Tuesday, January 9, 2018

DKT.SHEIN AZINDUA SOKO LA KINYASINI


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Mohamed Shein amefungua  Soko Jipya la Kinyasini lililojengwa na Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) ili kutatua changamoto za kukosekana kwa soko la kisasa katika Mkoa wa Kaskazini litakalowasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kuendesha biashara zao.

Mhe. Rais Shein amesema soko hilo litawagusa na kuwafikia  watu wenye kipato cha chini kuinuka kiuchumi kwa kuwanufaisha   Wajasiliamali wadogo wadogo vijijini pamoja na wafanyabiashara; Asasi ndogo ndogo za kifedha zinazotoa huduma vijijini; Vyama vya Msingi vya Ushirika/ Asasi za vijijini zinazojishughulisha na usindikaji wa mazao na masoko ya mazao kwa kushirikisha wanawake katika  makundi yote.

Katika uzinduzi huo uliofanyika Januari 09, 2018 Mkoa wa Kaskazini katika eneo la Kinyasini, Mhe.Rais alisema kujengwa kwa   soko hilo kuna manufaa makubwa kwa wakulima wadogo wakiwemo wafugaji, wavuvi na wafanya kazi za mikono.

“Soko hili litakuwa lenye tija kubwa kwa wananchi wa Zanzibar bila kujali maeneo wanakotoka. Soko hili ni letu sote, lisingeweza kujengwa kila mahali, au hewani lazima lingewekwa mahali, hivyo eneo hili la Kaskazini lilipata fursa hii, hivyo niwaombe liwe la wananchi wote wa Zanzibar.”Alisema Mhe.Rais
Sambamba na hilo Mhe. Rais alieleza kuwa kujengwa kwa soko hilo ni moja ya matunda ya Muungano na kuwataka Wananchi kuuenzi na Kuulinda Muungano huo.

“Miradi hii inayohusisha Bara ni moja ya mafanikio na matokeo makubwa ya Muungano wetu na hatuna budi kuuenzi”Alisisitiza Dkt.Shein

Katika hatua nyingine,Mhe. Rais aliitaka Halmashauri husika kuendelea kuweka mikakati mizuri ya kulitunza na kuliendeleza ili liweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa Wazanzibar wote.

“Niwaombe Halmashauri Kuona njia nzuri za kuendeleza kazi hii iliyofanywa na Programu hii na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi kama ilivyokusudiwa”Alisisitiza Mhe.Rais

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuzingatia mafanikio ya mradi huu ikiwemo kusaidia kupambana na umasikini na kuleta tija.
“Kuwepo kwa soko hili kutasaidia kupambana na umasikini na kuongeza mapato, hivyo washiriki watunze miundombinu hiyo pamoja na kuongeza thamani ili kuleta tija.”Alieleza Mhe.Mhagama .
Naye Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Hamad Rashid Mohamed alimalizia kwa kuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya MIVARF kuona umuhimu kuwajengea soko lenye ubora na litakalo tatua changamoto za kukosa soko la uhakika.
“Soko hili la Kinyasini  moja kati ya masoko 16 yaliyojengwa na Programu hii katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo litasaidia kuondokana na umasikini na wananchi kujikwamua kiuchumi”   
Programu hii ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inatekelezwa katika Halmashauri 62 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar, ikiwa  imegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo,  na Uvuvi Zanzibar.Programu ilianza utekelezaji wake Mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.