Wednesday, January 31, 2018

KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA USIMAMIZI WA MAAFA NCHINI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Fautin Kamuzora akifungua  Kikao cha Baraza la Usimamizi wa maafa Tanzania kilichofanyika mapema leo mjini Dodoma, kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa  Idara ya Uratibu wa Maafa Bw. Bashiri Taratibu, na kushoto ni  Muwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Kanali Jimmy Said.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Profesa Faustin Kamuzora ameongoa kikao cha Siku moja cha Baraza la Usimamizi wa Maafa nchini kinacholenga kujadili masuala ya Menejimenti ya Maafa.

Akifungua kikao hicho alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inadhibiti na kuweka miundombinu rafiki ili kukabili maafa yanayotokea nchini.

Akifafanua Profesa Kamuzora amebainisha kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kuunda Kikosi kazi cha Taifa kitakachoshughulikia tatizo la sumukuvu, uwepo wa panya wanaoharibu mazao, viwavi jeshi na kwelea kwelea wanao haribu mazao.

Aidha, hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kupeleka misaada ya kibinadamu katika   maeneo yaliyoathirika na mafuriko ikiwemo Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma na Kilosa mkoani Morogoro.

“Tayari Serikali imepeleka misaada ya kibinadamu ikiwemo mahema, vifaa vya kujihifadhi na mahitaji mengine muhimu yanayohitajika wakati wa maafa katika maeneo yaliyoathirika na maafa” alisisitiza Prof.Kamuzora

Katika kikao hicho Baraza litapitisha maamuzi ambayo yatasaidia katika usimamizi wa maafa nchini kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi, Idara zinazjitegemea chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuzingatia kuwa suala la maafa ni mtambuka.

Lengo kuu la kikao hicho ni kujadili Taarifa za Usimamizi wa Maafa na Misaada ya Kibinadamu, kujadili hatua zilizochukuliwa na Serikali kukabili na kurejesha Hali ya Tetemeko la Ardhi mkoani Kagera, taarifa za maghala ya Kanda na Vifaa vya Misaada ya kibinadamu, usimamizi, Mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika kukadili maafa.

Sambamba na hilo kikao kinalenga kupitia taarifa za mapendekezo ya ujenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Maafa nchini, taarifa za Utekelezaji wa Mkakati wa Afya Moja, taarifa za Hali ya Mlipuko wa Ugonjwa wa kipindupindu,  pamoja na Masuala ya Hali ya Hewa na Mfumo wa Kidunia wa Huduma  za  hali ya Hewa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Bashiri Taratibu alieleza kuwa Idara itaendelea kuratibu shulizi za Maafa nchiuni ili kuhakikisha suala la Menejimenti ya Maafa linaratibiwa kikamilifu ili kupunguza athariu zitokanazo na Maafa.

Kikao hicho kimefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Maafa namba 7 ya mwaka 2015 kinachoeleza masuala ya Menejimenti ya Maafa na kuhusisha Wajumbu kutoka Wizara mbalimbali ikiwemo; Wizara ya Fedha na Mipango, Kilimo,Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mamlaka ya Hali ya Hewa na Wakala wa Jiolojia Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Bashiri Taratibu akiongea wakati wa Kikao cha Baraza la Usimamizi wa maafa Tanzania kilichofanyika mapema leo mjini Dodoma, Katikati ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof. Fautin Kamuzora , kushoto Muwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Kanali Jimmy Said ambaye ni Makamu mwenyekiti wa Baraza hilo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof. Fautin Kamuzora (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Kikao cha Baraza la Usimamizi wa maafa Tanzania kilichofanyika mapema leo mjini Dodoma.


Sehemu ya Wajumbe wa Kikao cha Baraza la Usimamizi wa maafa Tanzania kilichofanyika mapema leo mjini Dodoma wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof. Faustin Kamuzora wakati wa Kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.