*Ataka kampuni
ya Mzinga Holdings isimamiwe kwa karibu
*Ahimiza
tarehe ya mwisho ni Januari 31, mwaka huu
ZIKIWA zimepita siku 20 tangu akague
ujenzi wa mji wa Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na
ujenzi unaoendelea katika eneo la Mji wa Serikali lililoko Ihumwa.
Hata hivyo, amesema kampuni ya ujenzi
ya Mzinga Holdings inahitaji kusimamiwa kwa karibu zaidi ili ikamilishe ujenzi
wa majengo yake kabla ya Januari 31, mwaka huu. “Nitakuja kukagua kazi na
kupokea funguo za ofisi siku hiyo,” amesema.
Ametoa kauli hizo leo mchana (Alhamisi,
Januari 16, 2019) mara baada ya kukagua ujenzi wa
ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo
la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye alianza kukagua
ujenzi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, ametembelea majengo ya wizara zote na
kubaini bado kuna changamoto zinazojitokeza kutokana na utendaji wa mazoea
miongoni mwa watumishi wa Serikali.
Akiwa katika jengo la Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri Mkuu alipokea malalamiko kutoka kwa meneja
mradi, Bi. Selemina Rwehumbiza kwamba aliandaa certificate tangu tarehe 13 Januari lakini hadi sasa hajapata
malipo. Alipofuatilia, alijibiwa na mshauri mwelekezi kwamba wamepokea certificate hiyo jana jioni (Jumatano,
Januari 16, 2019).
“Kama kazi hii muhimu ya Mheshimiwa
Rais, na anayesimamia ni Waziri Mkuu inacheleweshwa hivi, je akija mwananchi wa
kawaida huko ofisini kwenu atachukua muda gani kupatiwa huduma?,” Waziri Mkuu
alimhoji Mshauri Mwelekezi wa mradi huo kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Mhandisi
Hilary Msaki.
“Huu ni mfano halisi wa malalamiko
yanayotoka huko nje kwamba Serikali haijibu barua za wananchi. Sasa nyaraka
kutoka hapa Mtumba inachukua wiki nzima kwenda mjini, na mtu bado hajajibiwa.
Sielewi ni kwa nini barua iende hadi mjini, wakati wakandarasi wako huku. Kwa
nini ninyi msipokee hizo nyaraka na kuzikimbiza mjini kisha mrudishe majibu
hapa site?”, alihoji Waziri Mkuu.
“Kuanzia sasa, kazi zote mpokee ninyi,
na ninyi ndiyo mzipeleke huko mjini na kurudi na majibu hapa site kwa wateja wenu, kwani wakandarasi
wote wako hapa,” alisisitiza.
Akiwa katika eneo la Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri Mkuu alielezwa na Waziri Ummy Mwalimu
kwamba wana changamoto ya kutopatiwa taarifa za maendeleo ya mradi. “Tangu
mradi unaze hatujapewa taarifa hata moja, wakurugenzi wapo wanakuja, lakini
mshauri mwelekezi hatupi ripoti yoyote juu ya huu mradi,” alisema.
Alipohoji ni kwa nini taarifa
hazitolewi, Waziri Mkuu alibaini kuwa hata watu wa TEMESA pia hawakuwepo kwenye
zoezi hilo la ukaguzi. “Niliagiza TBA wahamie hapa, nao wameweka ofisi yao hapa
hapa. Nimeulizia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wako wapi, nikaambiwa wako
mjini. Ni kwa nini hawako hapa?” alihoji.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa
tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu alisema pamoja na
spidi anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora
unaotakiwa (quality).
Alisema kwa ujumla kazi nyingi
zimeboreshwa tangu alipokagua mradi huo Desemba 27, mwaka jana. Aliitaka TBA
kwa kushirikiana na Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia
Dodoma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa/Mkurugenzi wa Dodoma wawasimamie wakandarasi na
hasa wale wa Mzinga ili kazi yao ikailike kwa wakati.
“Nimesisitiza katika kila site, zile kazi ndogondogo zisizohitaji
ujuzi au ufundi mkubwa, zigawiwe kwa vijana ili kuongeza kasi lakini tuzingatie
ubora wa kazi,” alisisitiza.
Desemba 27, mwaka jana, Waziri Mkuu alikagua
ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali na kubaini kuwa baadhi ya wakandarasi
hawaendi na kasi inayotarajiwa na Serikali. Siku iliyofuata aliitisha kikao cha
Mawaziri wote, Makatibu Wakuu na wakandarasi wao ili waeleze kazi hiyo
itakamilishwa lini. Kikao hicho alikifanyia hukohuko Ihumwa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.