Na. OWM, DODOMA.
Kampuni ya MNG Group of Companies
ya nchini Uturuki imeonesha nia ya kufanya uwekezaji mkubwa nchini katika sekta
mbalimbali; zikiwemo sekta za Uchukuzi, Utalii, Nishati na Usafiri wa Anga.
Uwekezaji huo umebainishwa
na Mwenyekiti wa Bodi ya MNG Group of Companies, Mehmet Gunal, wakati
alipokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Angellah Kairuki (Mb), jijini Dodoma, tarehe 5
Januari 2019.
Waziri Kairuki amebainisha
kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha uwekezaji wenye tija nchini,
na kwa kutumia mfumo wa sera ya Ushirikiano
baina ya sekta Binafsi na Umma inahakikisha inavutia wawekezaji zaidi nchini.
“Tunazo fursa na miradi
inayohitaji mitaji ya uwekezaji hapa nchini, jukumu letu ni kuhakikisha
wawekezaji mnapata mazingira wezeshi katika fursa na miradi mnayotaka kuwekeza
ili nchi iweze kupata tija kutokana uwekezaji huo” Amesisitiza Mhe. Kairuki.
Akiongea katika kikao
hicho mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya MNG Group of Companies, Mehmet Gunal,
amefafanua kuwa , Kampuni hiyo iko tayari kuwekeza nchini katika Sekta mbalimbali,
kwa kuwa wamevutiwa na mazingira ya uwekezaji ya hapa nchini.
Aidha, Gunal alifafanua
kuwa wamejipanga kutumia fursa na miradi
yenye kuhitaji uwekezaji nchini ili kuweza kufanya uwekezaji mkubwa , pia
alisema kampuni yake ipo tayari kuwekeza hata kwa mfumo wa sera ya ushirikiano
baina ya Sekta ya Binafsi na Umma au kuwekeza wao wenyewe.
Kampuni ya MNG Group of
Companies inao uzoefu katika masuala ya uwekezaji kwa miaka 42 katika mabara
matatu Duniani, ikiwa imejikita katika
uwekezaji kwenye sekta sita na tayari
hadi hivi sasa imetekeleza miradi zaidi ya mia mbili katika mabara hayo.
Baadhi ya Miradi ambayo
imetekelezwa na Kampuni hiyo ni pamoja na , Bwawa la kufua Umeme la Chief Dam
la nchini Algeria, Ujenzi wa uwanja wa
Ndege wa Kimataifa KOTOKA (terminal
III), wa
nchini Ghana, Ujenzi wa makao makuu
ya na Benki ya Halk nchini Uturuki.
Kikao hicho kilihudhuriwa na
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe, Wataalamu
wa masuala ya Uwekezaji na maendeleo ya Sekta Binafsi wa Ofisi
ya Waziri Mkuu, pamoja na wataalam kutoka Kituo cha Uwekezaji nchini.
MWISHO.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe Angellah
Kairuki (Mb) pamoja na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Isack Kamwelwe (Mb), wakiwa katika kikao na wawekezaji
toka nchini Uturuki katika Kampuni ya MNG Group of Companies wakati walipofanya
kikao juu ya fursa na miradi ya uwekezaji nchini leo, tarehe 5 Januari, 2019,
jijini Dodoma.
Wawekezaji toka nchini
Uturuki katika Kampuni ya MNG Group of Companies wakifuatilia kikao na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Angellah Kairuki (hayupo pichani), wakati walipofanya kikao juu
ya fursa na miradi ya uwekezaji nchini leo, tarehe 5 Januari, 2019, jijini
Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji), Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akimkabidhi Kitabu chenye Fursa na Miradi
yenye Uhitaji Mitaji ya Uwekezaji nchini , Mwekezaji toka nchini Uturuki ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya
MNG Group of Companies mara baada ya kufanya kikao juu ya fursa na miradi ya
uwekezaji nchini leo, tarehe 5 Januari, 2019, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.