Na. OWM, SUMBAWANGA.
Ofisi ya Waziri Mkuu,
Idara ya Uratibu wa Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa maafa nchini
kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kuwa na mpango wa Kujiandaa na kukabili maafa ili
kuwa na uwezo wa utayari wa kujiandaa na
kukabili maafa kwa ufanisi.
Akiongea wakati wa
mafunzo kwa Kamati ya Usimamizi ya Maafa ya Mkoa wa Rukwa, juu ya Usimamizi wa
Maafa kwa Mujibu wa Sheria ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti
na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu, alifafanua kuwa Mpango huo
ni muhimu kwa kuwa huainisha majukumu na hatua zitakazochukuliwa na Kamati
za maafa kuanzia ngazi ya kijiji, wilaya na mkoa pamoja na
wadau wengine wa maafa.
“Ili kuweza kukabiliana
na maafa pindi yanapotokea na kuhakikisha kuwa wanazuia au kupunguza athari za maafa
yanapotokea kwa ufanisi tumeishauri kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa
Rukwa katika bajeti ijayo watenge bajeti kwa ajili ya maafa, pia wabuni mbinu za upatikanaji wa rasilimali
zinazohitajika katika usimamizi wa maafa, hili linawezekana iwapo kamati zote nchini za Usimamizi
wa maafa katika ngazi zote zikiwa na Mpango
wa kujiandaa na kukabili maafa” alisisitiza Taratibu
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya Mkoa wa Rukwa , Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa
huo, Winnie Kijazi, aliihakikishia ofisi ya Waziri Mkuu kuwa mkoa huo umeamua
kuandaa mpango huo kutokana na changamoto walizo zipata wakati wa maafa ya mvua
yenye upepo mkali uliotokea mwishoni mwa
mwaka jana katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na Nkasi.
“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri
Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa uratibu na misaada ya haraka pindi tulipopata
maafa , na sisi tumeamua kuwa na ufanisi katika usimamizi wa maafa kwa kuandaa
Mpango wa Kujiandaa na Kukabili maafa na tutaelekeza wilaya zote kuandaa
mipango yao na kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji huo”
alifafanua Kijazi
Naye Mratibu wa maafa
mkoani Rukwa Aziza Kalyatiilya alieleza kuwa, tayari wameandaa Mpango wa kutoa elimu
ya Maafa kwa Umma ili kuijengea jamii uwezo wa kujiandaa,
kuzuia, au kukabili na kurejesha hali kwa haraka na ufanisi pindi maafa
yatakapotokea mkoani humo.
Mnamo mwezi Desemba
mwaka jana Halimashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa zilipatwa
na maafa ya mvua yenye upepo mkali iliyosabaisha vifo, uharibifu wa mali na
Miundo mbinu. Aidha Kamati ya maafa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu, Idara
ya Uratibu Maafa, tayari shughuli za kurejesha hali zinaendelea.
Kwa
mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha
majukumu ya kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi
mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutafuta rasilimali
kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja na Kuratibu
na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya
Kijiji wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo
husika.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.