NA.MWANDISHI WETU
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Kushirikiana na Wadau wa masuala ya Mifugo, Kilimo na Uvuvi wameandaa Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta hizo ili kujadili matokeo ya tafiti zinazohusu sera za kilimo na maboresho ya sera hizo ili kujenga mazingira wezeshi kwa wakulima na sekta binafsi.
Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 mnamo Februari 13, 2019 Jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Kiraiya alipokutana na waandishi wa habari hii leo, Februari 12, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo.
Kongamano hilo linalenga kuchambua namna sekta ya kilimo inavyoweza kuwa msingi na chachu ya mageuzi ya viwanda pamoja na kuainisha mapendekezo ya maeneo ya kisera ambayo yanahitajika kuboreshwa.
Kaulimbiu ya Kongamano hilo kwa mwaka huu 2019 ni “Mchango wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Kuhamasisha Mageuzi ya Uchumi na Viwanda Kupitia ASDP-II”
Aidha, Mgeni rasmi wa kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Akielezea kuwa, kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki kutoka Sekta binafsi, wakulima, wataaluma, wabia wa maendeleo, watafiti na wadau kutoka sekta ya Umma na kuwataka waandishi wa habari kuendelea kulitangaza kongamano hilo kwani linaleta chachu kwa kuzingatia mchango wa wadau katika kuboresha sera za kilimo ili kufikia mageuzi ya viwanda.
“Wito wa Serikali kwa vyombo vya habari ni kuhakikisha mnaendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuboresha sera mbalimbali zinazohusu masuala la kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inahimiza juu ya mchango wa sekta hizo katika kuchochea mageuzi ya viwanda nchini”,alisema Kiraiya.
Naye Mratibu wa Jukwaa la Uchambuzi wa Sera za Kilimo Profesa, David Nyange alieleza umuhimu wa kongamano hilo ambalo litatoa fursa kwa wadau kujadili mada nane ikiwemo; Mazao ya Chakula na Lishe, Mazao ya Biashara, Mazao mapya, bidhaa mbadala na zile zinazoagizwa nje, Mazao ya Mifugo na Samaki pamoja na Pembejeo na huduma za kilimo
“Kongamano hili limekuja wakati sahihi kwani kati ya vipaumbele vya ukuaji wa uchumi, kilimo ndiyo msingi wa ukuaji wa viwanda kwani malighafi zilizotumika viwandani nyingi zinatokana na kilimo, hiyo kongamano hili ni muhimu kwani linatupa kujadili na kuchambua sera za kilimo na nini kifanyike kuwa na kilimo kinachokuwa kwa kasi na kuleta mageuzi ya viwanda,”alisisitiza Prof.Nyange
AWALI
Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu uchambuzi wa Sera linaratibiwa na Jukwaa la Watafiti na wachambuzi wa Sera na Kilimo linalojulikana kama Policy Analysis Group (PAG) ambapo inajumuisha Taasisi zaidi ya 19 ikiwemo; ANSAF, ESRF, REPOA, USAID/ASPIRES (MSU), USAID ENGINE (IESC), AGRA, FSDT, AMDT, EAGC, RESAKSS, FAO/MAFAP, SAGCOT, ACT, DALBERG, TPSF, ILRI NA TAHA.Aidha kundi hilo linashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara za sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinashirikiana katika uratibu. kongamano hilo litafanyika Ukumbi wa mikutano wa Hazina Dodoma kuanzia tarehe 12 hadi 15 Februari, 2019.
Afisa Programu kutoka Eastern Africa Grain Council (EAGC) Bw.Junior Ndesanjo akichangia jambo wakati wa mkutano huo. |
Bi.Tertula Swai kutoka Shirika la AMDT (Agricultural Markets Development Trust) akichangia jambo wakati wa mkutano huo.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.