Thursday, November 16, 2017

MALIASILI KAMILISHENI ZOEZI LA UWEKEJI ALAMA MAENEO YA HIFADHI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kukamilisha zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo yote ya hifadhi ifikapo Desemba 30, 2017.

Agizo hilo limekuja baada ya kuwepo kwa migogoro ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi ambapo baadhi ya wananchi wanaendesha shughuli za kijamii ndani ya hifadhi.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Novemba 16, 2017) wakati akijibu swali la mbunge wa Ulyankulu, Bw. John Kadutu wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.

Bw. Kadutu alitaka kujua hatua zilizofikiwa na Serikali katika uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo mbalimbali ya hifadhi ili kuwaondolea wananchi usumbufu.

“Wizara ifanye mapitio ya maeneo yote ya hifadhi ambayo bado hayajawekewa alama za mipaka na kukamilisha zoezi hilo ifikapo tarehe 30, Desemba, 2017.”

Pia Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wanaoishi maeneo ya karibu na hifadhi hizo au hata ndani watoe ushirikiano kwa wataalamu ili kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa wakati.

Waziri Mkuu amesema wananchi wanaoshi katika maeneo yaliyoko ndani ya hifhadhi wawaache wataalamu wakamilishe zoezi hilo na baada ya kukamisha Serikali itafanya mapitio na kisha kutoa maamuzi kwa manufaa ya Taifa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema sheria namba moja ya Ajira za Wageni ya mwaka 2015 inaruhusu utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni kwa muda wa miaka miwili.  “Hata hivyo vinaweza kuongezwa kulingana na mahitaji hadi kufikia vipindi viwili.”

Hata hivyo, Serikali imewapa masharti wageni wanaoomba vibali vya kufanya kazi nchini kuandaa mpango wa kuwarithisha ujuzi Watanzania ili kuchukua nafasi za wageni hao mara baada ya muda wa vibali vyao kumalizika.

Pia      Serikali inayataka makampuni yote uwekezaji kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania kwa kuwa kwa sasa tunao Wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbal
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kuteuliwa Bw. Abdallah Bulembo aliyetaka kufahamu wageni wanaokuja kufanya kazi nchini wanaruhusiwa kufanya kazi kwa muda gani.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.