*Ataka watenge siku
tatu hadi nne waende waliko wananchi
*Asema Serikali
hii haitaki mambo ya urasimu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
watumishi wote wa Serikali za Mitaa nchini watenge theluthi mbili ya muda wao
wa kazi kwa kuwasikiliza wananchi na kuwahudumia.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili,
Julai 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi
na viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, wilayani
Kahama mkoani Shinyanga.
“Jukumu la watumishi ni kuwatumikia wananchi,
Serikali hii hatutaki urasimu na wala hatutarajii kuwa mtatoa huduma kwa
urasimu. Lugha ya ‘njoo kesho, njoo kesho’ siyo ya kwa awamu hii.”
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wana
jukumu la kusimamia agizo hilo kwa kuhakikisha kuwa wanatoa usafiri kwa
watumishi hao ili waweze kufika vijijini kwa haraka. “Wakurugenzi wa
Halmashauri simamieni zoezi hilo kwa kupanga ratiba na kutoa gari ili maafisa
wanne au watano watumie gari hilo kwenda vijijini wakawahudumie wananchi.”
Amesema wananchi wengi hawana uwezo wa kusafiri kutoka
vijijini hadi mijini ili kuleta matatizo yao, kwa hiyo wakifanya hivyo, watumishi
watakuwa wamewapunguzia matatizo wananchi.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya
kikazi mkoani humo, amewataka watumishi wa idara ya ardhi wapime ardhi kwa
wingi na watoe hati mapema ili wananchi wazitumie kuongeza mitaji.
“Pimeni ardhi na kutoa hati ili wananchi wazitumie
kukopa na kupata mitaji ya kujiendeleza kiuchumi. Pia muweke mipango mizuri ya
ardhi ili kuepusha migogoro baina ya wananchi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.