya utoaji tahadhari na taarifa kwa
ajili ya kuweka mipango thabiti ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi nchini.
Kupitia
mradi huo vimejengwa vituo vipya 20 vya upimaji wa hali ya hewa katika
Halmashauri 11 za Tarime, Nyamagana, Muleba, Longido, Geita, Maswa, Kigoma,
Sikonge, Kongwa, Serengeti, na Kahama. Kuwepo kwa vituo hivyo kutaongeza
ufanisi katika upatikanaji wa taarifa za tahadhari hasa kwa majanga ya mafuriko
na ukame.
Ili matokeo
chanya ya shhughuli za uratibu maafa kuwa endelevu jamii lazima iweze kushiriki
kikamilifu katika kupunguza athari za Maafa, Serikali haina budi kuijengea
jamii husika uwezo wa kupunguza athari hizo.
Kupitia mradi huu ofisi ya
Waziri mkuu imeandaa Mipango ya kujikinga
na Usaidiaji wakati wa Majanga ambayo imewashirikisha wadau katika ngazi ya Vijiji, Kata na Wilaya
Kama vile katika wilaya za Liwale
(Lindi) na Arumeru (Arusha).
Vijana, Kazi na Ajira
Tunafahamu kuwa Vijana ndio wenye nguvu zaidi za
kufanya kazi, Vijana ni wabunifu, Vijana ndio chachu ya mabadiliko chanya
katika jamii na Vijana ndio warithi wa Taifa.
Hapa
nchini asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Hivyo, Serikali
inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi.
Ili
kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja na
kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi, lakini pia ili kutimiza adhima ya
matokeo chanya, Serikali imeshaanza kuchukua hatua za kufanya mapitio ya Sera
ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007 kutokana na kupitwa na wakati.
Kwa
kutambua nafasi ya Vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini,
Serikali imetoa mafunzo kwa vijana 9,120 katika fani za stadi za kushona nguo
na kutengeneza bidhaa za ngozi.
Wapo
vijana wenye ujuzi katika fani mbali mbali lakini hawakuwahi kupata mafunzo
rasmi, ili kufanya shughuli zao kuwa endelevu serikali imefanya mafunzo ya
kurasimisha ujuzi huo uliopatikana kwa mfumo usio rasmi kwa kuwapatia mafunzo
ya kukuza ujuzi na stadi za kujiajiri takribani vijana 1,469 wamehitimu mafunzo
hayo na kupata ajira.
Vijana wengine
7,651 wanaendelea kupata mafunzo kupitia viwanda vya TOOKU GARMENTS, MAZAVA
FABRICS, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), VETA na Don Bosco.
Ni vyema
ikaeleweka serikali inalenga kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi wa kujiajiri na
stadi za kazi kwa vijana 15,350 katika fani mbalimbali katika mwaka huu wa
fedha 2017/2018.
Shime
kijana huna budi kuchangamkia furs hizi na hatimaye kuwa mshirki kikamilifu
katika kujenga uchumi wa viwanda.
Serikali
kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi
bilioni 1.5 kwa vikundi vya vijana 297 katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Aidha,
Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia mapato yake ya ndani zimetoa Shilingi
bilioni 4.6 ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana 2,356.
Hatua
hizi zimekwenda sanjari na utengaji wa maeneo maalum yenye jumla ya ekari
85,603 kwa ajili ya shughuli za vijana za kilimo, biashara ndogo ndogo,
burudani na michezo.
“Haiwezekani
vijana wawe wanashinda vijiweni wanacheza pool, wakati wazee na akina mama wapo
mashambani wanalima. Kawahimizeni wafanye kazi, wasipofanya kwa hiari
walazimisheni kufanya kazi”
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mara bada ya
kuwaapisha wakuu wa mikoa, Machi, 2016.
Kwa kauli
hiyo ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli tungependa kutoa wito kwa Halmashauri zote
nchini kutenga asilimia tano (5) ya mapato yao kwa ajili ya vijana na asilimia
tano (5) kwa wanawake, ili waweze kutengeneza ajira zao.
Ifahamike tu,
kuwa hadi Machi 2017, jumla ya ajira 418,501 zimezalishwa nchini. Kati ya ajira
hizo, ajira 239,017 sawa na asilimia 57 zimezalishwa katika sekta binafsi
wakati ajira 179,484 sawa na asilimia 43 zimezalishwa kutokana na shughuli za
sekta ya umma ikiwemo miradi ya maendeleo.
