Saturday, September 2, 2017

MAMA MAJALIWA AHIMIZA BIDII YA MASOMO

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewataka watoto wanaojiandaa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, waongeze bidii kwani dunia ya sasa hivi inataka wasomi.

Mama Majaliwa ametoa wito huo jana (Jumamosi, Septemba 2, 2017) wakati akizungumza na wahitimu 166 wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Martin Luther, kwenye sherehe za mahafali ya 10 zilizofanyika shuleni hapo katika Manispaa ya Dodoma.

“Ninawapongeza wanafunzi wanaohitimu lakini ni lazima mtambue kwamba huu siyo mwishi wa safari yenu ya masomo kwani dunia ya sasa inataka wasomi. Kwa hiyo, muongeze bidii hadi mfike elimu ya vyuo vikuu,” alisisitiza.

Aliushukuru uongozi wa shule hiyo na walimu wote kwa malezi mema wanayoyatoa kwa watoto hao na kwamba mafunzo yao yanadhihirika miongoni mwa watoto kwa jinsi walivyolelewa kimwili, kiroho na kiakili.

“Mtoto wangu nilimleta akiwa na miaka mitano, ameanza elimu ya chekechea na sasa anahitimu darasa la saba. Sasa hivi amekua na ana hofu ya Mungu, anatambua mema na mabaya, tunawashukuru sana,” alisema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Gilbert Nhuguti wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji ya shule, alisema kwa zaidi ya miaka mitano, shule hiyo ambayo ni ya kutwa na ya bweni, imekuwa na rekodi ya kufanya vizuri kiwilaya na kimkoa kwa kushika nafasi za kwanza.

“Mwaka jana tulishika nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya saba kitaifa kwa wastani wa daraja la ‘A’. Hata mwaka huu, kwenye mitihani ya majaribio (mock exams) tumeshika nafasi ya kwanza, tumepania kuchukua nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya mwaka huu,” alisema.

Alisema mafanikio hayo yanachangiwa na ubora wa walimu wa shule hiyo ambao wana shahada, astashahada na stashahada.

Aliwataka wahitimu hao wawe mfano huko waendako, wamtangulize Mungu katika kila walifanyalo na wasiwe watu wa kutaka kupata makubwa bila kufanya kazi kwa bidii. “Fanyeni kazi kwa bidii na mafanikio yatakuja,” alisisitiza. Pia aliwataka waendeleza tabia ya kutunza  mazingira popote pale waendapo.

Naye Mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde ambaye alipewa nafasi kutoa nasaha kwa niaba ya wazazi, aliwataka wahitimu hao watambue kuwa wanapohitimu elimu ya msingi wajione kuwa wamejengewa msingi imara.

“Kuhitimu elimu ya msingi ni sawa na kujengewa msingi imara wa nyumba. Kwa hiyo, mkauendeleze kwa kujenga matofali imara, hautakuwa na maana kama mtaujenga kwa kutumia matofali mabovu juu yake,” alisema.

Wanafunzi wa darasa la saba kote nchini, wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa Septemba 6 na 7, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.