Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) waajiri mameneja wenye sifa ili kuepuka ubadhirifu ndani ya vyama hivyo.
Ametoa rai hiyo jana (Jumamosi, Julai 7, 2018) wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini humo.
Amesema watumishi ambao wamepata nafasi za juu katika AMCOS ni lazima wawe na elimu ya ushirika kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU). "Utumishi katika hivi vyama mara nyingi unaenda na uaminifu. Kama Chama kikiona kina mtu wanayemwamini, ni lazima kimpeleke chuoni ili apate sifa stahiki," alisema.
Alisema anataka kuona huduma za ushirika kwa wananchi zikiwianishwa na kile wanachofundishwa wataalamu kwenye vyuo vya elimu ya juu.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemwagiza Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi ahakikishe wanafunzi wanaopangiwa kufanya mafunzo kwa vitendo (field training) wanasambazwa kwenye AMCOS mbalimbali nchini.
"Wanafunzi wanaoenda field training kutoka kwenye Chuo chako, wapangiwe kwenda katika AMCOS. Hapa nchini tuna zaidi ya AMCOS 4,000 na wanafunzi wako 1,000 kwa hiyo kila mmoja akisimamia AMCOS nne, nne, watakuwa wamesaidia sana kupeleka elimu ya ushirika huko vijijini.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba na Naibu wake Dkt. Mary Mwanjelwa. Wengine ni Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula, Wakuu wa Mikoa ya Kagera, Mara, Simiyu, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa CCM.
Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa Jumamosi ya kwanza ya Julai kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ushirika kwa ulaji wa uzalishaji endelevu wa bidhaa na huduma.”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.