Thursday, June 7, 2018

WAZIRI MKUU: SUALA LA MISHAHARA LINAFANYIWA KAZI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma liko Serikalini na linaendelea kushughulikiwa.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni 7, 2018) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Susan Lyimo kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kufahamu 
ni kwa nini Serikali ya awamu ya tano, tangu iingie madarakani, imeshindwa kuwalipa watumishi wa umma nyongeza ya mishahara ambayo ni stahili yao ya msingi.

“Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie suala la nyongeza ya mishahara liko Serikalini na Mheshimiwa Rais ameshawahikikishia wafanyakazi kuwa atawaongeza mishahara lakini siyo lazima litangazwe hadharani, na pia mshahara ni wa mtu binafsi kwa hiyo hata ikiongezwa leo huwezi kujua kwa kuwa hatujatangaza.”

“Hatuwezi kutangaza kwamba tumeongeza mishahara kwa kiwango hiki; tukishafanya hilo tayari tunaleta kupanda kwa gharama za maisha na sisi Serikali tuna mkakati wa kupunguza gharama za watumiaji kwenye masoko ili Watanzania wote wamudu kununua,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema mtumishi anapolipwa, anakuta mshahara wake kwenye akaunti yake. “Na hata tunapolipa madeni hatutangazi, lakini kila mtumishi ambaye anadai, anaona malipo yanalipwa kupitia mshahara wake na hiyo sasa inasaidia pia kuchangia hata kwenye pensheni,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inachelea kutangaza nyongeza za mishahara hadharani ili kupunguza athari ambazo zinawapata watumishi hao na jamii kwa ujumla. “Si kwamba Serikali haikusudii kutoa nyongeza ya mishahara kwa mwaka, lakini unapotumia Mei Mosi kutangaza nyongeza ya mishahara unaleta athari kwenye jamii kwa sababu vitu vinaweza vikapanda bei, gharama hizi zikawasumbua pia na wananchi ambao hawalipwi mshahara,” amesema.

Amesema nyongeza za mwaka zinaendelea kutolewa kulingana na namna ambavyo Ofisi ya Rais (Utumishi) wameratibu. “Serikali yetu inao utaratibu wa kuwapa stahiki watumishi kadri wanavyotakiwa kuzipata na utaratibu huu unaratibiwa vizuri sana na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako tunayo orodha ya watumishi wote nchini. Orodha hii tulianza kufanya sensa ili kutambua watumishi halali na sasa kazi hiyo imekamilika; tunaendelea na uboreshaji wa maeneo yote hayo ikiwemo na nyongeza za mwaka, nyongeza za mishahara, upandishaji wa madaraja ikiwa ni stahiki za watumishi wetu.”

Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma waendelee kuiamini Serikali wakati ikiendelea kushughulikia maslahi yao hasa kwa vile ililenga kuokoa fedha za umma zilizokuwa zikipotea kwa kuwalipa watu ambao hawastahili.

“Naomba tu niwaeleze watumishi wa umma kwamba, kwanza wawe na imani na Serikali, mpango tuliouweka unasababisha Serikali kutopoteza fedha nyingi kwa kulipa watu ambao hawastahili; lakini, baada ya kuwa tumekamilisha taratibu hizi, sasa tunaweza kuendelea kulipa stahiki za watumishi. Tumeshaanza kulipa madeni ya watumishi ambapo Mheshimiwa Rais alitenga zaidi ya shilingi bilioni 200, wiki mbili au tatu zilizopita wameendelea kulipwa kwa awamu,”.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.