Msomaji, huna
budi kutambua kuwa ili shughuli ambazo huratibiwa na ofisi ya Waziri Mkuu ziwe
na matokeo chanya kwa watanzania hakuna budi ya kuhimiza mahusiano mazuri
mahala pa Kazi aidha katika sekta binafsi au Sekta ya umma.
Serikali
imefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 58 ya migogoro ya kikazi inatokana na
kutozingatiwa kwa taratibu za kuachisha kazi. Sekta zinazoongoza kwa migogoro
ya kazi ni usafirishaji, ujenzi, ulinzi binafsi, elimu, huduma za hoteli na
viwanda.
Katika kupunguza
migogoro mahali pa kazi, Serikali imefanya kaguzi na kusimamia uundwaji wa
Mabaraza ya Wafanyakazi.
Aidha, Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi imeendelea kutimiza wajibu wake wa kusuluhisha migogoro
ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari 2017, Tume imesajili jumla
ya migogoro 8,832 kati ya hiyo migogoro 3,319 sawa na asilimia 37.6 ya migogoro
yote iliyosajiliwa imesuluhishwa.
“Waajiri na waajiriwa wote nchini, zingatieni
Sheria za Kazi na imarisheni uhusiano mzuri kwenye maeneo ya kazi, ili muda
mwingi zaidi utumike kwenye uzalishaji mali badala ya kutatua migogoro. Vilevile, ni muhimu sana muimarisha kaguzi za kazi na
kuendelea kusaini mikataba ya kuunda na kusajili mabaraza ya wafanyakazi ili
kuimarisha zaidi mahusiano mahali pa kazi”
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Siku ya Wafanyakazi
Duniani, Mei, 2017.
Huduma
kwa Watu Wenye Ulemavu
Ofisi ya
Waziri Mkuu kama mratibu wa shughuli za serikali imeendelea kutoa huduma pamoja
na kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu, tayari
imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye Ulemavu
zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji.
Baadhi ya wanajamii huwanyanyapaa watu wenye
ulemavu, kwa kulitambua hilo tunaendelea
kuratibu kampeni za kupinga unyanyapaa
na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga,
Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na
kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.
Tunatambua
kuwa Mawasiliano ni njia pekee ya kuifanya jamii kushiriki kikamilifu kwa
maendeleo. Kama tujuavyo baadhi ya wana jamii wenye ulemavu wa kutosikia
wamekuwa wanashindwa kupata huduma ya mawsiliano hasa kupitia Vituo vya
Televisheni kwa kuwa hutumia lugha ya alama.
Serikali
inahakikisha kwamba watumiaji wa lugha ya alama wanapata haki ya kupata habari
na vituo vyote vya televisheni vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya
alama.
Watu
wenye ulemavu wanaendelea kupata huduma ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi
kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya kufundishia.
Katika masuala
mtambuka ambayo Ofisi hii huyaratibu ni Vita dhidi ya UKIMWI, Kwa kuwa suala
hili linahitaji jitihada elekezi za wadau mbalimbali ili kuweza kushinda vita
hii.
Ili
kuishinda vita hii nyenzo ya msingi ni rasilimali fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu
kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI, Tazania (TACAIDS), mnamo Desemba 2016
ilizindua Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ulioanzishwa na Serikali miaka miwili
iliyopita.
Kupitia
harambee iliyofanyika kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo, shilingi milioni 347
zilipatikana kama ahadi. Vilevile, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni
5.6 kwa ajili ya Mfuko wa UKIMWI.
Serikali
inaendelea kutoa huduma kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) ambapo
hadi Desemba, 2016 WAVIU 839,574 sawa na asilimia 63 ya WAVIU wote, walikuwa
wamepatiwa dawa. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwahamasisha WAVIU
kujitokeza na kuingia kwenye Mpango wa Tiba ya Kufubaza Athari za UKIMWI.
Ili vita
hii tuweze kuishinda lazima tuwe na mikakati endelevu, tayari serikali
imekamilisha uandaaji wa miongozo minne ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI
ikijumuisha Mpango Kazi wa Kinga, Mkakati wa Kondomu, Mkakati wa Uwekezaji na
Mpango kazi wa jinsia.
