Wednesday, January 9, 2019

WAZIRI MHAGAMA AWATAKA WATENDAJI KIWANDA CHA VIATU CHA KARANGA KUZALISHA KWA TIJA.



NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama amewataka watendaji wa kiwanda cha Viatu na bidhaa za ngozi cha Karanga Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuendana na Soko lililopo nchini.
Ametoa kauli hiyo alipotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki ili kukagua shughuli za uendeshaji wa kiwanda hicho na kujiridhisha na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
“Niwatake watendaji kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia viwango vinavyotatiwa”, Mhagama
Aidha Waziri aliwaasa watendaji wa kiwanda hicho kuendelea kutatua changamoto zinazowazunguka za kimfumo kwa kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa kiwanda hicho ili kuendana na ukuaji wa teknolojia na ushindani ulipo.
“Nisingependa kuona kiwanda kinakwama kuzalisha bidhaa zenye ubora, hivyo ni vyema kuzingatia sheria na kanuni za uendeshaji wa kiwanda katika ufanisi wa hali ya juu”,alisisitiza mhagama.
Waziri alieleza kuwa, ili kuwa na wateja wa uhakika ni vyema kutumia mbinu za kujitangaza juu ya shughuli na bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia vyombo vya habari ili kuendana na soko lililopo nchini.
Aidha waziri alieleza Mpango mkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Taifa katika eneo hilo la Gereza la Karanga na tayari eneo limetengwa kwa ajili ya ujenzi na kuboresha kiwanda kilichopo ili kuongeza uzalishaji kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Uwekezaji unalenga kuboresha kiwanda cha zamani kutoka kuzalisha pair 150 kwa siku na kuzalisha pair 400 kwa siku ingawa mpango mkakati uliopo ni kuwa na kiwanda kikubwa kitakachozalisha pair 4000 kwa siku”,alisisita Waziri Mhagama.
Naye Kaimu Mkuu wa Kiwanda hicho, Shalua Magandi alibainisha faida zinazotarajiwa kutokana na mradi wa kiwanda hichi ni pamoja na  uzalishaji wa ajira 5000 za moja kwa moja na zaidi ya ajira 4000 kutokana na shughuli za uzalishaji nchini, kuongeza Kodi kwa Manispaa, kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ngozi, kuongeza manufaa kwa mkoa pamoja na mikoa inayozunguka kwa kuboresha mfumo wa maisha na kuongeza kipato kwa wananchi.
Kwa upande wake Afisa masoko wa kiwanda hicho Bw. Fredrick Njoka aliwataka Watanzania kuendelea kununua viatu vinavyotengenezwa kwa bidhaa za ngozi kwa kuzingatia ubora na bei nafuu kwa kuwa kiwanda hicho kinatumia mashine za kisasa kutoa nchini Italia ambao ndiyo wenye ujuzi wa hali ya juu na teknoloji ya kisasa ya utengenezaji wa mashine hizo.
“Wananchi msiogope kututembelea na kununua bidhaa zetu kwa kuzingatia zina ubora wa na bei nafuu, na tunapokea mahitaji ya kila aina kulingana na uhitaji wa wateja wetu”,alisema Njoka
Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba alieleza namna watakavyotekeleza maagizo ya waziri pamoja na kuhakikisha usimamizi mzuri wa shughuli za serikali.
“Nikushukuru kwa ziara yako inatukumbusha kuendelea kusimamia utendaji wenye tija kwa watumishi wa Serikali pamoja kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha bidhaa bora na kulingana na mahitaji ya wateja”, alisema Warioba
Kiwanda cha viatu cha Gereza Kuu Karanga, Moshi kilizinduliwa rasmi Juni 3, 1977 na Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Kambarage Nyerere.Awali kilikuwa na ubia na Mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF ambapo baada ya mabadiliko ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo , kwa sasa kina ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.