Saturday, August 4, 2018

WAZIRI MKUU AUPONGEZA UONGOZI WA MAKUMBUSHO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuchora ramani ya Tanzania katika Kijiji cha Makumbusho ambayo itatumika kwenye ujenzi wa nyumba za utamaduni wa makabila mbalimbali nchini.

Amesema uamuzi huo utarahisisha watu kufika kwa urahisi katika nyumza za tamaduni za mikoa yao kwa kuwa watakuwa wanatumia ramani Tanzania.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumapili, Agosti 4, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Lindi kwenye kikao cha kujadili maandalizi ya Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania katika Kijiji cha Makumbusho, jijini Dar es Salaam.

“Kwa kutumia ramani hii kila mkoa utaweza kufika kwenye eneo lake kwa kutumia ramani ya Tanzania na mkoa wa Lindi tayari umeshaoneshwa eneo lake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba inayozingatia utamaduni wetu,” alisema.

Alisema kwa tamaduni za makabila ya mkoa wa Lindi nyumba zote hujengwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti upande wa maeneo ya pwani ya upande mwingine huezeka kwa nyasi, ambapo aina zote zitajengwa ili kuwakilisha tamaduni za wakazi wa mkoa huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaasa wananchi wa mkoa wa Lindi ambao kwa mwaka huu ndio waandaaji wa tamasha hilo wadumishe mshikamano wao ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea katika kuboresha maendeleo.

Alisema katika tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuanza Agosti 26 hadi 29 wahakikishe wanapeleka kila kitu ambacho kinahusiana na utamaduni wa mkoa huo ili kuwawezesha Watanzania wengine wajue kama vyakula na mavazi .

Pia alishauri wawepo wazee wenye kujua historia ambao watasimulia utamaduni wa wananchi wa Lindi pamoja na kutambulisha ngoma zao za utamaduni. “Halmashauri zote za mkoa wa Lindi zitumie fursa hii kutangaza vivuti vya utalii vilivyopo na Kilwa walete mtu atakayeelezea kuhusu magofu,”.

Waziri Mkuu alisema tamasha hilo ni muhumu kwa sababu utamaduni ulianza kufifia nchini kutokana  na mabadiliko ya kiteknolojia jambo ambalo lingeweza kuuondoa katika kumbukumbu, hivyo aliwashauri siku ya tamasha hilo wavae nguo za kitamaduni kulingana na kabila husika.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi wa mkoa wa Lindi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Godfrey Zambi kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri mwenendo wa zao la korosho.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Profesa Audax Mabulla alisema mwaka huu Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania linawakilishwa na jamii kutoka mkoa wa Lindi na kwamba anatumaini watafanya vizuri kwa kuwa uwezo na nia wanayo.

Profesa Mabula alisema mwaka 1994 Bodi ya Makumbusho ya Taifa ilianzisha siku ya utamaduni ili kutoa fursa kwa jamii mbalimbali nchini kuonesha utajiri walionao katika tamaduni zao na ufanisi wa siku hiyo unatokana ushirikishwaji wa wanajamii husika.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.