Tuesday, November 6, 2018

WATANZANIA KUFAIDI MATUNDA YA RELI YA KISASA MWAKANI

*Waziri Mkuu alidhishwa na kasi ya ujenzi
*Asilimia 96 ya walioajiriwa ni Watanzania


MIUNDOMBINU ni muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote ambalo linalohitaji kusonga mbele kiuchumi, kijamii kwa sababu husaidia Serikali katika kufanikisha malengo iliyojiwekea.

Miundombinu hiyo ambayo inalenga kuboresha na kuimarisha uchumi inajumuisha ujenzi wa miradi mbalimbali ya uchukuzi na usafirishaji kama reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, ununuzi wa ndege na meli.

Kukosekana kwa miundombinu ya uhakika kunachangia kupanda kwa gharama za maisha kutokana na kuongezeka gharama za uchukuzi.

Katika kutambua umuhimu wa miundombinu kwenye kukuza uchumi Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeamua kujikita katika kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ili kuhakikisha Taifa linasonga mbele kiuchumi.

Mradi huo wa ujenzi wa mfumo wa reli mpya ya kisasa (SGR) unaojengwa na Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), unatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam na Mwanza ina urefu wa km. 1,219.

Jumamosi, Novemba 3 mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kutembelea ujenzi wa reli hiyo kuanzia eneo la Shaurimoyo (Dar es Salaam) hadi Soga (Pwani) ambapo alisema ameridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi huo.

Alisema kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km. 300 kinatarajiwa kukamilika Novemba 2019 na kipande wa cha kutoka Shaurimoyo hadi  eneo la Pugu chenye urefu wa km. 20 ambacho kilipangwa kukamilika Julai 2019, lakini kwa kasi ya mkandarasi kitakamilika Machi 2019.

“Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi kwa sehemu ulivyofikia pamoja na ushiriki wa Watanzania wengi katika mradi huu, tunataka muendelee kujenga kwa kasi hii na kiwango hikihiki. Kazi mnayoifanya inavutia,” alieleza.

Waziri Mkuu alisema Serikali inataka kuona malengo ya Rais Dkt. Magufuli ya kutaka kuona SGR  inakamilika kwa wakati na kuanza kutumika nchini yanatimia kwani wananchi nao watakuwa wamerahisishiwa usafiri.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani hususani ambazo hazijapakana bahari pamoja na kupunguza muda wa safari katika maeneo ambayo mradi huo unapita.
Pia  itasaidia katika kutunza barabara na kupunguza gharama za ukarabati wa mara kwa mara kwa sababu mizigo mingi itakuwa inasafirishwa kwa njia ya reli na maroli yatapungua barabarani, hivyo kuzifanya ziwe imara na kudumu.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa SGR inakwenda kukuza sekta zingine za kiuchumi nchini kwa sababu nazo zinategemea uimara wa miundombinu ya usafiri wa uhakika.
Katika  sekta ya viwanda reli hiyo itasaidia kusafirisha bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda mbalimbali na kuwafikia watumia kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Akizungumzia kuhusu suala la ajira katika ujenzi wa mradi wa SGR, Waziri Mkuu alisema amefarijika kusikia asilimia 96 ya watu walioajiriwa katika mradi huo ni Watanzania, amewataka wawe mabalozi wazuri.
“Watanzania mnaofanya kazi katika mradi huu, hakikisheni mnawajibika kwa kufanyakazi kwa bidii, uadilifu na muwe mabalozi wazuri ili wananchi wengine waweze kupata ajira kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini ikiwemo ya ujenzi.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mradi huo wa reli  kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora unagharimu sh. trilioni 7.1.

Alisema awamu hiyo ya mradi wa ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa km 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umegawanyika katika vipande vitano, kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu km 300 na njia kuu 205 ambazo km 95 zitakuwa zinapisha kitagharimu sh. trilioni 2.7.

“Kipande kingine ni kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa km. 422  na njia kuu 336 ambazo km 86 zitakuwa zinapishana kitagharimu sh. trilioni 4.4, Makutupora hadi Tabora km. 376.5 chenye njia kuu 294 na km 73.5 zitakuwa zinapishana.

