Thursday, December 6, 2018

WAKUU WA MIKOA NA MAKATIBU TAWALA WAPIGWA MSASA JUU YA SHERIA YA USIMAMIZI WA MAAFA


Na. OWM, DODOMA.
Timu ya wataalamu wa Ofisi ya waziri Mkuu wanaohusika na shughuli za kuratibu usimamizi wa maafa nchini, pamoja na timu ya wataalamu wa uokoaji ya Mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa. Faustin Kamuzora wametoa elimu kwa wakuu wa mikoa na makatibu Tawala, juu ya menejimenti ya maafa nchini.
Akiongea wakati wa uwasilishaji mada za usimamizi wa maafa nchini kwenye mafunzo ya uongozi kwa viongozi hao yanayoendelea mjini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Faustin Kamuzora amewashauri viongozi hao kuizingatia sheria ya usimamizi wa maafa nchini ya mwaka 2015 inayozitaka kamati za maafa kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kutafuta rasilimali za usimamizi wa maafa katika ngazi husika.
“Ningependa niwashauri tumieni kamati zenu katika mkoa na wilaya ambazo zitawasaidiia kujua rasilimali mlizo nazo na kujua utaalamu wa kutumia, hivyo mtaweza kujenga uwezo mkubwa wa kukabili maafa yanayowapata na hayatahitaji kufika ngazi ya kitaifa na kwa kuzingatia ngazi ya kitaifa tunategemea mfuko wa maafa ambao bajeti ni finyu hivyo jitahidini kutumia rasilimali zenu katika kujiandaa zaidi kuliko kusubiri kutumia rasilimali nyingi wakati wa kukabili“ Amesisitiza,  Kamuzora.
Awali akiongea katika Mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Timu ya Wataalamu wa uokoaji ya Dar es Salaam, Dkt. Christopher Mzava, alifafanua kuwa timu hiyo imeundwa mahususi na mkoa huo ili kuwezesha kamati ya maafa ya mkoa huo kufanya shughuli za usimamizi wa maafa  kwa weledi, tayari imefanikiwa kuzijumuisha asasi na taasisi zote za Serikali, zisizo za Kiserikali na za watu Binafsi zinazoshughulika na maafa katika Mkoa huo na kutengeneza Mpango mkakati wa kukabili maafa mkaoni humo.
Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha  majukumu ya  kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja na  Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji  wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akifafanua juu ya masuala ya menejimenti ya maafa wakati wa  majadiliano  ya mada ya Usimamizi wa maafa nchini kwa Wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wanaohudhuria mafunzo ya Uongozi  yanayoendelea mjini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akifuatilia majadiliano wakati wa  majadiliano  ya mada ya Usimamizi wa maafa nchini kwa Wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wanaohudhuria mafunzo ya Uongozi  yanayoendelea mjini Dodoma.

Baadhi ya Makatibu tawala wakifuatilia uwasilishaji wa mada ya Usimamizi wa maafa nchini, kwa Wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wanaohudhuria mafunzo ya Uongozi  yanayoendelea mjini Dodoma.

Mratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka akiwasilisha mada juu ya Dhana ya Maafa,  kwa Wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wanaohudhuria mafunzo ya Uongozi  yanayoendelea mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Timu ya Uokoaji mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Christopher Mzava akiwasilisha jinsi Mkoa wa Dar es salaam ulivyoweza kutekeleza Sera ya maafa,  kwa Wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wanaohudhuria mafunzo hayo  yanayoendelea mjini Dodoma.

 MWISHO.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.