Tunatambua
kuwa suala la UKIMWI ni mtambuka na ambalo huihitaji juhudi za makusudi
kupambana nalo kwa sekta zote za umma na binafsi, ili vita hii iwe na matokeo
chanya, serikali imeirisha uratibu wa
afua za UKIMWI kwa wadau wote wa sekta ya umma na binafsi na kupitia mifumo ya
uratibu iliyoanzishwa.
Serikali
kwa kushirikiana na wadau pia inaendelea kujenga uwezo Kamati zilizo katika
ngazi ya jamii hususan vijiji na kata ili kufikia malengo ya kitaifa na
kimataifa ya kupunguza na kumaliza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia mfumo
ulio katika jamii.
Vilevile,
Serikali itakamilisha utafiti wa nne wa kubainisha viwango vya maambukizo ya
UKIMWI nchini na kuboresha ushiriki wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi katika
kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI.
Tunatoa
wito kwa watanzania wote kushirikiana katika kutokomeza maabukizi mapya ya
UKIMWI nchini.
Takwimu
zinaonesha kuwa maabukizi mapya yameshuka kwa asilimia 50 mkwa watoto miongoni
mwa watoto duniani 290,000 wapya walioambukizwa mwaka 2010 na watoto wapya
150,000 waliambukizwa mwaka 2015. Maambukizo mapya kwa watu wazima hayajashuka
tangu 2010 duniani.
“Tuungane
Kutokomeza Maambukizo Mapya ya Virusi vya UKIMWI”
Vita
Dhidi ya Dawa za Kulevya
Dawa za
kulevya zinaathiri maisha ya vijana wetu wengi na hivyo kuzima ndoto za maisha
yao na kupunguza nguvu kazi ya Taifa. Suala hili linaoneka kumgusa Rais wa
Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya kuwaapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Tanzania ambapo alitoa wito kwa vyombo vya ulinzi kuendeleza vita dhidi ya
biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
“Madawa ya Kulevya yanapoteza nguvu kazi za
watanzania hasa vijana, hivyo hii kazi si ya mtu mmoja ni ya wanzania wote
kushirikiana kwa pamoja katika kupambana na jambo hili kwa manufaa ya nchi”
Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, Februari, 2017.
Katika
kuhakikisha matokeo chanya katika hili la kupambana na janga hilo, Ofisi ya
waziri Mkuu kama mratibu wa shughuli za serikali Bungeni, Tayari Bunge
limefanya marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5
ya Mwaka 2015.
Marekebisho
hayo yameipa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nguvu ya
kukamata, kupeleleza na kushitaki watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za
kulevya.
katika
kipindi cha Julai, 2016 hadi Januari, 2017 watuhumiwa 11,303 walikamatwa kwa
tuhuma za kujihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za
kulevya katika sehemu mbalimbali nchini.
Kati ya
watuhumiwa hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa
hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao
unaendelea. Pia tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa
79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea.
Tunaamini
kwa jinsi tulivyo dhamiria kkutratibu kwa matokeo chanya kwa watanzania wote ,
ni imani yetu kuwa, Mamlaka ya Udhibiti
wa Dawa za Kulevya itaendeleza kwa kasi zaidi juhudi za kupambana na uingizaji,
uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini.
Pamoja na
kuwa shughuli za uratibu kuwa imara lakini bila jamii kushiriki kikamilifu
hatuwezi kufanikiwa hivyo tunatoa wito wazazi kuwa karibu na vijana wao na
kufuatilia nyendo zao ili wasiingie kwenye mtego huu wa dawa za kulevya.
Tunahitaji
taifa la watu wenye afya njema ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujenga
uchumi wa viwanda kama ilivyo dhamira ya seerikali ya awam ya tano amabao pia
inasisitiza watu kufanya kazi.
Tunaamini
msomaji wa Makala hii umeweza kuelewa kwa jinsi tulivyodhamiria na kuweza
kuratibu shughuli za serikali ndani nan je ya Bunge pamoja na masula mtambuaka.
Aidha , kwa kuwa Makala hizi zinaendelea Kutolewa na Taasisi za serikali hasa
nasi tunaamini taasisi amabazo zipo chioni ya Ofsis ya Waziri Mkuu zitafafanua
kwa kina utekelezaji wa mipango na mikakati yao.
Tataendelea kukuhudumia
kwani Dira yetu ni kutoa huduma bora za Serikali kwa umma na dhima
inayotekelezwa sasa ni kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kwa kuratibu
sekta zote kwa ufanisi na tija.
“Tumedhamiria, Tunaratibu Kwa
Matokeo Chanya nchini.”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.