|
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof.Faustin Kamuzora (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali alipowatembelea Julai4, 2018.
NA.MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof.Faustin Kamuzora amewataka watumishi wa Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali kuzingatia ubora na ufanisi katika uchapaji wa nyaraka za Serikali.
Wito huo ameutoa hii leo Julai 4, 2018 alipotembelea katika Idara hiyo ili kuangalia namna wanavyoendesha shughuli zao za kila siku.
Prof.Kamuzora alieleza umuhimu wa kuendelea kuwa na ubunifu katika utendaji kwa kuzingatia unyeti wa nyaraka za Serikali wanazochapisha na kuongeza wigo wa uzalishaji kwa kuwa na machapisho yenye ubora na viwango vya kuendana na soko ili kuongeza mapato ya nchi.
“Niwaombe watumishi wote mzingatie uzalishaji wenye tija kwa kuchapisha nyaraka zenye ubora na ufanisi utakao saidia kuongeza mapato ya nchi hivyo ni vyema kuwa na ubunifu wa hali ya juu,”alisema Prof.Kamuzora
Pamoja na maagizo hayo aliwasisitiza kuzingatia uzalendo wa nchi yao kwa kuwa waadilifu katika kuitumikia kwa uaminifu bila kutoa siri za Serikali.
“Ni lazima mzingatie maadili ya utumishi wa umma kwani Idara hii ni nyeti inayoshughulika na uchapaji wa nyaraka za Serikali hivyo ni lazima kuwa na namna bora ya uendeshaji wa shughuli zenu kwa kuaminiana na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine,”alisisitiza Prof.Kamuzora
Kwa upande wake Kaimu Mpigachapa Mkuu wa Serikali Bw.John Kaswalala alimpongeza Katibu Mkuu kwa kuona umuhimu wa kuitembelea Idara hiyo, na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo aliyotoa kwa lengo la kuboresha utendaji wa Idara ili kuwa na uzalishaji wenye tija na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
“Kipekee nikushukuru kwa kuona umuhimu wa kuitembelea idara hii na kujua mazingira na changamoto za kiutendaji, nimefarijika kwa hatua hii hivyo tumeyazingatia maagizo yote tutayatekeleza ili kuendana na soko na mabadiliko ya kiteknolojia nchini,”alisisitiza Kaswalala.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.