*Waziri Mkuu apokea maandamano ya wafanyakazi wakimpongeza Rais
SHIRIKISHO
la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) limeyataka makundi ya wanasiasa
kutowatumia wao kama njia ya kujitafutia umaarufu kwa kuzungumzia
masuala yao na badala yake wawaachie viongozi wa vyama hivyo kwa sababu
wanajitosheleza.
Pia
shirikisho hilo limesema litaendelea kuiunga mkono na kushirikiana na
Serikali ya awamu ya tano pamoja na rais wake Dkt. John Magufuli na
kwamba watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti
ya ajira zao.
Hayo
yamesemwa leo (Jumatatu, Januari 7, 2019) na Katibu Mkuu wa TUCTA,
Yahya Msigwa katika hotuba yake aliyoitoa kwa wafanyakazi baada ya
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupokea maandamano ya amani ya vyama vya
wafanyakazi.
Watumishi
wa taasisi mbalimbali leo wameandamana jijini Dodoma katika viwanja vya
Nyerere Squarekwa lengo la kumpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa uamuzi
wake kufuta kikotoo kipya cha mafao ya wafanyakazi kilichopendekezwa
katika kanuni za sheria ya Mifuko ya jamii.
Katibu
huyo wa TUCTA amesema mara nyingine makundi ya wanasiasa yamekuwa
yakisema maneno ambayo wao hawajayasema jambo ambalo limekuwa
likiwachonganisha na wadau wao wakiwemo wanachama pamoja na Serikali.
”Wafanyakazi
wanaona fahari kwa sababu Rais Dkt. Magufuli anasikiliza kero
mbalimbali zinazowakabili na kuzitatua kwa wakati. Aliposema atafufua
Shirika la Ndege Tanzanzia amelifufua na sasa tuna ndege saba pamoja na
ujenzi wa miradi mkubwa ya umeme, barabara ambayo yote inaenda
kutengeneza ajira.”
Hata
hivyo, ameiomba Serikali ifanye uchunguzi kwenye miradi inayotekelezwa
na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa sababu hawana uhakika kama miradi hiyo
imerejesha fedha. Pia ameiomba Serikali iongeze mishahara kwa watumishi
wa umma.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema Serikali
ipo tayari wakati wote kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wafanyakazi ikiwa
ni pamoja na kuboresha mishahara na maslahi yao. “Wito wa Serikali ni
kuwa wafanyakazi watekeleze majukumu yao kwa uadilifu,weledi na kujituma
ikiwa ndio chachu ya kufikia malengo na ustawi wa nchi yetu.”
Kuhusu
suala la kupandisha mishahara, madaraja na maslahi ya wafanyakazi kwa
ujumla, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli alishalitolea maelekezo
na kwamba Serikali inayafanyia kazi maelekezo yake, hivyo amewaomba
wafanyakazi waendelee kuwa wavumilivu.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kulipa stahili za watumishi wa
umma kwa wakati na kulipa madeni hatua kwa hatua, ambapo kati ya Julai
2018 hadi Septemba 2018, Serikali imelipa sh. bilioni 184.9 za madai
mbalimbali ya watumishi.
“Kati
ya kiasi hicho Serikali imelipa shilingi bilioni 49 kwa ajili ya
malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 28,214 ambayo yanajumuisha
shilingi bilioni 19.2 walizolipwa walimu 16,214. Hata hivyo Serikali
inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi katika wizara na taasisi
mbalimbali ili kupanga vizuri mishahara na motisha kwa watumishi wa
umma.”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.