Monday, April 23, 2018

SPIKA EALA AIPONGEZA TANZANIA KWA MAENDELEO

SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dkt. Martin Ngoga ameishukuru na kuipongeza Serikari ya Tanzania kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa reli kwa sababu inaleta manufaa hata kwa nchi jirani.

"Miradi hiyo ambayo kwa sasa inatekelezwa kwa kasi si kwamba inachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania, bali hata wa nchi nyingi za jirani kwa kuwa nazo zitanufaika na miradi hiyo kwani si nchi zote zina bandari".

Dkt. Ngoga ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 23, 2018) alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Bungeni mjini Dodoma. 

Amesema tayari wamejadili ripoti iliyotokana na ziara iliyofanywa na wabunge hao katika upande wa korido ya kuishi na korido ya kaskazini ambapo wametoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na baraza la mawaziri.
"Tayari tumeshajadili miswada miwili inayohusu Itifaki ya Sarafu Moja ambayo ni mswada wa taasisi ya Fedha na  mswada wa Takwimu yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  ya mwaka 2017."
Pia Spika huyo amesema wamefurahia uwepo wao nchini, ambapo mbali na shughuli zao za kibunge pia kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wameshiriki kampeni ya kukijanisha Dodoma kwa kupanda miti 1,000 kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema amefarijika na uamuzi wa Bunge la EALA kufanya vikao vyake katika nchi wanachama kwa sababu unatoa fursa ya kujua mazingira ya nchi hizo pamoja na maendeleo yake.

Amesema nchi wanachama wanamatumaini makubwa na bunge hilo katika kuimarisha na kuboresha maendeleo ya mataifa yao,  hivyo amewatakia mjadala mwema.

Katika hata nyingine, Waziri Mkuu amewakaribisha wabunge hao na marafiki zao kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanja, utalii, kilimo na madini.

Kwa mara ya kwanza vikao vya Bunge la Afrika Mashariki, (EALA) vinafanyika Dodoma katika ukumbi wa Bunge wa Msekwa ulipo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vikao hivyo vilianza Aprili 17, 2018 na vinatarajiwa kumalizika Aprili 29, 2018.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.