Kipande kingine ni cha kutoka Tabora hadi Isaka km 162.5 chenye njia kuu 130 na km 32.5 zitakuwa za kupishana na Isaka hadi Mwanza km. 311.25 njia kuu 249 huku km 62.5 zitakuwa za kupishana.”

Mkurugenzi huyo alisema kukamilika kwa reli hiyo ya kisasa itachochea mipango ya Serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza sera ya Tanzania ya viwanda na kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia Mkurugenzi huyo alisema reli hiyo itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususan kwa nchi zisizopakana na bahari kwani watasafirisha mizigo yao kwa haraka na uhakika.

“Kuchangia katika pato la Taifa na sera ya viwanda kwani mradi huo umeongeza mahitaji ya saruji, kokoto, nondo pamoja na vifaa vingine vya ujenzi, hivyo kuvifanya viwanda vyetu vya ndani kupata soko la bidhaa zake.”

Akizungumzia mradi huo kwa ujumla, Mkurugenzi huyo alisema maendeleo ya mradi huo ni asilimia 32 kwa kipande cha Dar es Salaam-Morogoro na asilimia 3. 31 kwa kipande cha Morogoro-Makutupora.

Alisema jumla ya km. 722 za ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa kwa sasa zinatekelezwa katika vipande viwili, kipande cha Dar Es Salaam-Morogoro km. 300 kinajengwa kwa ubia wa kampuni ya YAPI MERKEZI ya Uturuki na MOTA-ENGIL ya Ureno na kipande wa Morogoro-Makutupora km. 422 kinajengwa na kampuni ya YAPI MERKEZI.

Kadogosa alisema katika mradi huo wa reli za kisasa mfumo wa uendeshaji wa treni utatumia nishati ya umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na tayari taratibu za kumpata mkandarasi za kujenga njia za umeme upo katika hatia za mwisho.

Kuhusu ujenzi wa madaraja Kadogosa alisema kazi ya ujenzi wa madaraja na makaravati unaendelea ambapo daraja refu katikati ya jiji la Dar es Salaam ina jumla ya urefu wa km. 2.56 na ujenzi wake umefikia asilimia 46.

 “Kuna madaraja ya kati 26 na makaravati 243, madaraja ya treni kupita juu yapo 17, madaraja ya treni kupita chini yapo 15 na madaraja reli juu ya reli yapo matano, pia jumla ya stesheni sita zitajengwa kati ya Dar es Salaam na Morogoro, kati ya hizo kubwa zitakuwa mbili na nne zitakuwa ndogo.”

Alisema usanifu wa stesheni hizo umezingatia mazingira na asili ya Tanzania ambapo stesheni ya Dar es Salaam ina sura ya madini adimu ya Tanzanite wakati stesheni za kati usanifu wake umezingatia utamaduni na nyumba za asili na stesheni ya Morogoro itaonesha uhalisia wa milima ya Uruguru.

Kadhalika, Mkurugenzi huyo alizungumzia kuhusu ajira katika mradi huo ambapo alisema una jumla ya wafanyakazi 5,440, vibarua 4,743 ambapo jumla ya asilimia 96 ni Watanzania na asilimia nne ni wageni, wataalamu 189 wa Kitanzania na 258 wa kigeni kwa uwiano wa asilimia 42 Watanzania na wageni asilimia 58.

Pia jumla ya ajira 626 za Watanzania wasio na utaalamu na 19 za wenye utaalamu zimepatikana kupitia kampuni za wazawa (sub-contractors) wanaoshiriki moja kwa moja kwenye mradi huo.

Akizungumzia kuhusu ardhi na mali nyingine, Kadogosa alisema mali za wananchi wapatao 6,514 zenye thamani ya kiasi cha sh. bilioni 83.099 zitakiwa kuhamishwa ili kupisha ujenzi wa reli kwa kipande wa Dar es Salaam-Morogoro.

(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.