WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon amemaliza ziara yake ya kiserikali ya siku tatu hapa nchini na kusindikizwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo wa Korea ambaye ameondoka leo (Jumatatu, Julai 23, 2018) saa 9.14 alasiri, ameelekea Oman ambako atakuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili. Aliwasili nchini juzi akitokea Kenya ambako pia alikuwa na ziara ya siku mbili.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu wa Korea Kusini alisindikizwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam
Kabla ya kuondoka alishuhudia burudani kutoka vikundi vya ngoma na matarumbeta uwanjani hapo.
Mara baada ya mgeni wake kuondoka, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na wasanii waliokuwepo uwanjani na kuwapongeza kwa kujitokeza kutoa burudani kila wakati wageni wanapoitembelea Tanzania.
“Tunawashukuru sana wasanii kwa sababu mlikuja wakati wa mapokezi ya mgeni wetu na sasa mmekuja tena kumsindikiza. Mgeni wetu amefurahia sana ngoma zetu na amesema atarudi tena Tanzania.”
“Kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, tunatambua kuwa mnajitoa muda wenu kila mnapokuja kupokea na kusindikiza wageni ili kuweka sura nzuri ya Taifa letu wakati wa kupokea wageni wetu, tunawashukuru sana,” amesema.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.