SERIKALI imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani ili kupata masoko ya uhakika ya zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo (Alhamisi, Novemba 8, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.
Mbunge huyo alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu bei ya korosho ambayo imeshuka katika msimu wa mwaka huu hadi kusababisha wakulima kugomea baadhi ya minada, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali.
“Tunaendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa ili tujue ni nani atanunua korosho na kwa kiasi gani, hivyo tunawaomba wakulima waendelee kuwa watulivu, Serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linatafutiwa masoko. Korosho zitanunuliwa tu.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya ujenzi wa viwanda vya mbolea, ambapo inatoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vikiwemo vya pembejeo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mgaya aliyetakakujua Serikali ina mpango gani katika kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya mbolea ili wakulima waweze kuipata kwa gharama nafuu.
Amesema viwanda vya mbolea vilivyopo nchini ni vichache na havitoshelezi mahitaji, hivyo kwa sasa kuna utaratibu wa kujenga viwanda vingine viwili kimoja kitajengwa Kilwa mkoani Lindi na kingine kitajengwa Mtwara. Kukamilika kwa viwanda hivyo kutaongeza uzalishaji wa mbolea na kupunguza uagizaji kutoka nje ya nchi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amefafanua kuhusu suala la wakulima wa mahindi kukosa masoko, ambapo amesema ruhusa ya kuuza mahindi nje ya nchi ilishatolewa. Amesema jambo hilo lilitolewa ufafanuzi na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba.
Waziri Mkuu amesema licha ya kuwepo kwa kibali cha kuuza mahindi nje ya nchi ni lazima Serikali itambue kiasi gani kinachotolewa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, hivyo muuzaji anatakiwa awasisilishe taarifa zake kwa wakuu wa wilaya. “Tunahitaji kuwa na takwimu za mauzo na bei ili kujua kiasi kilichouzwa pamoja na kiasi cha fedha kilichopatika.”
Kuhusu upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu ikiwemo mbolea, Waziri Mkuu amesema suala hilo linaratibiwa vizuri na Wizara ya Kilimo na tayari asilimia 60 ya mahitaji ya pembejeo tayari imeshaingia nchini, hivyo Serikali itahakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Lucia Mlowe, Mbunge wa Viti Maalumu aliyehoji Serikali inatoa tamko gani kuhusu tatizo kubwa la wakulima wa mahindi kukosa masoko ya uhakika.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.