Tuesday, January 8, 2019

MHAGAMA ARIDHISHWA NA UTENDAJI WA PSSSF SINGIDA

NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama ameridhishwa na utendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa umma wa PSSSF Mkoani Singida katika utoaji wa huduma kwa wanachama wake.
Hayo yamebainishwa wakati wa ziara yake mkoani humu Januari 08, 2019 katika kukagua utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Magufuli aliyoyatoa Desemba 28, 2018 alipokuwa akizungumza na viongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA), viongozi wa vyama vya waajiri, Watendaji wa Wizara inayohusika na Mifuko ya hifadhi ya jamii Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Lengo la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa maagizo hayo ikiwa ni pamoja na; zoezi la uhakiki wa taarifa za wanachama, Kufuatilia masuala ya uwekezaji katika mifuko, kufuatilia namna mifuko ilivyojipanga kubana matumizi pamoja na  kupunguza na kuangalia upya gharama za uendeshaji wa shughuli za mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSF na NSSF nchini.
 “Nimetembelea mifuko hii miwili na kuridhishwa na utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais ikiwa tayari wa wastaafu 89 kati ya 143 wameshaanza kufanyiwa uhakiki tangu utekelezaji wake ulipoanza wiki hii”,alisema Mhagama.
Waziri aliwata watendaji wa mifuko hiyo kuendelea kusimamia na kutekeleza maagizo yote kwa wakati ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuzingatia weredi katika kufikia malengo yanayotarajiwa.
“Hatuta kuwa na msamaha na watendaji wazembe katika kutekeleza maagizo hayo, lazima utekelezaji wake uwe kwa wakati na watakaozembea watachukuliwa hatua za kisheria”,alisisitiza Mhagama.
Waziri alieleza furaha yake kwa upande wa mfuko wa PSSSF kwa kuendelea kuwafikia wanachama kwa wakati na kuonesha mbinu za kuwafikia wanachama wake ikiwa ni utoaji wa taarifa za haraka kupitia simu za mkononi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe.Mhandisi Paskasi Muragili aliwata watendaji wa mifuko kuwa wabunifu katika kuelimisha umma na kuwa wabunifu katika kuongeza wanachama wapya katika mifuko hiyo.
“kuna haja ya kubadili mifumo ya utoaji taarifa kwa umma na jinsi ya kuwafikia wanachama wapya kwa kuwa na programu maalum zitazotoa elimu kwa umma juu ya huduma za mifuko hiyo”,alisisitiza Muragili.
Aliongezea kuwa, mifuko inapaswa kuendelea kujitangaza na kuonesha umuhimu wa mifuko ili kuendelea kuwafikia wanachama wapya na wale wa zamani ili jamii inufaike na uwepo wa mifuko nchini.
Aidha mmoja wa wastaafu Mkoani Singida Bi. Magreth Mfaume aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuhudumia na kujali wastaafu kwa kuwapatia taarifa pamoja na mafao yao kwa wakati.
“tunamshukuru Mhe. Rais kuendelea kutujali kwa kuboresha huduma za wastaafu ikiwa ni utoaji wa mafao yetu kwa wakati na kurejesha nidhamu kwa watendaji wa Serikali wenye weredi wa hali ya juu”.alisisitiza Magreth.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.