Serikali imejipanga
kikamilifu katika kuhakikisha inayakabili maafa yanayotokea nchini kwa
kuangalia sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali zinazohusika na masuala ya
Menejimenti ya Maafa ili kuepuka madhara yatokanayo na maafa nchini.
Kauli hiyo imetolewa
na Mkurugenzi Masaidizi Idara ya Uratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
Bw. Bashiru Taratibu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza
Maafa yaliyofanyika Kitaifa mjini Dodoma na Kuwashirikisha wananchi, wanafunzi
na wadau mbalimbali.
Katika kuhakikisha
wananchi wanakuwa salama na kuepuka madhara yatokanayo na maafa tayari Serikali
imepima Viwanja zaidi ya milioni moja na nusu katika Halmashauri mbalimbali
hapa nchini ikiwa ni moja ya mikakati ya kuondoa makazi holela na kuepusha
maafa yanayotokana na matumizi ya ardhi yasiyozingatia sheria kanuni na
taratibu zinazosimamia sekta ya Ardhi.
“Wananchi wazingatie
sheria, Kanuni, na Taratibu kwa kuepuka kujenga maeneo hatarishi kama mabondeni,
maeneo yenye mafuriko na mengine yote yanayokatazwa kisheria ili kuepuka maafa”
Alisisitiza Taratibu
Akifafanua Taratibu
amesema kuwa Viongozi wa Serikali katika maeneo yote hapa nchini wanajukumu la
kusimamia sheria zilizopo ili kuepusha maafa kwa kuzingatia Kauli mbiu ya mwaka
huu inayosema “MAKAZI SALAMA: Punguza
Makazi katika Maeneo Hatarishi, Punguza kuhama kutokana na maafa”.
Akizungumzia mikakati
ya Serikali kuondoa maafa na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa maafa amesema
kuwa Idara ya Maafa imekuwa ikitoa elimu kwa Umma ili kuwasaidia wananchi kuwa
na uelewa utakaosaidia kuepuka athari za maafa.
Aidha alitaja hatua
nyingine zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni kutungwa kwa sheria ya maafa ya
mwaka 2015, Miongozo, Kanuni na kuwekwa kwa taratibu mbalimbali za kusimamia masuala ya maafa hapa nchini.
Kwa upande wake
Mratibu wa Maafa Wilaya ya Chamwino Bi Lilian Zakaria amesema kuwa wamekuwa
wakitoa elimu kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Vijjiji wakishirikisha Kamati za Maafa
katika ngazi zote ili kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na maafa pale
yanapotokea na pia kuzuia viashiria vyake.
Pia Bi Zakaria
amewataka wananchi kuepuka kujenga na kuishi katika maeneo hatarishi na
kuzingatia taratibu zote zilizowekwa na Serikali kuepuka maafa.
Naye Mwakilishi wa Asasi
za Kirai Bw. Mussa Mussa amesema kuwa
wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na maafa hali
inayosababisha wananchi kuishi salama katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
AWALI:
Chimbuko la Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ilitokana na Azimio Na. 64/200 lililopitishwa na
Baraza la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Desemba, 2009 ambapo iliamuliwa Oktoba 13
ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ikiwa na lengo la Kukuza
utamaduni wa kupunguza madhara ya maafa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia,
kupunguza madhara, Kujitayarisha, Kukabili na Kurejesha hali kuwa bora zaidi na
mwaka huu kaulimbili inasema: “MAKAZI SALAMA: Punguza Makazi
katika Maeneo Hatarishi, Punguza Kuhama kutokana na Maafa”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.