*Ni kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.
Amesema Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika shughuli nyingine jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Januari 20, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Bitiama katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere cha Mara.
Pia Waziri Mkuu aliagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Bw Solomon Ngiliule pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri Bw. Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo Bw. Robert Makendo.
Alisema viongozi hao wanatakiwa wachunguzwe kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwemo sh. milioni 12 walizotumia kuandaa profile ya Halmashauri hiyo.
Waziri Mkuu alisema fedha zingine ni pamoja na sh. milioni 70 za elimu maalumu, sh. milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazijulikani zimetumikaje. “Hatuwezi kuvumilia vitendo hivi fanyeni uchunguzi na naomba taarifa yake mara mtakapokamilisha.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliiagiza Taasisi ya Kuzuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara imkamate na kumuhoji Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoani Mara, Mhandisi Peter Salim baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Butiama.
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali ilitoa sh milioni 600 Aprili, 2017 kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya hiyo lakini hadi sasa wakala huo haujafanya kazi yoyote.
Katika maelezo yake Mhandisi Salim alisema ujenzi wa ofisi hiyo hadi kukamilika utagharimu sh. bilioni tatu, kati ya sh. milioni 600 zilizotolewa na Serikali sh milioni 400 zimetumika kujengea msingi, kauli ambayo ilipingwa na Mkuu wa wilaya hiyo Bibi Anna-Rose Nyamubi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu siyo kweli kwamba kuna kazi inayoendelea bali kilichopo pale ni mashimo ambayo hayajulikani ni ya nini. Pia kuna jengo moja lilijengwa kwa mabati kama stoo na hakuna mafundi wanaoendelea na kazi"
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali iko katika mchakato wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi za watumishi na kwamba haitamvumilia mtu yeyote atayekwamisha juhudi hizo.
Waziri Mkuu baada ya kuwasili wilayani Butiama akiambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa walizuru kaburi la Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere, katika Kijiji cha Mwitongo na kufanya mazungumzo na mjane wa Baba wa Taia, Mama Maria Nyerere.
Baada ya kuwasili katika eneo alilozikwa Mwalimu Nyerere, Waziri Mkuu na Mkewe waliweka shada la maua juu ya kaburi na kisha walishirikiana na wananchi kufanya maombi yaliyoongozwa na Chifu wa Wazanaki, Japheth Wanzagi.
Pia Waziri Mkuu alihutubia wakazi wa wilaya ya Butiama kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwenge, ambapo alitumia fursa hiyo kueleza juhudi mbalimbali za kuwaletea maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.