Saturday, February 16, 2019

VIONGOZI WA CCM KAGUENI MIRADI-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wajumbe wa Halmashauri Kuu za Mkoa na Wilaya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wahakikishe wanakagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye maeneo yao na wajiridhishe kama inalingana na thamani halisi ya kiasi cha fedha kilichotumika.

Amesema iwapo viongozi hao hawataridhishwa na utekelezwaji wa mradi husika wasisite kuchukua hatua kwa kutoa taarifa katika ngazi huzika, lengo ni kuhakikisha miradi yote inakuwa na ubora na inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 16, 2019) wakati akizungumza na viongozi wa CCM, wabunge pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Kigoma kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya CCM ya mkoa wa Kigoma.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mlezi wa CCM mkoa wa Kigoma amesema ni muhimu kwa viongozi hao kujiridhisha na muenendo wa utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yao zikiwemo za afya, maji, elimu na kilimo.

Amesema CCM itaendelea kuimarisha misingi ya utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi, hivyo amewataka viongozi wa CCM pamoja na viongozi wa Serikali washikamane ili malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo yatimie.

“CCM ni chama imara chenye mipango inayotekelezeka na kilicholenga kuwaletea wananchi maendeleo na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili na ndicho chama pekee chenye kuleta matumaini kwa Watanzania wote.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza wanachama na wapenzi wa CCM wasome katiba ya chama na kuzielewa kanuni, taratibu na sera ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Akisisitiza jambo hilo Waziri Mkuu amegawa nakala za katiba ya CCM kwa viongozi hao. 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga alisoma taarifa ya mkoa huo, ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu linaloendelea kwenye mkoa huo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2018 jumla ya wahamiaji haramu zaidi ya 4,135 walikamatwa kwenye msako uliofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.


 (mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.