WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU
mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Makale kumkamata mkandarasi wa kampuni ya
Palimon baada ya kushindwa kukamilisha mradi wa mradi wa maji wenye thamani ya
sh. bilioni 2.06 wilayani Kwimba.
Ametoa agizo leo (Ijumaa, Februari 16, 2018) wakati akizungumza
na watumishi na wananchi kwenye kijiji cha Igumangobo wilayani Kwimba.
Mkandarasi huyo alianza ujenzi wa mradi huo Oktoba 28, 2013 na alitakiwa kukamilisha
Mei 28, 2014.
Waziri Mkuu amesema kitendo cha mkandarasi kutokamilisha
mradi huo kwa wakati licha ya kupewa fedha hakivumiliki, hivyo amemtaka kamanda
wa TAKUKURU kutafuta popote alipo na kumuhoji.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya wananchi wa vijiji
vya Mhande, Shirima na Izizimba ‘B’ ambao mradi huo unatekelezwa katika vijiji
vyao. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili mradi wao ukamilike na
wao wapate huduma ya maji.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la
Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kutotumia fedha za miradi ya
maendeleo kulipana posho.
“Fedha zinazopelekwa si za kulipana posho ni za maboresho na
Serikali inataka wananchi wahudumiwe wasipate shida.”
Waziri Mkuu amesema watumishi wahakikishe wanawahudumia
wananchi ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za
maendeleo.
Amesema wilaya hiyo imegeuka kama shimo la kuteketeza fedha
za Serikali kwa sababu miradi mingi inayotekelezwa haikamili, hivyo ameitaka
ijipange. Alitolea mfano sh. milioni 94 za ujenzi wa mradi wa kliniki ya mifugo
ambayo haijakamilika na fedha zimekwisha.
Awali, Waziri Mkuu alifungua mradi wa maji
wa kijiji cha Igumangobo kilichopo katika Tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba.
Chanzo cha maji hayo ni ziwa Victoria.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.