Na.
OWM, Kigoma.
Ofisi ya Waziri Mkuu chini
ya Baraza la Taifa la Biashara, kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya
Biashara na Uwekezaji unaotekelezwa katika mkoa wa Kigoma na Dodoma,
umefanikiwa kuboresha Mazingira ya Biashara na uwekezaji katika mikoa hiyo kwa
kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 16 hadi
kufikia Desemba 2018.
Mradi huo ambao utekelezaji
wake unajikita katika Uwekezaji na Biashara katika Halmashauri kupitia mfuko wa
(SIFF), Kuimarisha minyororo ya thamani pamoja na kuimarisha majadiliano kati
ya Serikali na Sekta Binafsi, tayari umefanikiwa kuboresha Mazingira ya
Biashara kwa Wakulima na wavuvi wa mkoani Kigoma.
Akiongea katika ziara yake
mkoani Kigoma wakati wa kukagua shughuli za utekelezaji za Baraza la Taifa la
Biashara, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana
na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amefafanua kuwa Baraza la Taifa la
Biashara kwa kushirikiana na Mradi huo wameweza Kuwawezesha wananchi kiuchumi
kupitia uwekezaji kwenye miradi midogo midogo inayochochea ongezeko la ajira na
kipato.
“Nimetembelea Mwalo na Soko la Samaki la Kibirizi,
hapa mkoani Kigoma nimeridhishwa jinsi Mradi huu ulivyoboresha miundo mbinu ya mwalo
huu katika kuhakikisha wavuvi wanapunguza upotevu wa mazao ya samaki na dagaa.
Niyaombe Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya yaendelee na mfumo wa
majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha walengwa wa mradi
huu wanaendelea kunufaika” Alisisitiza Mhagama.
Mhagama alifafanua
kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kupunguza
vikwazo na kero kwa wafanyabiashara lakini pia Kuimarishwa kwa mahusiano kati
ya Serikalii na Sekta Binafsi na kuongezeka kwa
ushirikishwaji wa Sekta Binafsi
katika Mipango ya Serikali.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo, Mratibu
wa Mradi (Masuala ya Majadiliano ya Sekta ya Umma na Binafsi), Andrew Mhina
alibainisha kuwa Mradi huo unalenga kuhakikisha kuwa unaboresha mazingira ya
Biashara na uwekezaji nchini tayari
umeandaa mwongozo wa Majadiliano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi ngazi ya Mkoa
na Wilaya ili kuyajengea uwezo Mabaraza ya Mikoa yaweze kuwa endelevu na yenye ufanisi
ambapo Baraza la Taifa la Biashara kwa kushirikiana.
Katika ziara hiyo, Waziri Mhagama, pamoja na
kutembelea mwalo wa soko la Samaki la Kibirizi waziri alitembelea Kituo cha
Biashara (One Stop Business Centre – Kigoma), Soko la Jioni la Mwanga, na Mradi
wa Kuwezesha Vijana Kushiriki katika Kilimo Biashara na Mnada wa Mifugo Buhigwe.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.