*Yawataka waandike barua wakionesha tani wanazohitaji na lini watazichukua
*Yasema zaidi ya hapo haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena
SERIKALI
imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho
wawe wamepeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha
tani wanazohitaji na lini watazichukua.
“Hivyo
wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa
wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya
siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe
wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24.”
Hayo
yamesemwa leo (Ijumaa, Novemba 9, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho,
ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Baada
ya kupita siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote
waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua
lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho
imesema haitakubaliana nacho.
“Mwenye
nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho
na waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24 wana nafasi ya
kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango
wanachokihitaji. Zaidi ya hapo Serikali haitoruhusu kampuni yoyote
kununua korosho tena.”
Waziri
Mkuu amesema kwenye msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu,
walishuhudia kusuasua kwa minada, ambapo Serikali ilikutana na wanunuzi
wa korosho katika kikao kilichoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambapo
walikubaliana kununua kwa bei inayoanzia sh 3,000 na kuendelea.
“Mjadala
ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo
ilikuwa inaanzia sh. 3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi
katika minada imeendelea kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa
zilikuwa kidogo sana. Sisi tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si
sawa sawa sana kwani malengo yetu sisi na sekta binafsi ni kumfanya
mkulima apate bei nzuri.
Hali
hii haifurahishi kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha mazao
yanayolimwa na wakulima kwa kuwasaidia kuanzia katika hatua za
utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na masoko ili waweze
kunufaika na kilimo na kupata tija katika mazao hayo.”
Waziri
Mkuu amesema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo Serikali ilifanya
jitihada za kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na
kupata bei halisi ambayo bado inatosha kumlipa mkulima sh 3,000.
Hatua
hiyo imekuja baada ya zao la korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya
chini na idadi ya wanunuzi kuwa ya chini licha ya uzalishaji wa mwaka
huu kuwa mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka jana.
Amesema
msimu wa mwaka jana uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na mwaka
huu zinatarajiwa tani zaidi ya 200,000 hivyo wafanyabiashara wanao uwezo
kununua korosho zilizopo.
Hata
hivyo Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini
kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia
suala hilo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.