*Waziri Mkuu asema kwa mwaka jana wanafunzi 57 walikatishwa masomo
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza viongozi na wazazi wilayani Siha mkoani
Kilimanjaro washirikiane kuhakikisha watu wote waliowapa mimba wanafunzi
wanasakwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Amesema
katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka jana jumla
ya wanafunzi wa kike 57 walikatishwa masomo baada ya kupata mimba na
hadi sasa kesi zilizofunguliwa ni sita tu.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Februari 24, 2019) alipokuwa
akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
uwanja wa Isanja, Sanya Juu wilayani Siha wakati akihitimisha ziara yake
ya kikazi mkoani Kilimanjaro.
“Jambo
hili halipendezi, kesi sita tu ndio zimefikishwa mahakamani.
Hakikisheni wahusika wote waliowapa mimba wanafunzi wanatafutwa popote
walipo, wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria.”
Waziri
Mkuu alisema Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike
lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi
na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.
Watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa
mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa, kumpa ujauzo
na hata ukikutwa naye nyumbani kwako, katika nyumba ya wageni.
“Tukikukuta na binti wa shule katika kona isiyoeleweka tunakukamata na kukuchukulia hatua za kisheria. Ole wenu vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela, sasa tafakari kabla ya kutenda.”
Waziri
Mkuu alisema kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto wa kike ambao
bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto kwenda
kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria.
“Kuna
taarifa nimezipata kuwa baada ya watoto kupewa mimba wazazi au walezi
mnamalizana na wahusika kwa kupeana ng’ombe. Sasa tukikukamata
unamalizana na mtu aliyempa mimba mwanafunzi na wewe tunakufunga.”
Pia
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi wote hususani wa
kike wasome kwa bidii ili watimize ndoto zao na wasikubali kushawishika
kwa sababu watashindwa kuendelea na masomo yao.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.